Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madagascar: Uratibu, mshikamano na mabadiliko kuanzia chini hadi juu

Upatikanaji wa maji ni kipaumbele miongoni mwa idadi kubwa ya watu wa vijijini Kusini mwa Madagascar
UN News/Daniel Dickinson
Upatikanaji wa maji ni kipaumbele miongoni mwa idadi kubwa ya watu wa vijijini Kusini mwa Madagascar

Madagascar: Uratibu, mshikamano na mabadiliko kuanzia chini hadi juu

Tabianchi na mazingira

Je, ni jinsi gani watu wanaweza kusaidiwa ipasavyo wakati wa migogoro ya kibinadamu kukiwa na bajeti ndogo ya misaada? Na je, ni jambo gani linaloweza kufanywa ili kuwasaidia watu hao kuuacha utegemezi wa mara kwa mara unaosababishwa na migogoro na kuyafanikisha zaidi maendeleo endelevu?

Haya ni maswali yanayozingatiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyo nchini Madagaska taifa hilo la kisiwa linapopambana na mabadiliko ya tabianchi, mahitaji makubwa ya kibinadamu, na ukosefu wa maendeleo.

Naibu Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa l kuhudumia watoto UNICEF, na Msimamizi wa Miradi Gilles Chevalier na Natasha van Rijn Mwakilishi Mkazi wa Miradi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP wanajadili jinsi mabadiliko ya utendakazi wao yanavyosaidia kuimarisha uthabiti na maendeleo endelevu.

Gilles Chevalier: Moja ya maamuzi makubwa tuliyoyafanya katika shirika la UNICEF ni kuimarisha uwepo wa wafanyakazi wetu kusini mwa Madagaska ambalo ni eneo lililoathiriwa na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi na athari za El Nino. 

Watu katika sehemu hii ya nchi wamo hatarini sana, wengi wao wanakumbwa na utapiamlo na ukosefu wa huduma za msingi, hivyo kuna mahitaji mengi ya kibinadamu.

Naibu mwakilishi wa UNICEF, Mkuu wa programu Gilles Chevalier (Kushoto) akiwa na Mwakilishi mkazi wa UNDP (Kulia) Natasha van Rijn nchini adagascar
UN Madagascar
Naibu mwakilishi wa UNICEF, Mkuu wa programu Gilles Chevalier (Kushoto) akiwa na Mwakilishi mkazi wa UNDP (Kulia) Natasha van Rijn nchini adagascar

Kuna idadi kubwa ya mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ambayo yanashirikiana ili kuchangia juhudi za misaada katika eneo la Grand Sud. Mashirika hayo pia yanatafuta njia za kuzuia na kupunguza athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo hayo ya kusini kimfumo.

Natasha van Rijn: Viashiria vya maendeleo ya maeneo ya kusini, kwa mfano, vya afya, elimu, lishe, miundombinu na usambazaji wa nishati, vyote ni dhaifu zaidi ukilinganisha na sehemu nyingine za kisiwa, na hilo ni jambo muhimu sana sio tu katika mipango na mazungumzo yanayopaswa kufanyika bali pia katika hatua za dharura za kibinadamu zinazoendelea kwa sasa.

Umoja wa Mataifa hushiriki katika shughuli za kibinadamu na za maendeleo. Mojawapo ya njia ya kuzitofautisha ni kufikiria kazi za kibinadamu kama kushughulikia dalili za ugonjwa katika hali ya dharura, ilihali kazi za maendeleo zinalenga afya na ustawi kwa kushughulikia masuala ya miundo msingi ambayo huenda hatimaye yakasababisha mgogoro wa kibinadamu.

Gilles Chevalier: Kwa kadri tunavyoweza, tunajaribu kuepuka kufanya kazi kwa viwango vidogo katika maeneo kadhaa tofauti. Badala yake, tunatafuta ni vipi tunaweza kuchanganya kazi za Umoja wa Mataifa na washirika wake. Tumeteua maeneo tunayoyaita  ya makutano kulingana na hatari za aina mbalimbali zinazopatikana katika wilaya mbalimbali.

Natasha van Rijn: Kuwekeza kwa kiasi kikubwa zaidi katika eneo moja la kijiografia kumeweza kuunda mazingira ambayo wengine wanaweza kunufaika na uwekezaji unaofanyika.

