Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu yaendelea wakati tsunami ya COVID-19 ikighubika India

Programu ya utoaji chanjo kubwa kabisa duniani ilipoanza India Januari 2021.
© UNICEF/Ruhani Kaur
Programu ya utoaji chanjo kubwa kabisa duniani ilipoanza India Januari 2021.

Hofu yaendelea wakati tsunami ya COVID-19 ikighubika India

Afya

Mfanyikazi wa Umoja wa Mataifa nchini India ameelezea kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa maambukizi ya virusi vya corona au COVID-19 ambako ni nchini mwaka katika siku za hivi karibuni kama ni "tsunami", na amezungumzia "hofu" aliyohisi, wakati familia yake ya karibu ilipoambukizwa virusi hivyo. 

Idadi ya maambukizo mapya nchini India inaongezeka zaidi ya wagonjwa 300,000 kwa siku na zaidi ya 200,000 wamekufa kutokana na maambukizo, ingawa wengi huko wanaamini idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi. 

Anshu Sharma, anafanya kazi katika idhaa za Kihindi ya  UN News na ameelezea hisia hizi binafsi kutoka katika kituo chake cha kazi huko New Delhi, akiangazia kuishi katika kivuli cha janga hilo. 

“Kuna hali ya mshikamano na nimesikia hadithi nyingi za huruma zinazohusisha marafiki, majirani na wageni.”-Anshu 

"Wakati coronavirus">COVID-19 ilipoanza kuenea nchini India mnamo Machi 2020, hakuna mtu aliyeelewa uzito wa janga hilo, lakini leo, zaidi ya mwaka mmoja baadaye janga hilo limechukua sura mbaya kutuathiri sisi sote, ikiwemo familia yangu mwenyewe.” 

Ameendelea kusema kama mwandishi wa Habari wa Umoja wa Mataifa, nilianza kama mtazamaji aliyejitenga akifuatilia athari za COVID-19 kote Asia Kusini. Lakini hali hiyo ilibadilika wakati mmoja wa wanafamilia yangu alipokufa kutokana na kucheleweshwa kwa matibabu kulikosababishwa na huduma za afya kulemewa na kutanda kwa hofu kwenye mifumo ya huduma za afya. Ilikuwa wakati wa kusikitisha sana na wa huzuni kwa familia yangu wakati tulipofarijiana tulipokuwa katika amri za kusalia majumbani. 

Na wakati huo binamu yangu alikuwa amekwama nchini Nigeria, tulikuwa tunajaribu kumrejesha nyumbani kwa miezi kadhaa na mnamo Julai tulifanikiwa na ghafla tulikuwa na mwangaza wa matumaini kati kati ya kiza hicho totoro. 

Anshu Sharma wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa ya Kihindi kabla ya janga la Corona akiwa makao makuu New York.
UN News
Anshu Sharma wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa ya Kihindi kabla ya janga la Corona akiwa makao makuu New York.

 

Kwa hakika majaribu yalikuwa bado yaja 

Anshu anasema alianza na kujitenga hotelini kwa siku 14, kama sheria, lakini alipata homa na alikimbizwa hospitalini. Kabla ya madaktari kumpima na kugundua hali yake, alikufa kwa sababu ya viungo vingi vya mwili kushindwa kufanyakazi.  

Tulifahamu baadaye kwamba alikuwa amekufa kutokana na malaria. Ingawa sio moja kwa moja, kwa mara nyingine tena, virusi vya corona vilikuwa vimemnyakua mshiriki mwingine wa familia yangu. 

Hata hivyo nyakati za majaribu zilikuwa bado zaja. Miezi michache baadaye, mnamo Septemba, nilienda kumtembelea mama yangu mzee na kaka katika mji mwingine na licha ya kuchukua tahadhari zote iwezekanavyo hofu yangu mbaya zaidi ilitimia; sisi sote tulipimwa na kukutwa na virusi vya COVID-19 na kwa wiki mbili tulikuwa tukipambana na maambukizi ya kutisha ya gonjwa hilo. 

Nikiwa na hofu ya mabaya zaidi kutokea katika kipindi hiki, nilikuwa nikiamka usiku kuangalia kila mtu. Kila siku nilihisi kama ni mapambano na nilipata wasiwasi mwingi. Kitulizopekee ni kwamba sote tulipona tukiwa nyumbani katika  karantini na hakuna hata mmoja wetu aliyelazimika kulazwa hospitalini. 

Mchezo mbaya wa akili 

Sasa naweza kusema kuwa kutokana na hali ya sintofahamu na kutokuwa na uhakika, COVID-19 ilicheza na akili yangu, zaidi ya athari za kimwili, afya, ni mchezo mbaya wa akili! 

