Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miezi sita ya vita Gaza kumekuwa na mashambulizi zaidi ya 700 ya Israel Ukingo wa Magharibi: OCHA

Kituo cha ukaguzi Hebron kwenye Ukingo wa Magharibi
© UNICEF/Ahed Izhiman
Kituo cha ukaguzi Hebron kwenye Ukingo wa Magharibi

Miezi sita ya vita Gaza kumekuwa na mashambulizi zaidi ya 700 ya Israel Ukingo wa Magharibi: OCHA

Amani na Usalama

Katika kuelekea miezi sita tangu kuanza mapigano mapya Ukanda wa Gaza Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya mashambulizi 700 ya Israel dhidi ya Wapalestina yamerekodiwa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, katika kipindi cha takriban miezi sita iliyopita.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, kumekuwa na wastani wa mashambulizi manne ya ya Israel dhidi ya Wapalestina katika kipindi cha miezi sita tangu shambulio la umwagaji damu la Hamas la lililofanyika Oktoba 7 mwaka jana kusini mwa Israel na Israel kuamua kulipiza kisasi dhidi ya Gaza. 

Kwa jumla, OCHA imerekodi mashambulizi 704 ya Israel dhidi ya Wapalestina, kulingana na takiwmu zilizorekodiwa kuanzia Oktoba 7, 2023 na hadi Aprili 1, 2024.

Mashambulizi haya yamesababisha vifo katika matukio 69, uharibifu wa mali ya Wapalestina katika matukio 558, na uharibifu wa mali na majeruhi katika matukio77.

"Kwa jumla, Wapalestina 17 waliuawa na zaidi ya 400 kujeruhiwa katika muktadha huu, zaidi ya miti 9,900 imeharibiwa na nyumba 40 kusambaratishwa," OCHA imeripoti. 

Kwa kulinganisha, takriban matukio 560 yanayohusisha Israel yaliorodheshwa kati ya Oktoba 7, 2022 na Aprili 1, 2023.

Askari wa Israel wakishika doria Jerusalem Mashariki
UN News/Shirin Yaseen
Askari wa Israel wakishika doria Jerusalem Mashariki

Wapalestina 428 waliuawa na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi

OCHA inasema tangu Oktoba 7 na hadi Aprili 1, Wapalestina 428, wakiwemo watoto 110, wameuawa na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, wakiwemo watu 131 tangu kuanza kwa mwaka 2024.

"Katika matukio matatu tofauti karibu na eneo la Khallet el Louza la Bethlehem kati ya Machi 30 na Aprili 1, walowezi waliingia katika ardhi ya Palestina na kuharibu milango, paneli za sola na matangi ya maji katika matukio mengine ikiwa ni pamoja na vyoo na milango ya nyumba pamoja na kamera za uchunguzi katika tukio la tatu tatu”.

Hati hiyo inaonyesha kuwa kati ya Machi 26 na Aprili 1, vikosi vya Israeli vilifanya angalau operesheni 155 katika Ukingo wa Magharibi, haswa shughuli za kusaka na kukamata watu. 

Nyingi zilifanyika katika eneo la Hebroni ambako pekee kulikuwa na operesheni 46, ikifuatiwa na mikoa ya Yerusalemu na Bethlehemu ambako kulikuwa na operesheni 37 kila moja.

Usafi ukiendelea katika kambi ya Nur Shams Ukingo wa Magharibi kufuatia operesheni za Israel
© UNRWA/Mohammed Alsharif
Usafi ukiendelea katika kambi ya Nur Shams Ukingo wa Magharibi kufuatia operesheni za Israel

Wapalestina 1,244 wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia za walowezi

Wakati huo huo, shirika la OCHA linasema vikosi vya Israeli vimefanya, tangu Oktoba 7, 2023, wastani wa operesheni 690 kwa mwezi. 

Katika kipindi hicho, vikosi vya usalama vya Israel viliwashikilia zaidi ya Wapalestina 6,000 na kusababisha uharibifu mkubwa kwa miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na barabara, mifumo ya maji na mitandao ya usafi wa mazingira, nyumba za makazi, miundo ya maisha na bidhaa nyingine za umma.

