Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jopo huru la uchunguzi latoa ripoti ya mwisho kuhusu UNRWA

Timu za UNRWA zinaendelea kutoa huduma za matibabu katika vituo vinane vya afya na makazi ya muda huko Gaza.
© UNRWA
Timu za UNRWA zinaendelea kutoa huduma za matibabu katika vituo vinane vya afya na makazi ya muda huko Gaza.

Jopo huru la uchunguzi latoa ripoti ya mwisho kuhusu UNRWA

Msaada wa Kibinadamu

Jopo huru limetoa ripoti yake iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu leo Jumatatu Aprili 22 kuhusu Shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), likitoa mapendekezo 50 na kubainisha kuwa mamlaka za Israel bado hazijatoa uthibitisho wa madai yao kwamba wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanahusika na mashirika ya kigaidi.

Ripoti ya Mwisho, inayoongozwa na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ufaransa Catherine Colonna, ilipaswa kutolewa baadaye Jumatatu; Bi. Colonna pia alikuwa anajitayarisha kuzungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliopangwa kufanyika saa sita mchana mjini New York kama Mwenyekiti wa Kundi Huru la Mapitio kuhusu UNRWA.

Kikundi huru cha uhakiki kiliwasilisha matokeo ya ripoti ya muda na mapendekezo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wiki nne zilizopita. Hizi ni pamoja na ushahidi kwamba UNRWA ilikuwa na "idadi kubwa ya mbinu na taratibu za kuhakikisha ufuasi wa kanuni ya kibinadamu ya kutoegemea upande wowote", ingawa "maeneo muhimu ... bado yanahitaji kushughulikiwa," ofisi ya Bw. Guterres ilibainisha wakati huo.

Jopo la mapitio - likifanya kazi na mashirika ya utafiti yanayoheshimiwa Taasisi ya Raoul Wallenberg, Chr. Taasisi ya Michelsen na Taasisi ya Denmark ya Haki za Kibinadamu - ilitangaza kwamba itaendelea na kuandaa mapendekezo madhubuti na ya kweli ili kuimarisha na kuboresha wakala.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito hii leo wa "kuunga mkono kikamilifu" shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia wakimbizi wa kipalestina, UNWRA, akiongeza kuwa alikubali matokeo ya mwisho ya uchunguzi huru kuhusu shirika hilo, ulioanzishwa lengo likiwa ni kujibu madai ambayo hayajathibitishwa kwamba wafanyakazi wa UNRWA walishiriki katika mashambulizi yaliyofanyika 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israeli.

"Katibu Mkuu anakubali mapendekezo yaliyomo katika ripoti ya Bi. Colonna," Msemaji wa Bw. Guterres alisema katika taarifa yake," Amekubaliana na Kamishna Mkuu wa (UNRWA) Philippe Lazzarini kwamba UNRWA - kwa msaada wa Katibu Mkuu - itaanzisha mpango wa utekelezaji wa mapendekezo yaliyomo katika Ripoti ya Mwisho."

Ghasia za Gaza, Ukingo wa Magharibi hazijasitishwa

Haya yanajiri huku kukiwa na ripoti za mashambulizi zaidi ya Israel kote Gaza mwishoni mwa juma na kuongezeka kwa viwango vya vurugu katika Ukingo wa Magharibi.

Huko Rafah, mji wa kusini kabisa katika Ukanda wa Gaza, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi, UNFPA, lilmeripoti  hii leo kwamba mtoto mchanga aliokolewa na kufanyiwa upasuaji wa dharura baada ya mama yake kujeruhiwa vibaya katika shambulio la anga na baadaye kufariki.

"Madaktari huko Gaza waliweza kuokoa maisha ya mtoto kutoka tumboni mwa mama yake aliyefariki kutokana na jeraha la kichwa alilokuwa amepata," alisema Dominic Allen, Mwakilishi wa UNFPA kwa Palestina. Mama huyo alikuwa na ujauzito wa wiki 30 alipofariki, pamoja na mume wake na ndugu wa mtoto huyo, Bw. Allen alibainisha.

Kusubiri kwa mabomu kuanguka

Huko Geneva, Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya afya ameangazia adha kubwa ya afya ya akili ambayo miezi ya hivi karibuni na miongo kadhaa ya ghasia imewakumba wakazi waliozingirwa pamoja na wataalamu wa matibabu.

"Fikiria kuishi chini ya kutazamia mara kwa mara bomu au bunduki, au kupigwa risasi unapojaribu kupata chakula au maji au kucheza. Hiyo yenyewe ni aina ya vurugu,” alisema Dk Tlaleng Mofokeng. "Kutarajia kwamba maisha yako yanaweza kuzimwa wakati wowote na kwa watoto kukua na kiwango hicho cha kiwewe sio kawaida. Lakini kwa miongo kadhaa, hilo limekuwa la kawaida kwa watu wa eneo linalokaliwa kwa mabavu la Palestina.

Kila siku maisha yanaendelea kuwa mabaya kwa wakazi wa kawaida wa Gaza baada ya takriban miezi saba ya mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel na operesheni ya ardhini, iliyoanzishwa kujibu mashambulizi ya kigaidi yanayoongozwa na Hamas kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya watu 1,200 na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka.

Mtoto hufariki dunia kila baada ya dakika 10 katika eneo hilo, UNRWA ilisema mwishoni mwa juma, katika wito mpya wa kukomesha ghasia na kuruhusu misaada ya kibinadamu inayohitajika sana kuingia ndani ya eneo hilo.

Hadi sasa, mamlaka ya afya ya Gaza inaripoti kuwa zaidi ya Wapalestina 34,000 wameuawa na wengine 77,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7,2023.

Ikisisitiza hatari za kiafya zinazokuja kutokana na hali ya joto ya majira ya kuchipua, UNRWA ilionesha wasiwasi mpya juu ya usimamizi mbaya wa taka na magonjwa. Katika chapisho kwenye mtandano wa kijamii wa X, zamani Twitter, Scott Anderson, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya UNRWA huko Gaza, alionya kwamba uhaba wa maji na usafi wa mazingira viko chini sana ya kile ambacho idadi ya watu walihitaji ili kuwa na afya njema.