Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na wadau 11 wasio wa kiserikali kushirikiana kuendeleza huduma za afya Tanzania

Kampeni ya ya kitaifa ya chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi nchini Tanzania uliambatana na wanawake na wanaume kubeba mabango yenye ujumbe kuhusu usalama wa chanjo hiyo, ikiongozwa na wadau wa huduma za afya nchini humo.
WHO
Kampeni ya ya kitaifa ya chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi nchini Tanzania uliambatana na wanawake na wanaume kubeba mabango yenye ujumbe kuhusu usalama wa chanjo hiyo, ikiongozwa na wadau wa huduma za afya nchini humo.

WHO na wadau 11 wasio wa kiserikali kushirikiana kuendeleza huduma za afya Tanzania

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO jana limetia saini mkataba wa miaka 2 wa maelewano MoU, na wahusika kumi na moja wasio wa kiserikali ili kuendeleza huduma za afya na kuharakisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote nchini Tanzania

Mashirika hayo 11 wadau ni pamoja na Chuo Kikuu cha Elimu cha Dar es Salaam DUCE, Catholic Relief Services, Madaktari kutoka Afrika-CUAMM, Sikika na Chuo Kikuu cha Mzumbe, Tanzania Health Summit, Wakifu wa kitabibu wa Afrika AMREF, Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), wakfu wa Raising-Up Friendship RUFFO na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Akizungumza wakati wa utiaji saini huo, Dkt Charles Sagoe-Moses Mwakilishi wa WHO nchini Tanzania amesema, “Kupitia makubaliano hayo ya ushirikiano, WHO inalenga kuimarisha ushirikiano na watendaji wasio wa serikali nchini Tanzania”. 

Amebainisha kuwa ushirikiano huo utaiwezesha Tanzania kutumia utaalamu, rasilimali, na mitandao ya mashirika hayo ili kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoikabili nchi.

Ameongeza kuwa “Utiaji saini wa MOU umefanyika lakini kazi inaanza sasa. Kwa kufanya kazi kwa pamoja, nina imani kuwa tunaweza kupata matokeo makubwa zaidi na kupiga hatua kubwa katika kuboresha afya na ustawi wa watu wa Tanzania.”

Makubalianoni hatua kubwa kwa Tanzania

WHO inasema utiaji saini wa makubaliano hayo umekuwa wa muhimu katika kuanzisha hatua kubwa za kiafya nchini Tanzania, ambapo jukumu muhimu la ushirikiano kwa ajili ya afya kwa ujumla kwa ajenda zote haliwezi kusisitizwa zaidi ya hapo. 

Hivi sasa, kuna idadi kadhaa ya watendaji wasio wa serikali wanaosaidia sekta ya afya na hii inahitaji uratibu madhubuti ili kukuza utawala bora, uwajibikaji na uwazi wa mwonekano wa mashirika yasiyo ya kiserikali au NGOs na kuimarisha uhamasishaji wa rasilimali, ramani ya rasilimali na ufuatiliaji wa rasilimali limeongeza shirika hilo la afya duniani.

Waliohudhuria utiaji saini huo ni pamoja na Meneja wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Umma kutoka Wizara ya Afya, Ambele Mwakilango, Mwenyekiti wa Kikundi cha Washirika wa Maendeleo (DPG H), Bwana. Matthew Cogan na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCONGO) Rachel Chagonja. 

Jukumu muhimu la NGOs

Kwa pamoja wamesisitiza jukumu muhimu ambalo NGOs zinafanya katika kutoa huduma za afya. 

Na zaidi amebainisha umuhimu wa ushirikiano huu kama ni kitu kitakachoongeza  utaalamu, rasilimali, na mitandao ya mashirika kwa dhamira ya pamoja ya kuimarisha mifumo ya afya na kushughulikia changamoto za afya zinazokabili nchi.

“Tunaamini NSA-H iliyopata fursa hii ya kutia saini makubaliano na WHO itaendelea kuwenda sanjari na vipaumbele vya sekta ya afya. Ninataka kuzihimiza NSAs zetu zilizofaulu kufikia jamii zetu na kushirikiana na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali ili kupata matokeo ya juu katika mfumo wetu wa afya.”, Amesema Bwana Ambele Mwakilango, meneja wa Maabara ya Kitaifa ya Afya ya Umma.

Washirika hao 11 waishukuru WHO

Wadau hao 11 wametoa shukrani zao kwa WHO kwa kuanzisha mpango huu na ushirikiano huu na kuthibitisha fursa yao kubwa ya kuwa sehemu ya kikundi cha watendaji wasio wa serikali ili kuendeleza huduma za afya katika jamii.

Kwao, "huu sio tu ushuhuda wa maono na shauku yao ya kuona afya kwa ajenda zote ikifikiwa lakini pia kutumia ushirikiano huu kutabadilisha maisha ya watu wengi, kukuza upatikanaji wa huduma za afya na kuboresha ustawi wa jumla wa watu nchini Tanzania"  kwa mujibu wa Profesa Apolinary Kamuhabwa Makamu Mkuu wa MUHAS.

Kutiwa saini kwa MOU na wahusika 11 wasio wa serikali ulikuwa mchakato wa mwisho kufuatia kauli ya nia iliyozinduliwa mwezi Desemba 2022 kwenye Magazeti ya Kitaifa. 

Kati ya mawasilisho 46, mawasilisho 11 yalichaguliwa baada ya sehemu ya mchakato mkali na mchakato wa FENSA kwa kila mdau ulifanywa kama ilivyoagizwa na Baraza la Afya Ulimwenguni mwaka 2016.