Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Rohingya wanakabiliwa na njaa na kupoteza matumaini baada ya kupunguzwa tena mgao wa chakula: UNHCR

Mkimbizi wa Rohingya akipokea mgao wa chakula huko Cox's Bazar.
© WFP/Nihab Rahman
Mkimbizi wa Rohingya akipokea mgao wa chakula huko Cox's Bazar.

Wakimbizi wa Rohingya wanakabiliwa na njaa na kupoteza matumaini baada ya kupunguzwa tena mgao wa chakula: UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Katika kambi za Cox's Bazar, nchini Bangladesh wakimbizi wa kabila la Rohingya kutoka nchini Myanmar wanaopata hifadhi kambini hapo wanahisi athari za kupunguzwa kwa mara ya pili kwa mgao wao wa chakula katika muda wa miezi mitatu limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Katika kituo cha usambazaji wa chakula Cox's Bazar, ambako ni nyumbani kwa kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, Amina mwenye umri wa miaka 66 ni miongoni mwa wakimbizi wengi wa Rohingya ambao wanatembea taratibu kupita rafu za chakula cha msaada.

Baada ya kuchanganua safu za dengu, vitunguu saumu, viazi, vitunguu, mayai na mchele, anaanza kulia kwa simanzi kwani ni chupa ndogo tu ya mafuta ya kupikia na mfuko wa pilipili nyekundu ndio vitu pekee anavyoweza kumudu kwa mkopo uliosalia kwenye vocha yake ya kulipia chakula ambayo ni dola 8 tu kwa mwezi.

"Sijui nitafanya nini?, nitaishije kwa hili, pamoja na mchele mdogo ambao nimebakisha kwa muda wote wa mwezi uliobaki? Majirani zangu walikuwa wakinisaidia nilipokosa chakula, lakini sasa nao wanashindwa kuhimili gharama,” anasema huku mikono yake ikitetemeka akiingiza vitu vyake kwenye mfuko mkubwa wa gunia, ambao unaonekana tupu kama vile alipofika.

Kwa mujibu wa UNHCT takriban Warohingya milioni moja wamesalia kukwama katika mazingira yenye msongamano mkubwa wa watu, na wakati mwingine hatari katika kambi hizi kusini mwa Bangladesh, wengi wao baada ya kukimbia ghasia nchini Myanmar karibu miaka sita iliyopita.

Msaada wa chakula wanaopokea kutoka kwa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataida duniani, WFP, umekuwa chanzo pekee cha kutegemewa ambacho wanaweza kukitumia ili kukidhi mahitaji yao ya msingi ya chakula na lishe. 

Lakini tangu kuanza kwa mwaka huu, njia hii ya kuokoa maisha imekuwa chini ya shinikizo kubwa kutokana na kupungua kwa ufadhili kulikosababisha ukata mkubwa.

Mgao wa chakula umepunguzwa hadi dola senti 27 kwa siku

Likikabiliwa na uhaba wa fedha, shirika la WFP limelazimika kufanya maamuzi magumu ili kuendeleza msaada wa chakula hadi mwisho wa mwaka. 

Mwezi Machi, thamani ya vocha za chakula kwa wakazi wa kambi ya Cox’s Bazaar ilipunguzwa kutoka dola 12 kwa kila mtu kwa mwezi hadi dola 10, na mwezi Juni mwaka huu ikapunguzwa tena hadi dola 8 pekee saw ana dola senti 27 kwa siku.

Punguzo hilo limekuja wiki chache baada ya maelfu ya wakimbizi kupoteza makazi yao kutokana na kimbunga Mocha, ambacho kilifuatia moto mkubwa kambini hapo mapema mwaka huu.

"Ilinibidi kupunguza sehemu ya chakula cha watoto wangu lakini kwa muda gani? Hakuna chakula cha kutosha kwa ajili ya familia yangu na kwa kweli sijui tutaishi vipi,” anasema Morjina mwenue umri wa 27, mama asiye na mwenzi na analea watoto watatu.

Mayai hyakipangwa kwa ajili ya kusambazwa kwa wakimbizi katika Cox's Bazar nchini Bangladesh.
© WFP/Nihab Rahman
Mayai hyakipangwa kwa ajili ya kusambazwa kwa wakimbizi katika Cox's Bazar nchini Bangladesh.

