Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pfizer yahitaji -70℃, AstraZeneca 2 °C hadi 8 °C sasa ipi inafaa wapi na kwa nini?

Ram Dawadi, mhudumu wa afya katika kituo cha afya huko Gorkha nchini Nepal akiwa amebeba chanjo za COVID-19 aina ya AstraZeneca akipeleka ili wahudumu wa afya wapatiwe dozi ya pili.
© UNICEF/Prasad Ngakhusi
Ram Dawadi, mhudumu wa afya katika kituo cha afya huko Gorkha nchini Nepal akiwa amebeba chanjo za COVID-19 aina ya AstraZeneca akipeleka ili wahudumu wa afya wapatiwe dozi ya pili.

Pfizer yahitaji -70℃, AstraZeneca 2 °C hadi 8 °C sasa ipi inafaa wapi na kwa nini?

Afya

Ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 ulitangazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kuwa janga la afya ya umma duniani tarehe 30 mwezi Januari mwaka 2020.

 

 

Chanjo ya COVID-19 aina ya Pfizer/BioNTech ni ya kwanza kuanza kutumika katika baadhi ya nchi duniani.
BioNTech
Chanjo ya COVID-19 aina ya Pfizer/BioNTech ni ya kwanza kuanza kutumika katika baadhi ya nchi duniani.

Ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi WHO mpaka sasa imeshaidhinisha aina 6 za kwa ajili ya matumizi ya dharura ya chanjo dhidi ya coronavirus">COVID-19.

Chanjo hizo ni Pfizer/BioNTech, AstraZeneca/Oxford moja ikitengenezwa na Korea Kusini na ile inayotengenezwa na taasisi ya Serum nchini India, Moderna, Johnson & Johnson, Sinovac na Sinopharm. Chanjo hizo ni miongoni mwa chanjo zaidi ya 200 ambazo ziko kwenye utafiti ili kukabili Corona. 

Chanjo ya AstraZeneca/Oxford dhidi ya COVID-19 inatengenezwa nchini India chini ya leseni maalum.
© UNICEF/Dhiraj Singh
Chanjo ya AstraZeneca/Oxford dhidi ya COVID-19 inatengenezwa nchini India chini ya leseni maalum.

Ubaridi wa kuhifadhi chanjo unatofautiana

Mwongozo wa WHO unaonesha kuwa kila chanjo iliyoidhinishwa kwa matumizi ya dharura ina masharti yake hasa katika uhifadhi na utumiaji ili iweze kuwa na ufanisi. Mathalani Pfizer inahitaji ubaridi wa nyuzi joto hasi 70 katika kipimo cha selsiyasi (-70℃). Halikadhalika lazima chanjo iwe imeganda, na iwapo itayeyuka na kuganda tena basi ufanisi wake  unapungua. Kiwango hicho cha ubaridi cha uhifadhi ni changamoto kwa nchi nyingi za kipato cha chini na kati ambazo hazina miundombinu ya majokofu ya kuhifadhi na kusambaza chanjo.

Majokofu yenye baridi kali yanayotumiwa na Rwanda kuhifadhi chanjo ya COVID-19 aina ya Pfizer/BioNTech. Hapa ni katika kituo cha serikali ya Rwanda cha kuhifadhi chanjo kilichoko mjini Kigali. Rwanda ni miongoni mwa nchi zilizopokea chanjo ya Pfizer/BioNT
UNICEF/Andy Rugema
Majokofu yenye baridi kali yanayotumiwa na Rwanda kuhifadhi chanjo ya COVID-19 aina ya Pfizer/BioNTech. Hapa ni katika kituo cha serikali ya Rwanda cha kuhifadhi chanjo kilichoko mjini Kigali. Rwanda ni miongoni mwa nchi zilizopokea chanjo ya Pfizer/BioNTech kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa COVAX.

AstraZeneca kwa upande wake inahitaji ubaridi wa kati ya nyuzi joto 2 hadi 8 katika kipimo cha selsiyasi ( +2 °C hadi 8 °C,) kiwango ambacho ni sawa na chanjo za kawaida ambazo hutolewa katika nchi za kipato cha chini na kati. Na chanjo hizi hazihitajiki kuwa zimeganda barafu wakati anapatiwa mhusika.

Wataalamu wanasema kuwa chanjo kama Pfizer na Moderna zinazotumia teknolojia ya kuchochea seli ya mwili kuzalisha protini ili kuongeza kinga ya mwili dhidi ya virusi na hivyo zikipata joto au baridi kupitiliza zinaharibika na kama ilivyo kwa samaki, chanjo iliyoharibika lazima itupwe na WHO haitaki hata dozi moja ya chanjo itupwe. Hivyo lazima nchi kuzingatia mifumo na masharti ya uhifadhi wa kila chanjo.

