Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR washtushwa na ongezeko la wakimbizi wa ndani Magharibi wa DRC

Mwanamume mkimbizi wa ndani akiwa amepumzika katika makazi ya jamii huko Bandundu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC
© UNHCR/Simon Lubuku
Mwanamume mkimbizi wa ndani akiwa amepumzika katika makazi ya jamii huko Bandundu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC

UNHCR washtushwa na ongezeko la wakimbizi wa ndani Magharibi wa DRC

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umeshtushwa na ongezeko kubwa la wakimbizi wa ndani huko magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo DRC baada ya kuibuka kwa mapigano mapya ya wenyewe kwa wenyewe mwezi Julai huko Kwamouth.

Taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR hii leo kutoka Geneva Uswisi imesema watu 142 wameuwawa katika mapigano hayo ambayo chanzo chake ni kodi ya ardhi kwa ajili ya kilimo.

UNHCR imeeleza kuwa hadi kufikia Oktoba sita mwaka huuu, zaidi ya watu elfu 27 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wamekimbilia kusaka hifadhi katika majimbo ya Kwilu na Mai Ndombe huku wengine zaidi ya 2,600 wakivuka mto congo kusaka hifadhi katika nchi jirani ya Jamhuri ya Congo.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa UNHCR nchini DRC Angele Dikongue-Atangana mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha wakati watu wakijaribu kukimbia machafuko ziliwafanya wengi kushindwa kutumia njia zenye usalama na pia usafirishaji wa misaada ya kibinadamu nao umekuwa washida kwakuwa magari yanashindwa kufikisha msaada wa kuokoa maisha.

Mwakilishi huyo pia anaeleza familia zimesalia kuwa na kiwewe kutokana na mapigano ya ghafla na makali yaliyozuka katika maeneo yao.

“Waliambia timu zetu kwamba walikimbia kuokoa maisha yao na walikimbilia msituni na walizunguka wakiwa na watoto wao. Wengi wameacha mashamba yao na kuacha mavuno yao kwenye maghala. Waliokimbia makazi yao wanaendelea kuhisi hatari kwa sababu kuishi kwao kunategemea nia njema ya wengine na pia kusaidiwa na jamii za wenyeji na mamlaka za maeneo hayo.”

 

Hali ya usalama Kwamouth bado ni tete

Mji wa Kwamouth na vijiji kadhaa vinavyozunguka kwa sasa vimetelekezwa.

Familia nyingi ambazo zilikuwa zikiishi Kwamouth na vijiji vinavyozunguka zimeondoka eneo hilo kwani mzozo ulikuwa ukienea haraka.

Watu walitembea kwa siku kadhaa kabla ya kufikia eneo lenye usalama huko Bandundu, mji mkuu wa Jimbo la Kwilu ambao upo kilomita 245 kutoka mji wa Kwamouth.

UNHCR imeelezaa kwa ujumla hali ya usalama bado ni ya wasiwasi  na kwamba serikali ya DRC imefanya mazungumzo na viongozi wa eneo hilo ili kupeleka jeshi la DR Congo huko Kwamouth kurejesha utulivu.

Eneo la Kambi ya wakimbizi wa ndani la Kalunga, lililoko kilomita chache kutoka kituo cha Kalemie, limewahifadhi takriban watu 10,000 waliokimbia makazi yao kutokana na ghasia kati ya jamii katika jimbo la Tanganyika.
© UNOCHA/Endurance Lum Nji

Wenyeji wema

Jamii za Bandundu zilizowapokea wakimbizi zimekuwa zikionesha ukarimu kwa wananchi waliokimbia machafuko huku mifano ikitolewa na viongozi wao wa vijiji.

Mfano mmoja ni familia iliyopokea watu 28 akiwemo mwanamke aliyekuwa mjamzito ambaye muda mfupi baada ya kupokelewa alipelekwa katika Hospitali ya Bandundu kujifungua ambapo alijifungua kwa upasuaji.

Familia nyingine iliyotembelewa na UNHCR ilikutwa imewahifadhi watu 77 na wote wakitegemea choo kimoja.

Kiujumla mazingira ya walikopokelewa ni magumu huku wengi wakikaribia kuishiwa kuishiwa mahitaji muhimu ambapo familia nyingine zimeanza kujibana kwa kupata mlo mmoja kwa siku.

 

Misaada kwa wa wakimbizi

Pamoja na kuwa viongozi wa serikali katika maeneo ya Mai Ndombe na Kwilu wameanzisha kamati maalum zinazoshughulikia mahitaji, UNHCR nao kwa kaushirikiana na wadau wao wameongeza usaidizi

“UNHCR inatuma turubai kwa ajili ya kwenda kujengfa makazi ya muda kwa wakimbizi huko Bandundu na iko tayari kusaidia mahitaji mengine ya kipaumbele kama makazi, vifaa vya nyumbani na ulinzi.” Alisema Dikongue-Atangana.

UNHCR pia inashirikiana na serikali za mitaa katika uandikishaji wa wale wanaowasili katika maeneo hayo.

Katika Jamhuri ya Kongo, jumuiya na mamlaka za mitaa zimekaribisha waomba hifadhi wanaowasili. UNHCR inaunga mkono mamlaka katika mpaka, ikiwa ni pamoja na kusajili wapya wanaowasili na kutoa usaidizi.

Hata hivyo UNHCR imetoa ombi kwa jumuiya za kimataif kusaidia katika kumaliza mzozo huko kwamouth ili kuondoa mateso kwa wakimbizi.

Mpaka sasa nchi hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa mahitaji kwa ajili ya wakimbizi  na wakimbizi wa ndani ambapo takwimu zinaonesha wakimbizi wamefikia 521,000 huku wakimbizi wa ndani wakiwa ni zaidi ya milioni 5.5 na ufadhili ni chini ya asilimia 40 kwa kiwango kilichoombwa ambacho ni dola milioni 225.4.


TAGS: UNHCR, DRC, Wakimbizi, Wakimbizi wa ndani, mizozo, msaada wa kibinadamu, machafuko