Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugonjwa wa PPR waua mamilioni ya kondoo, mbuzi na maisha ya wafugaji

Nchini Niger kondoo zinakabiliwa na hatari ya ugonjwa wa PPR
©FAO/Andrew Esiebo
Nchini Niger kondoo zinakabiliwa na hatari ya ugonjwa wa PPR

Ugonjwa wa PPR waua mamilioni ya kondoo, mbuzi na maisha ya wafugaji

Ukuaji wa Kiuchumi

Zaidi ya nchi 45 leo zimesisitiza ahadi yao ya kutokomeza ugonjwa wa PPR au tauni inayokatili Wanyama wengi wadogo kama mbuzi na kondoo ifikapo mwaka 2030. Kwamujibu wa shirika la chakula na kilimo FAO na lile la kimataifa la afya ya mifugo OIE, wakizungumza katika mkutano uliomalizika leo mjini Roma Italia, ugonjwa huo wa kuambukiza unaua mamilioni ya mbuzi na kondoo kila mwaka .

Inakadiriwa kuwa familia milioni 300 zinazotegemea ufugaji wa wanyama kama chanzo cha chakula na mapato, wako hatarini kupoteza riziki zao na kulazimishwa kuhama kwenye maeneo yaliyo na migogoro, au uhaba wa chakula na rasilimali. Utokomezaji wa ugonjwa huu ni lazima upewe kipaumbele kama tunataka kuhakikisha kuwa mapato na mali za familia hizi zinalindwa ili waweze kuwa na masiha bora yenye afya.

Programu ya kutoa chanjo dhidi ya PPR katika kauti ya Samburu nchini Kenya mnamo Septemba 2017
©FAO/Luis Tato
Programu ya kutoa chanjo dhidi ya PPR katika kauti ya Samburu nchini Kenya mnamo Septemba 2017

Mambo mtano unavyopaswa kujua kuhusu ugonjwa huu:

Mosi, inakadiriwa kuwa kuna wanyama bilioni mbili wanaocheua duniani. Ugonjwa huu wa tauni unaweza kuambukiza hadi asilimia 80 ya wanyama wanaocheua duniani endapo hautodhibitiwa. Utokomezaji wa ugonjwa huu ni muhimu katika jitihada za kukomesha umaskini na njaa duniani. Unaweza pia kudhibiti uhamiaji wa familia nzima.

 Pili, ugonjwa wa PPR umeenea kwa kasi kubwa kwa miaka 15 sasa. Zaidi ya nchi 70 zimeripoti ugonjwa huu tangu ugunduliwe kwa mara ya kwanza nchini Ivory Coast miaka ya 1940. Nchi zilizopo Afrika, Mashariki ya Kati, Asia na nchi nyingine mbalimbali, ziko hatarini endapo ugonjwa huu hautodhibitiwa na kusababisha hasara na adha kwa baadhi ya wakazi waishio maeneo duni.

 Tatu, gonjwa huu pia husababisha athari mbaya kiuchumi. Inakadiriwa kuwa PPR husababisha hasara za zaidi dola bilioni 2 kwa mwaka. Utokomezaji wa ugonjwa huu unawezakana kwa ajili ya kuhifadhi msingi wa mapato na vyanzo vya chakula kwa mamilioni wa wafugaji wadogowadogo wanaotegemea kondoo na mbuzi kwa mapato na kulisha familia zao. Ukomeshaji wa PPR unaweza kuimarisha usalama na uwezeshaji wa wanawake sababu mara nyingi huwajibika kuangalia mifugo.

Nne, Chakula kinachotokana na kondoo na mbuzi ni muhimu katika mlo wa kila siku kwa watu waishio vijijini, na ni muhimu katika udhibiti wa utapiamlo. Maziwa ya kondoo na mbuzi yana virutubisho muhimu haswa kwa lishe ya watoto. Ukomeshaji wa ugonjwa huu unaweza kuongeza usalama wa chakula na lishe bora kwa mamilioni ya watu duniani.

 

Kaunti ya Samburu nchini Kenya, mfugaji akisubiri mbuzi wake wachanjwe dhidi ya PPR.
©FAO/Luis Tato
Kaunti ya Samburu nchini Kenya, mfugaji akisubiri mbuzi wake wachanjwe dhidi ya PPR.

Tano, utokomezaji wa ugonjwa wa tauni unawezekana ifikapo mwaka 2030. Chanjo ya gharama nafuu ambayo hutoa kinga ya maisha ipo. Mpango wa miaka mitano wa kudhibiti virusi kwa njia ya chanjo ipo. Uwekezaji wa haraka unahitajika kwa ajili ya kupambana na PPR, ili kuokoa riziki za watu wanaoishi katika mazingira duni wanaotegemea kondoo na mbuzi.

FAO na Shirika la Afya ya mifugo duniani (OIE), zinafanya kazi pamoja kuhamasisha jumuiya ya kimataifa, haswa kuzingatia nchi zilizoathirika Afrika, Mashariki ya Kati na Asia.  Ushirikiano wa FAO na OIE umeonyesha mafanikio makubwa katika ukomeshaji wa ugonjwa wa Rinderpest, ungojwa wa mifugo unaofanana na PPR. Tukifanya kazi pamoja, tunaweza kukomesha ugonjwa wa tauni unaoathiri mbuzi na kondoo ifikapo mwaka 2030.