Bima ya afya ni muarobaini wa afya kwa wote- Dkt. Maro
Upatikanaji wa bima ya afya kwa kila mtu ni suala mtambuka ambalo Umoja wa Mataifa na mashirika yake , wameendelea kulipigua chepuo ili ifikapo mwaka 2030 kila mtu bila kujali rika, uwezo au rangi yake ana uwezo wa kununua bima ya afya. Utekelezaji wa hoja hiyo unaenda sambamba na mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya afya popote pale alipo, UHC au Universal Health Coverage.