Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti: Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa UN aonya dhidi ya 'mzunguko usioisha wa vurugu'

Watu wakitembea katika wilaya ya Turgeau, mojawapo ya vitongoji vya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, vilivyoathiriwa zaidi na ghasia za magenge.
© UNICEF/U.S. CDC/Roger LeMoyne
Watu wakitembea katika wilaya ya Turgeau, mojawapo ya vitongoji vya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, vilivyoathiriwa zaidi na ghasia za magenge.

Haiti: Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa UN aonya dhidi ya 'mzunguko usioisha wa vurugu'

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk Jumanne ya leo ameonya dhidi ya "mzunguko usio na mwisho wa ghasia" nchini Haiti huku magenge yakiendelea kuwatendea watu ukatili wa kupindukia, na magenge kujichukulia sheria mkononi. 

"Kila ripoti ninayopata kutoka Haiti inasisitiza ukubwa wa mateso, na hiyo inatuma ujumbe kuwa Wahaiti wanahitaji msaada wa haraka, na wanauhitaji sasa," Türk amesema hii leo mjini Geneva, Uswisi. 

"Ninasisitiza wito wangu kwa jumuiya ya kimataifa kupeleka kikosi cha usaidizi kinachoendana na wakati, maalumu na kinachotii haki za binadamu, chenye mpango wa utekelezaji wa kina wa kusaidia taasisi za Haiti," ameongeza. 

Katika mwezi wa Aprili pekee, zaidi ya watu 600 waliuawa katika wimbi jipya la ghasia kali zilizokumba wilaya kadhaa katika mji mkuu, kulingana na taarifa zilizokusanywa na Huduma ya Haki za Kibinadamu ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti (BINUH). Hii inafuatia mauaji ya watu wasiopungua 846 katika miezi mitatu ya kwanza ya 2023, pamoja na 393 waliojeruhiwa na 395 kutekwa nyara katika kipindi hicho - ongezeko la asilimia 28 la ghasia katika robo ya awali. 

Ikiwa imezidiwa na ukosefu wa usalama unaoongezeka kila mara, Haiti inashuhudia ongezeko la kutisha la mauaji ya kundi la watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa genge, huku takriban mauaji 164 kati ya haya yakirekodiwa mwezi Aprili. 

"Ni wajibu wa Serikali kulinda raia wake. Watu wanapaswa kuwa na uwezo wa kutegemea polisi na mamlaka ya mahakama ili kukabiliana na vurugu za magenge. Lakini ukweli ni kwamba Serikali haina uwezo wa kujibu. Kwa hivyo watu wanajichukulia sheria mkononi - lakini hii itachochea tu kuongezeka kwa vurugu," ameongeza Türk. 

Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa na BINUH leo zimezindua taarifa yao ya robo mwaka (Januari hadi Machi), ambalo linaangazia kuibuka kwa vikundi vya wahalifu, kufuatia wito wa baadhi ya viongozi wa kisiasa na waandishi wa habari kuwataka raia kuunda mashirika ya kujilinda ili kupambana na ghasia za magenge. 

Ripoti hiyo pia inasisitiza kwamba ghasia sio tu zinazidi kukithiri na mara kwa mara lakini zinaenea bila kuchoka huku magenge yakijaribu kupanua udhibiti wao. Maeneo ya mji mkuu hapo awali yalizingatiwa kuwa salama, hasa Kenscoff na Pétion Ville, pamoja na idara ya Artibonite, sasa yameathiriwa. 

Miongoni mwa njia nyinginezo zinazotumiwa na magenge, ripoti hiyo inabainisha matukio ya wavamizi kuwafyatulia risasi watu kiholela barabarani au kuwafyatulia risasi majumbani, na watu kuchomwa moto wakiwa hai kwenye usafiri wa umma. 

Aidha Türk amesema "Hatupaswi kusahau kwamba umaskini uliokithiri na ukosefu wa huduma za kimsingi ndio chanzo cha vurugu za sasa na nguvu ya magenge juu ya jamii. Serikali, kwa kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, inapaswa kufanya kila iwezalo kutekeleza wajibu wake kuwapa watu upatikanaji wa mara kwa mara na usiozuiliwa wa maji safi, chakula, afya na makazi.”  

"Dharura ya sasa ya haki za binadamu inataka majibu madhubuti – haraka." Ameongeza.