Kama mwanamke anaeendesha kaya yake familia yake inapata msaada kutoka kwa WFP ambao umemsaidia wanawake kama yeye wasiojiweza na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu kama wanawake, Watoto, wazee na watu wenye ulemavu kwa vocha za kununua chakula kikiwemo matunda, mbogamboga na ptotini ili kukidhi mahitaji ya lishe bora.

Mbali ya msaada wa chakula hicho cha kila siku WFP pia inatekeleza programu ya lishe kwa kina mama wajawazito na wanaonyonyesha na Watoto walio chini ya umri wa miaka 5.

Licha ya msaada wa ziada kaya zilizo hatarini bado zina haha kuweka mlo mezani na suluhu pekee ya kuzuia hali kuwa mbaya zaidi kwa mujibu wa shirika hilo la wakimbiz “ni kurejesha mgao kamili wa chakula kwa wakimbizi wote wa Rohingya mara moja.”

Dom Scalpelli, mkurugenzi wa WFP nchini Bangladesh amesema "Kupunguzwa kwa mgao ndio suluhisho letu la mwisho. Wafadhili wengi wamejitolea kutupa ufadhili lakini tulichopokea hakitoshi. Ni muhimu sana kuwapa familia za Rohingya msaada kamili wanaostahili. Kadiri tunavyosubiri, ndivyo njaa inavyoongezeka zaidi katika kambi na tayari tunashuhudia watoto zaidi wakiingizwa katika programu za matibabu ya utapiamlo.”

Ufadhili toka kwa wahisani unapungua 

Sio WFP pekee inayohisi ukata kutokana na kushuka kwa viwango vya ufadhili wa wahisani wa kimataifa wakati hali ya wakimbizi wa Rohingya inazidi kuwa ya muda mrefu. 

Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na misaada ya kibinadamu wa mwaka 2023 kwa Warohingya umefadhiliwa kwa robo tu. 

Mashirika zaidi na zaidi ya kibinadamu sasa yanalazimika kuendelea tu na msaada muhimu zaidi, na hiyo inamaanisha kuwa mahitaji ya msingi hayafikiwi. 

Athari za upunguzaji huo wa msaada ni mbaya sana kwa wanawake na watoto, ambao ni zaidi ya asilimia 75 ya idadi ya wakimbizi wote na wanakabiliwa na hatari kubwa ya unyanyasaji, unyonyaji na ukatili wa kijinsia.

“Bila chakula cha kutosha na hakuna njia ya kupata mapato halali, wakimbizi wamechukua hatua zinazozidi kuwakatisha tamaa za kuishi kama vile ndoa za utotoni na ajira ya watoto, na pia kuanza safari hatari za kutumia mashua. Limeonya shirika la UNHCR.

Haja ya fursa zaidi za kujikimu

Kwa mujibu wa UNHCR msaada zaidi utahitajika kutoka kwa jumuiya ya kimataifa ili kuhakikisha kwamba msaada wa kimaisha unatolewa kwa wakimbizi na uwekezaji unafanywa katika jamii zinazowahifadhi.

Kwa muda mrefu, Johannes van der Klaauw, mwakilishi wa UNHCR nchini Bangladesh, anasema njia pekee ya kuzuia hali ya kibinadamu katika kambi isizidi kuzorota ni kwa kuwekeza katika elimu, mafunzo ya ujuzi na fursa za kujikimu kimaisha.

Hii itawaruhusu wakimbizi kujitegemea na kutimiza kwa sehemu kuwa mahitaji yao ya msingi kupitia njia zao na zaidi ya yote, kuwatayarisha kwa ajili ya kujenga upya maisha yao wakati wanaweza kurejea Myanmar kwa hiari na salama."

Bila fursa kama hizo, wakimbizi wa Rohingya kama Morjina wanaona punguzo la hivi karibuni la mgao wa chakula kama sio tu litaongeza njaa zaidi, lakini pia linawaondolewa matumaini.

Mkimbizi huyo anasema "Kwa sasa, hatima yetu haiko mikononi mwetu. Hatuwezi kurejea nyumbani, hatuna uhuru wa kutembea hapa, na njaa ndiyo njia pekee ya kupitisha siku zetu."