Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa FAO wa kupunguza upotevu na utupaji wa chakula nchini Thailand wainua kipato cha wafanyabiashara

Mradi wa FAO nchini Thailand wa kupunguza upotevu wa chakula na taka kuna jukumu muhimu katika kubadilisha mifumo ya kilimo na chakula.
© FAO/Alisa Suwanrumpha
Mradi wa FAO nchini Thailand wa kupunguza upotevu wa chakula na taka kuna jukumu muhimu katika kubadilisha mifumo ya kilimo na chakula.

Mradi wa FAO wa kupunguza upotevu na utupaji wa chakula nchini Thailand wainua kipato cha wafanyabiashara

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kupunguza upotevu na utupaji wa chakula kuna jukumu muhimu katika kubadilisha mifumo ya kilimo na chakula. Kati ya malengo 17 ya Maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo yanafikia kilele mwaka 2030 lengo namba 2 linahimiza kutokomeza njaa, lengo namba 8 linahimiza kazi nzuri na ukuaji wa kiuchumi na lengo namba 12 lina himiza utumiaji na uzalishaji wenye kuwajibika lengo likiwa kuwa na mifumo endelevu ya utumiaji wa rasilimali. Malengo yote haya yanaenda sambamba na harakati za kupunguza upotevu na utupaji wa chakula.

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uhamasishaji juu ya Upotevu na utupaji wa Chakula Septemba 29 nchini Thailand shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na kilimo FAO linatekeleza mradi wa kuwapatia ujuzi wafanyabiashara wadogo na wa kati ili waweze kupunguza upotevu na utupaji wa chakula na pia kuongeza thamani ya mazao yao na hatimaye kujipatia kipato zaidi. Tuungane na Evarist Mapesa katika Makala hii akitujuza ziadi kuhusu mradi huo. 

Rais wa chama cha ushirika cha Ban Lao Farmers wives Natakarn Dakawong.
FAO
Rais wa chama cha ushirika cha Ban Lao Farmers wives Natakarn Dakawong.

Wana ushirika wa Ban Lao Farmers Wives

Wafanyabiashara wa kiwanda cha kukoboa na kusaga mchele wa kahawia huko jimboni Sakon Nakhon chini Thailand, walipotembelewa na FAO walikuwa wakiendelea na shughuli ka kukoboa na kusaga mchele lakini Rais wa chama cha ushirika cha Ban Lao Farmers wives Natakarn Dakawong aliwaeleza biashara inaenda mrama. 

“Tukikausha mchele kidogo, mchele utapata ukungu. Na tukikausha mchele kwa muda mrefu basi utavunjika wakati wa kusaga, na kwasababu ya hilo tungepata mchele kidogo.” 

Ili kuwasaidia wafanyabiashara hao FAO chini ya ufadhili wa Japan wakishirikiana na serikali ya Thailand ilianzisha mradi wa kutoa mafunzo ya kusaga na kukoboa kwa kutumia mbinu za kiteknolojia ikiwemo kupima joto kwa kidijitali na tayari kikundi hicho kimefanikiwa kuokoa kilo 450 za mchele walizokuwa wakipoteza kila mwezi kama anavyothibisha Makamu wa Rais wa chama hicho Duangta Dakawong. 

“Tangu kuja kwa mradi huu wametusaidia kutambua hasara na upotevu, wametupa nyezo na kutuwezesha kudhibiti uzalishaji. Wametusaidia kuongeza faida.” 

Pamoja na kuwa biashara ndogo ndogo na za kati huchangia takriban asilimia 91 ya shughuli za usindikaji wa chakula nchini Thailand, suala la upotevu na utupaji wa chakula sio kipaumbele cha juu kwa wafanyabiashara wengi.

Wanawake wakivuna mchele huko Chiang Rai, kaskazini mwa Thailand.
UN Women/Pornvit Visitoran
Wanawake wakivuna mchele huko Chiang Rai, kaskazini mwa Thailand.

Faida za kupunguza upotevu wa chakula

Kwa mujibu wa FAO upotevu wa chakula ni kitendo cha kushuka kwa ubora au kumwagika kwa chakula kabla hakijamfikia muuzaji wa rejareja hali hii huwakumba watu kama wakulima vyakula walivyolima vinapoharibika au wateja wa jumla kutoka mashambani.

Na utupaji wa chakula ni kitendo cha chakula kuharibika kwa mfanya biashara wa rejareja mfano muuza genge ambaye baadhi ya bidhaa zimeharibika kabla ya kuziuza kwa mlaji au kwa mteja wa mwisho mfano mboga za majani ambazo hazikuhifadhiwa vyema zikaharibika hutupwa.  

Afisa Mwandamizi anayehusika na masuala ya upotevu na utupaji wa chakula wa FAO Rose Rolle anasema “mbinu hizo rahisi wanazozitoa katika mradi kama unaotekelezwa nchini Thailand zimewasaidia si tu wazalishaji na wasindikaji kufikia viwango vya kitaifa vya ubora wa mazao bali pia kupunguza upotevu na uharibifu wa chakula, kuboresha ubora wa bidhaa zao, na tuwaongezea mapato.”

Ulimwenguni kote asilimia 13 ya chakula kinachozalishwa hupotea na asilimia 17 huaribika na tatizo hili Bi Rose Rolle amesema linadhihirika kwenye suala la njaa, uhakika wa upatikanaji wa chakula, lishe na mapambano ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Upotevu na utupaji wa chakula huathiri uhakika wa upatikanaji wa chakula kwa mamilioni ya watu ulimwenguni kote kwani hupunguza upatikanaji na ufikiaji wa chakula. Pia ina athari kwa mifumo  uendelevu ya kilimo, kwa sababu jinsi chakula kinavyo haribika kwenye dampo, na pia chakula kinavyosafirishwa kwenye mnyororo mzima wa usambazaji, huzalisha gesi chafuzi.”

Utupaji wa chakula kama unavyodhihirishwa hapa kwenye soko moja nchini Uganda. Hii ni changamoto siyo tu kwa wauzaji wa vyakula bali pia wakulima.
© FAO/Sumy Sadurni
Utupaji wa chakula kama unavyodhihirishwa hapa kwenye soko moja nchini Uganda. Hii ni changamoto siyo tu kwa wauzaji wa vyakula bali pia wakulima.

FAO kupeleka mradi nchi nyingine

Mradi huu wa kuwapa elimu wafanyabiashara wadogo na wa kati umeonesha uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazo athiri mazingira. 

FAO imeeleza kwamba jumla ya makampuni 25 ya Thailand yamenufaika na mradi huo na kupunguza upotevu na utupaji wa chakula. 

FAO sasa inakamilisha mwongozo wa kiufundi kwa lugha nyingi ili kusaidia makampuni katika nchi nyingine kufikia matokeo sawa na waliyoyapata wafanyabiashara wa Thailand.