Kutokana na hali hiyo, zaidi ya Wapalestina 900 walikimbia makazi yao, hasa katika kambi za wakimbizi za Jenin, Tulkarm na Nur Shams. 

Tangu Oktoba 7, wastani wa kila mwezi wa Wapalestina 280 wamefurushwa makwao katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, ikilinganishwa na Wapalestina 128 waliokimbia makazi yao kila mwezi katika miezi tisa ya kwanza ya 2023.

Zaidi ya hayo, tangu Oktoba 7, 2023, angalau watu 1,244, ikiwa ni pamoja na watoto 600, wamekimbia makazi yao kutokana na vurugu za walowezi wa Kiyahudi na vikwazo vya upatikanaji wa msaada. 

Kaya zilizohamishwa zinatoka kwa angalau jamii 20 za wafugaji Wabedouin.

Zaidi ya hayo, Waisraeli 16, wakiwemo wanajeshi watano wa Israel na walowezi saba, waliuawa na 111 kujeruhiwa katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, na Israel, kati ya Oktoba 7, 2023 na Aprili 1 mwaka huu. “Kati yao, 14 waliuawa na Wapalestina wawili waliuawa kimakosa na wanajeshi wa Israel wakati wa shambulio la Wapalestina.”

Hema lililojengwa kwa makopo ya chakula katika makazi ya Deir Al-Balah, Gaza
UN News/Ziad Taleb
Hema lililojengwa kwa makopo ya chakula katika makazi ya Deir Al-Balah, Gaza

Kusitishwa kwa utoaji wa misaada

Kuhusiana na hali ya Gaza, Umoja wa Mataifa umesema ulisimamisha usafiri wa usiku kwa angalau saa 48 katika eneo la Palestina siku ya Jumanne wiki hii ili kutathmini hofu ya usalama, kufuatia vifo vya wafanyakazi wa shirika la misaada la World Central Kitchen.

Hata hivyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP linaendelea na shughuli zake za kila siku, ikiwa ni pamoja na kutuma misafara ya kila siku kaskazini mwa Gaza.

Kwa upande wake, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO limesema kwa mara nyingine tena liliomba mamlaka ya Israeli siku ya Jumatano kuwezesha operesheni yake katika Hospitali ya Al Shifa katika Jiji la Gaza.

Maombi kadhaa yamekataliwa, kuahirishwa au kuzuiwa kwa muda wa wiki mbili zilizopita. 

Timu za WHO pia zilipanga kuzuru hospitali nyingine mbili kaskazini mwa Gaza siku ya Alhamisi, ambazo ni Sahaba na Ahli, lakini hazikupata kibali.

Uharibifu mkubwa wa makazi ya watu Gaza
UN News/Ziad Taleb
Uharibifu mkubwa wa makazi ya watu Gaza

Zaidi ya watu 33,000 wameuawa Gaza

Kwa mapana zaidi, Umoja wa Mataifa unaweza tu kusisitiza, kwa mara nyingine tena, kwamba kuahirishwa na kukataliwa kwa operesheni za kibinadamu sio tu ni kuzuia kuwafikia wale wanaohitaji msaada huo lakini pia kunaathiri shughuli zingine, kwa kupeleka rasilimali chache.

Takriban Wapalestina 33,037 wameuawa na wengine 75,668 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7, kulingana na ripoti za vyombo vya habari, kwa kutumia takwimu za wizara ya afya ya Palestina. 

Pia Wapalestina 62 waliuawa na 91 kujeruhiwa katika muda wa saa 24 zilizopita, imeongeza wizara hiyo.

Kwa upande wake, jeshi la Israel limebainisha kuwa wanajeshi 255 wameuawa na wanajeshi 1,549 wamejeruhiwa huko Gaza tangu kuanza kwa operesheni ya ardhini, kulingana na hesabu iliyofanywa Aprili 3. 

Zaidi ya hayo, Waisraeli 1,200 na raia wa kigeni wamejeruhiwa waliouawa nchini ya mamlaka ya Israel, wengi wao Oktoba 7. 

Kufikia Aprili 3 mwaka huu, mamlaka ya Israel inakadiria kuwa Waisraeli 134 pamoja na raia wa kigeni bado wanashikiliwa mateka huko Gaza, wakiwemo marehemu ambao miili yao haijaachiliwa.