Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaanza uchunguzi wa mlipuko Lebanon uliojeruhi walinda amani

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakipiga doria huko El Odeisse, kusini mwa Lebanon.
UNIFIL/Pasqual Gorriz
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakipiga doria huko El Odeisse, kusini mwa Lebanon.

UN yaanza uchunguzi wa mlipuko Lebanon uliojeruhi walinda amani

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani kusini mwa Lebanon, UNIFIL, umetangaza kuwa unachunguza mlipuko uliotokea eneo la Rmeish, na kujeruhi walinda amani wanne ambao walikuwa wakifanya doria bila silaha kwenye eneo lisilo la mapigano au BLUE LINE ambalo linatenganisha Israel kutoka Lebanon na milima ya Golan inayogombaniwa na pande zote mbili.

Taarifa iliyotolewa jumamosi na msemaji wa UNIFIL, Andrea Tenenti inasema majeruhi hao ni waangalizi watatu wa kijeshi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, UNTSO, na mkalimani wa lugha ya kilebanon, na wote walisafirishwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Shirika la habari la Lebanon, liliripoti kuwa walinda amani hao wa Umoja wa Maaifa walikumbwa na kombora lililorushwa na Israeli, kombora ambalo lilirushwa kwa kutumia ndege isiyo na rubani au droni. Hata hivyo msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter, amesema jeshi la Israeli, IDF, hakulilenga magari yoyote ya UNIFIL kwenye eneo la Rmeish.

Bwana Tenenti alieleza kuwa waangalizi kutoka UNTSO, walikuwa sehemu ya kundi la uangalizi la Lebanon, OGL, wakisaidia UNIFIL kutekeleza jukumu lake na kusaidia serikali ya Lebanon kusimamia mipaka yake.

Je "Blue Line" ni nini? Bofya hapa kuelewa zaidi.

Pande zote kwenye mzozo zina wajibu kisheria

Msemaji huyo amesisitiza wajibu wa pande zote kinzani kwenye mzozo huo, kwa mujibu wa sheria ya kimataifa wahakikishe ulinzi wa watu wasio kwenye mapigano, na ametoa wito wa sitisho la makabiliano ya kijeshi yanayotumia silaha nzito, ili kuepusha watu wengi zaidi kujeruhiwa.

Akihojiwa na vyombo vya h abari, Bwana Tenenti amesema, kufuatia mashambulio ya Hamasi tarehe 7 Oktoba dhidi ya ISraeli, thali kusini mwa Lebanon imezidi kuwa tete, huku mashambulizi ya makombora yakiendelea ndani ya Lebanon ambayo “yanaweza kuchochea mzozo zaidi.”

Siku mbili kabla ya mlipuko huo, UNIFIL ilieleza wasiwasi wake juu ya ongezeko la ghasia kwenye eneo lisilo la mapigano mpakani mwake na Israeli, ghasia ambazo zimesababisha idadi kubwa ya majeruhi raia ,na  uharibifu wa nyumba na njia za kujipatia kipato.

Amesihi pande zote kuanza mchakato wa endelevu wa kisaisa na kidiplomasia ili hatimaye kufikia suluhisho.

Kauli ya Guterres

Baadaye Jumamosi, Katibu Mkuu wa UN António Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, alieleza kuwa hali kwenye eneo hilo lisilotakiwa kuwa na mapigano (Blue Line)  inaendelea kutia hofu, akigusia makabiliano ya kila siku ambayo yamekuwa yakiendelea kati ya vikundi visivyo ya kijeshi huko Lebanon na jeshi la ulinzi la Israel tangu tarehe 8 Oktoba 2023.

Idadi ya vifo miongoni mwa raia ambavyo vimeripotiwa, uharibifu wa makazi na maeneo ya kilimo na ukimbizi wa makumi ya maelfu ya watu pande zote za eneo hilo lisilopaswa kuwa na mapigano, haikubalili, amesema Katibu Mkuu wa UN, akisema inatishia usalama na utulivu wa Lebanon, Israeli na ukanda mzima.