Mwanamke akifanyiwa vipimo katika ckliniki tembezi  inayousaidiwa na Umoja wa Mataifa Kusini mwa Madagascar
UN News/Daniel Dickinson
Mwanamke akifanyiwa vipimo katika ckliniki tembezi inayousaidiwa na Umoja wa Mataifa Kusini mwa Madagascar

Katika maeneo haya ya makutano, na kwa ujumla kama kanuni, ni muhimu sana kusisitiza kwamba watendaji wa kimaendeleo na kibinadamu wanafanya kazi kwa ushirikiano. Kila mmoja analeta ujuzi na maarifa tofauti kulingana na suala iwe ni uzoefu wa muda mrefu na washirika wa kitaifa au namna ya kuchukua hatua za dharura mgogoro unapozuka.

Bila shaka, ni muhimu pia kutambua jukumu la washirika wa kitaifa, serikali, sekta binafsi, asasi za kijamii au jamii kwani ni uti wa mgongo wa kazi ya haki za misaada ya kibinadamu na maendeleo.

Gilles Chevalier: Tumeona tayari mabadiliko makubwa kabisa namna washirika walivyobadilisha mwelekeo kuhusu jinsi wanavyofanya miradi katika maeneo ya makutano. Washirika wengi hawazingatii tu juhudi za kuhifadhi maisha, bali zaidi wanazingatia ujenzi wa uthabiti. Tunafurahi kuona kwamba washirika wafadhili wanachangia kiasi kikubwa zaidi cha fedha wakiwa na malengo ya muda mrefu, wakitambua umuhimu wa matokeo mazuri na endelevu. Hili linawezekana tu ikiwa mifumo inaimarishwa kwa ngazi ya kienyeji na suluhu zinazingatia muktadha wa kijamii.

Madagascar UN inaweka kipaumbele katika misaada yake katika maeneo yaliyo hatarini zaidi
UN News/Daniel Dickinson
Madagascar UN inaweka kipaumbele katika misaada yake katika maeneo yaliyo hatarini zaidi

Natasha van Rijn: Tunaliita hili ujumuishwaji wa kibinadamu na maendeleo. Ujumuishwaji huu unahusu kuunganisha juhudi za kukabiliana na hatari, kuzuia hasara za maendeleo, na kujenga uthabiti katikati ya mgogoro. Amani ni mtazamo wa tatu wa ujumuishwaji huu pamoja na maendeleo na kutimiza mahitaji ya kibinadamu. Hakuna moja kati ya haya linaloweza kufikiwa bila lingine.

Mfano mzuri wa hili ni Hazina ya Ujenzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa huko Betroka, wilaya ya Anosy katika eneo la Grand Sud la Madagaska , eneo ambalo lilikumbwa na ukosefu wa usalama kutokana na wizi wa mifugo. Kazi ya Hazina hii huko ilichangia katika kustawisha hali ya eneo hilo na kuruhusu mashirika ya kibinadamu kutoa misaada kwa usalama zaidi na kwa watendaji wa kimaendeleo kuanza majadiliano na mamlaka ya maeneo hayo kuhusu masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na utawala wa kienyeji, ulinzi na kukuza shughuli za kiuchumi.

Gilles Chevalier: Ni muhimu kwa Madagaska kuzidi kuangaziwa siyo tu kwa washirika wetu wa kiserikali, bali pia kwa wafadhili. Kimataifa, Madagaska  haikupewa kipaumbele kwa muda mrefu, lakini sasa inatambulika kama moja ya nchi zilizoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi duniani. Kwa hivyo, Madagascar imejitambulisha vyema kwenye ramani katika miaka ya hivi karibuni.

Natasha van Rijn: Tukijikita kutazama hali nchini Madagascar kwa kina, basi tunapata nafasi ya kukabiliana na mahitaji yake yote kwa kuzingatia muktadha na utata katika sekta mbalimbali. Kwa bahati mbaya, njia za kawaida za ufadhili mara nyingi hazifai daima kwa hilo kwani zinalenga kwenye uingiliaji wa kibinadamu au maendeleo au ujenzi wa amani.

Hii ndio sababu jukumu la kuratibu la Umoja wa Mataifa, na haswa Ofisi ya Mratibu Mkaazi, ina umuhimu kama kutumia nyanja ya njia jumuishi kwa sababu inawakutanisha washirika wote pamoja kujadili njia bora zaidi ya kuchangia katika utulivu na ustawi wa muda mrefu wa Madagascar.