Chanjo zaidi zinaendelea kutengenezwa na zinafanyiwa utafiti kabla ya kuidhinishwa na WHO. Miongoni mwao ni hii ya Sputnik V kutoka Urusi.
RDIF/Stas Zalesov-Nakashidze
Chanjo zaidi zinaendelea kutengenezwa na zinafanyiwa utafiti kabla ya kuidhinishwa na WHO. Miongoni mwao ni hii ya Sputnik V kutoka Urusi.

Matumizi yako vipi?

Kwa chanjo ya Pfizer, iwapo haijachanganywa na imehifadhiwa katika nyuzi joto hasi 90 hadi hasi 60 (-90 °C hadi -60 °C) inaweza kutunzwa kwa miezi 6 tangu itengenezwe. Lakini ikiwa kwenye nyuzi joto 2 hadi 8 inaweza kutumika ndani ya siku 5 tu,na joto likipanda zaidi na kuwa nyuzi joto 30 inapaswa iwe imetumika ndani ya saa 2. Na iwapo itachanganywa na iko katika nyuzi joto 2 hadi 30 basi lazima itumike ndani ya saa 6.

Kwa upande wa AstraZeneca kichupa cha chanjo ambacho hakijafunguliwa na kimehifadhiwa katika nyuzi joto kati ya 2 hadi 8 (2 °C hadi 8 °C ) kinaweza kutumika hadi miezi 6. Kile ambacho kimeshafunguliwa lakini kiko katika ubaridi wa kati ya nyuzijoto 2 hadi 25 katika kipimo cha selsiyasi (2 °C hadi 25 °) kinaweza kutumika ndani ya saa 6 tu.

Muhudumu wa afya akimchanja mtu wa pili kupata chanjo ya COVID-19 nchini Angola kwa mfumo wa COVAX.
© UNICEF/COVAX/Carlos César
Muhudumu wa afya akimchanja mtu wa pili kupata chanjo ya COVID-19 nchini Angola kwa mfumo wa COVAX.

Kwa nini chanjo hizo zimeorodheshwa kwa matumizi ya dharura?

WHO inasema ni kwa kuzingatia mazingira ya janga la Corona, chanjo zinaweza zisiwe zimekidhi vigezo vya awali vya kuidhinishwa moja kwa moja, na hivyo basi jopo linazipitia na kuidhinisha ziwe kwenye orodha ya matumizi ya dharura ili kuchagiza mchakato wa upatikanaji wake na matumizi ya dawa ambazo bado hazijapatiwa leseni lakini zinahitajika katika dharura ya kitabibu ili kulinda afya ya umma.

Nchi za Afrika zilizochukua Pfizer

Mwezi Februari mwaka huu kampuni ya Pfizer-BioNTech iliridhia mataifa manne ya Afrika ambayo ni Cabo Verde, Rwanda, Afrika Kusini na Tunisia kupokea chanjo yake ya Pfizer. Kwa mujibu wa WHO kanda ya Afrika, Katika kuwasilisha ombi za chanjo hiyo ya Pfizer, nchi zilitakiwa kuwasilisha maombi ambapo nchi 13 ziliwasilisha na maombi yao kufanyiwa tathmini ikiwemo kiwango cha cha vifo kutokana na COVID-19 na uwezo wa kuhifadhi chanjo hizo katika joto la -70°C.

Mhudumu wa afya akikagua kiwango cha ubaridi katika bohari ya serikali ya kuhifadhi chanjo huko New Delhi nchini India.
© UNICEF/Amarjeet Singh
Mhudumu wa afya akikagua kiwango cha ubaridi katika bohari ya serikali ya kuhifadhi chanjo huko New Delhi nchini India.

Wito wa WHO kwa nchi zinazochukua chanjo

Nchi lazima ziwe na mkakati wa kitaifa wa utoaji wa chanjo na wakati huo huo mkakati huo ujumuishe uimarishaji wa mnyororo wa kupokea, kuhifadhi na kusambaza chanjo hizo na usimamizi wake n ahata vifaa vinavyotakiwa kama mabomba ya sindano, majokofu na makasha ya kutupia sindano zilizotumika. Usambazaji huo ufikie hadi maeneo ya ndani kabisa ya nchi ili kila mtu anayehitaji kupata chanjo apatiwe.