Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya kijamii lazima iwe msingi wa mabadiliko ya ulimwengu wa ajira: ILO

Mtaalamu wa mashine wa kukata akifanya kazi katika kiwanda cha nguo huko Lesotho.
© ILO/Marcel Crozet
Mtaalamu wa mashine wa kukata akifanya kazi katika kiwanda cha nguo huko Lesotho.

Haki ya kijamii lazima iwe msingi wa mabadiliko ya ulimwengu wa ajira: ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Haki ya kijamii lazima iwe msingi wa mpito wa kimataifa kuelekea ajira zenye haki na endelevu zaidi kwa wote amesema Katibu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa video kwenye ufunguzi wa mkutano wa dunia wa ajira ulioanza jana Jumatano mjini Geneva Uswis.

Mkutano huo wa siku mbili  unaomalizika leo umeandaliwa na shirika la kazi  la Umoja wa Mataifa duniani ILO ili kufahamisha pendekezo lake la Muungano wa Kimataifa wa Haki za Kijamii, linaolenga kupunguza na kuzuia ukosefu wa usawa.

"Ulimwengu uko katika wakati wa kufanya maamuzi. Sera za leo kuhusu mabadiliko ya tabianchi, vitisho kwa usalama wa kimataifa, juu ya mshikamano wa kijamii na zaidi, zitaunda mustakbali wetu, wa watoto na wajukuu wetu”. Amesema Guterres

Kwa hivyo, Mkutano huo unatoa fursa "kutafuta suluhu ambazo zitafanya mustakabali huo kuwa wa haki zaidi, usawa, endelevu na shirikishi", ameongeza.

Wafanyakazi wanajadili mipango katika tovuti ya ujenzi wa usafiri wa haraka huko Delhi, India.
© ADB/Eric Sales
Wafanyakazi wanajadili mipango katika tovuti ya ujenzi wa usafiri wa haraka huko Delhi, India.

Ujumbe wa viongozi wa kimataifa

Leo katika siku ya pili na ya mwisho ya mkutano huo viongozi mbalimbali wa kimataifa wamepata fursa ya kuzungumza wakiwemo Rais wa Madagascar Andry Rajoelina, Raisi wa Jamhuri ya Kenya William Samoei Ruto na Mia Amor Mottley Waziri mkuu wa Barbados.

Hao ni miongoni mwa viongozi 17 wa nchi na serikali wanaozungumza kwenye mkutano huo wa ngazi ya juu utakaomalizika leo 15 Juni, chini ya kaulimbiu ya “Haki ya Kijamii kwa Wote”.

Andry Rajoelina, Rais wa Madagaska akizungumza kwenye mkutano huo amesema, "Hakuwezi kuwa na haki ya kijamii bila kuwa na fursa kwa kila mtu," akisisitiza kwamba "Upatikanaji wa huduma za afya, upatikanaji wa elimu, upatikanaji wa mafunzo, upatikanaji wa chakula, na pia upatikanaji wa ajira. Kwa sababu ajira ndio msingi wa jamii yenye haki na usawa.”

Pia amesema, “Vita dhidi ya ukosefu wa usawa kazini lazima iendeshwe kwa ushirikiano mkubwa wa kimataifa.”

Rais huyo wa Madagascar ametoa wito wa "uhamasishaji wa kimataifa kusaidia juhudi za kufufua ukuaji endelevu. Ni wajibu wetu kuonyesha mshikamano ili kuhakikisha kwamba haki ya kijamii inatimia, na kwamba kazi zenye staha ni haki inayopatikana kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”

Mjadala wa Kaskazini dhidi ya Kusini ufungwe

Kwa upande wake Rais wa Kenya Willian Samoei Ruto amesema "Ni msimamo wangu kwamba tunapaswa kuacha mazungumzo yasiyo na maana kuhusu mvutano wa Kaskazini dhidi ya Kusini."

Amefafanua, kwa kusema "Kaskazini kuna shida kama ilivyo Kusini linapokuja suala la mabadiliko ya tabianchi. Na tunapaswa kuwa na mazungumzo tofauti. Mazungumzo ambayo yatatupa matokeo ya ushindi wa wote."

Rais Ruto ameongeza kuwa “Ili haki ya kijamii kwa wote itafsiriwe katika mabadiliko ya maana ya hali ya ajira, na kwa ajili ya mkutano wa kilele wa ulimwengu wa kazi kueleza kikamilifu matarajio ya maeneo bunge yanayowakilishwa hapa, inabidi kuwekeza haraka katika njia kabambe za kuwapata mamilioni ya watu wasio na ajira, hasa katika Ukanda wa Kusini, kufanya kazi, na kuchukua hatua za kijasiri za kitaasisi ili kuunda kwa makususudi fursa kwao.”

Winnie Kakunta, msimamizi wa uendelezaji wa kampuni ndogo za kati katika Idara ya uhusiano wa jamii ya kampuni ya madini ya Barrick. Kampuni hii imeshirikiana na idara ya ajira bora nchini Zambia kujenga makazi kwa ajili ya wakazi na wafanyakazi wake.
ILO/Crozet M.
Winnie Kakunta, msimamizi wa uendelezaji wa kampuni ndogo za kati katika Idara ya uhusiano wa jamii ya kampuni ya madini ya Barrick. Kampuni hii imeshirikiana na idara ya ajira bora nchini Zambia kujenga makazi kwa ajili ya wakazi na wafanyakazi wake.

Kunatofauti kubwa kati ya Kusini na kaskazini

Mia Amor Mottley, waziri mkuu wa Barbados amesema, "Kuna tofauti ya wazi katika ulimwengu huu kati ya Kaskazini na Kusini ndani ya nchi zetu na katika mipaka yote. Na ni juu yetu kuweza kutambua kuwa kila mtu anastahili utu na hadhi ambayo inaelekea kuwa ndani ya mwanadamu.”

Pia amesema, "Ninaunga mkono muungano wa kimataifa wa haki za kijamii. Kuna utambuzi wa kina kwamba kufanya ulimwengu huu kuwa mahali pazuri zaidi, hakuna mada moja, au shirika moja, au hakuna kiongozi anayeweza kuruhusu kutokea peke yake. Ili kuifanya dunia yetu kuwa mahali pazuri na penye haki tunahitaji muungano wa watu walio tayari kufanya kazi pamoja.”

Washiriki wengine wanajumuisha wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka Umoja wa Mataifa, mashirika mengine ya kimataifa, na mashirika ya waajiri na wafanyakazi.

Washiriki wamekuwa wakijadili sera na hatua zinazoweza kuendeleza haki ya kijamii na kuangazia jukumu muhimu la haki ya kijamii katika kuunda ulimwengu endelevu na wenye usawa.