Tahadhari bado zilikuwa zinazingatiwa kwa kiwango kikubwa, lakini watu walikuwa wameanza kupata uzembe. Hii ilikuwa ni utulivu kabla ya dhoruba! 

“Kipindi hiki kimebadilisha kabisa mtazamo wangu na sasa ninaelewa thamani halisi ya maisha. Ni muhimu kuishi maisha kwa ukamilifu na kutumia wakati na wapendwa wako.” 

Kuelekea mwisho wa 2020, wagonjwa wa COVID-19 walianza kupungua na ilionekana kana kwamba India ilikuwa imelishinda janga hilo.  

Na wakati ulimwengu ulikuwa ukiipongeza India kwa ushindi wake juu ya virusi, nchi ilikuwa ikijiandaa kuanza kampeni kubwa zaidi ya chanjo duniani. 

Ilionekana kana kwamba mwisho wa janga ulikuwa umekaribia na maisha yalikuwa yakirudi katika hali ya kawaida. Masoko na maduka makubwa yalifunguliwa na yalikuwa yakijaa pilika. 

Tahadhari zilikuwa bado zinachukuliwa na kuzingatiwa kwa kiasi kikubwa , lakini watu walianza kuzembea. Na huu ulikuwa ni utulivu tu kabla ya dhoruba kubwa. 

Utoaji chanjo nchini India.
WHO India
Utoaji chanjo nchini India.

Wimbi la pili la maambukizi 

Na kisha likaja wimbi la pili la COVID-19, ambalo lilimshangaza kila mtu. 

Idadi ya maambukizi ilianza kuongezeka, kutoka elfu chache kwa siku, hadi zaidi ya 300,000, tsunami ya COVID-19 ilikuwa ikienea kote nchini.  

Na kisha watu wengine watatu wa familia yangu ya karibu walipata virusi, na moyo wangu ulizama katika hofu. 

Nilipitia mihemko isiyoelezeka. Mwanzoni, nilikuwa na hasira na mimi mwenyewe kwa kukutupilia mbali tahadhari niliyoichukua awali na kutojilinda zaidi.  

Nilikabiliwa na kutokuwa na uwezo wowote juu ya virusi hivyo na nilikuwa na wasiwasi wa kutaka kujua ikiwa kingamwili kutoka kwa maambukizo yangu ya zamani zingenilinda dhidi ya kuambukizwa tena? 

Ujumbe wa rambirambi 

Leo, majimbo na miji mingi nchini India iko chini ya amri ya kutotoka nje na wafanyikazi wa afya wanafanya kazi mchana na usiku kuzuia kuenea zaidi kwa maambukizi wakati vyombo vikuu vya Habari na mitandao ya kijamii, inaongozwa na hadithi mbaya za majonzi ya COVID-19.  

Mikono na moyo wangu umechoka kuandika ujumbe wa pole. Mfumo wa huduma za afya umelemewa.  

Maombi ya kutaka dawa, vitanda vya wodi za magonjwa mahututi ICU hospitalini, mitungi ya hewa ya oksijeni na sindano, yako kila mahali kwenye mitandao ya kijamii. Janga hili limeifanya nchi hii ya watu bilioni 1.3 kuungama. 

 

Miongoni mwa juhudu kudhibiti Corona ni vikwazo vinavyowekwa.
Sandeep Datta
Miongoni mwa juhudu kudhibiti Corona ni vikwazo vinavyowekwa.

Hadithi za huruma 

Mapambano yangu ya kibinafsi na COVID-19 yanaonekana hayana maana ikilinganishwa na yale ambayo wenzangu wanapitia, lakini kuna mazuri yaliyojitokeza. 

Hapo awali, wagonjwa wa COVID-19 walichukuliwa kama wasioweza kuguswa na jamii iliwaepuka. Lakini sasa, watu wanasaidiana. 

Kuna hali ya mshikamano na nimesikia hadithi nyingi za kutia huruma zinazohusisha marafiki, majirani na wageni 

Majirani wanasaidiana, wenye maduka wanapeleka bidhaa kwa wale wanaohitaji, sehemu za ibada zinabadilishwa kuwa vituo vya kutengwa wagonjwa ili kukidhi uhaba wa vitanda vya hospitali, na kumbi za jamii zinakusanya pesa na kupanga mitungi ya kujaza oksijeni. 

Wimbi la kwanza lilitenganisha wapendwa, na ingawa la pili limewaleta watu pamoja, hakuna nyumba hata moja huko India ambapo COVID-19 haijatia kivuli chake cha machungu na masikitiko. 

Kama watu binafsi na kama nchi, bado tunatafuta mwangaza wa taa mwishoni mwa handaki hili.