Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zimepigwa katika vita dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wenye VVU:WHO

Msichana mdogo akipokea chanjo yake ya kwanza ya HPV kumkinga na saratani ya shingo ya kizazi  nchini Mauritania
© UNICEF/Raphael Pouget
Msichana mdogo akipokea chanjo yake ya kwanza ya HPV kumkinga na saratani ya shingo ya kizazi nchini Mauritania

Hatua zimepigwa katika vita dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wenye VVU:WHO

Afya

Ikiwa ni miaka miwili tangu kuzindiliwa mkakati wa kimataifa wa kusongesha hatua za kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi na kuweka taarifa za hatari ya kupata saratani hiyo kwa wanawake wanaoishi na virusi vya ukimwi VVU, shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO linasema kuna hatua zilizopigwa katika nyanja zote. 

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo amabyo ni siku ya kuchukua hatua kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi, WHO imesema mwaka 2021 makadirio yanaonyesha kwamba wanawake zaidi ya milioni 1.9 wanaoishi na VVU wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi katika nchi 19. 

Na katika kuchukua hatua kutokana na mwongozo mpya wa WHO kuhusu upimaji na matibabu ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi nchi 53 ama zimefanyia marekebisho sera zake kujumuisha mapendekezo ya WHO au zinapanga kufanya hivyo katika miaka 3 ijayo. 

Wahudumu wa afya ni kiungo muhimu katika kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi
Pan American Health Organization
Wahudumu wa afya ni kiungo muhimu katika kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi

Mradi wa kutokomeza saratani umewahamasisha wadau 

Kwa mujibu wa Dkt. Meg Doherty, mkurugenzi wa programu za WHO za VVU, homa ya Ini na Magonjwa ya zinaa STIs "Mpango wa kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi umehamasisha nchi, washirika, watekelezaji, wafadhili, na asasi za kiraia kuharakisha upatikanaji na matumizi ya kinga na matibabu ya saratani ya mlango wa kizazi. Ni juhudi za kweli za kimataifa na matokeo katika miaka hii michache ni ya kuvutia. Ahadi hii ya kuokoa maisha ya wanawake lazima iendelee.” 

Ameongeza kuwa pamoja na hatua zilizopigwa bado kuna mengi zaidi ya kufanya. WHO inasema matokeo yaliyochapishwa leo kuhusu athari za VVU kwenye saratani ya shingo ya kizazi nchini Afrika Kusini yanaonyesha kuwa “utokomezaji wa saratani ya shingo ya kizazi inawezekana hata katika mazingira ya mzigo mkubwa wa VVU.” 

 Tathimini tatu huru zimetabiri kupungua kwa kiwango kikubwa kwa matukio ya saratani ya shingo ya kizazi ynayoendana na umri baada ya mkakati wa wa chanjo wa WHO wa kutokomeza saratani, upimsji wa mara mbili ktika maisha kubaini kuhusu saratani ya shingo ya kizazi na matibabu.  

Takriban thuluthi moja ya visa vya saratani ya shingo ya kizazi miongoni mwa wanawake kwa ujumla na wanawake wanaoishi na VVU vilizuiliwa katika kipindi cha miaka 25 ya kwanza. 

Wanafunzi wawili wa shule ya msingi nchini Rwanda wakipatiwa chanjo dhidi ya virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi, HPV.
© UNICEF/UN0261446/Rusanganwa
Wanafunzi wawili wa shule ya msingi nchini Rwanda wakipatiwa chanjo dhidi ya virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi, HPV.

Bado ni mtihani miongoni mwa wenye VVU 

Shirika la WHO limesma kufikia kutokomeza kabisa saratani ya shingo ya kizazi miongoni mwa wanawake wanaoishi na VVU itakuwa changamoto zaidi.  

Licha ya kufikia punguzo la zaidi ya asilimia 85% katika matukio ya saratani ya shingo ya kizazi, kizingiti cha kutokomeza visa vya saratani katika kiwango cha chini cha watu 4 kwa kila wanawake 100 000 kilifikiwa tu wakati wanawake wanaoishi na VVU walipochunguzwa mara kwa mara (kila baada ya miaka 3). 

WHO imesisitiza kuwa kupanua huduma ya chanjo salama na yenye ufanisi ya papillomavirus ya binadamu inayokwenda sanjari na na uchunguzi wa mara kwa mara kwa wanawake wanaoishi na VVU, kama inavyopendekezwa katika mwongozo wa WHO wa uchunguzi na matibabu ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi, itakuwa muhimu.