Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa sikukuu ya Pasaka ulete mabadiliko chanya duniani- Balozi Francis

Rais wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la UN Balozi Dennis Francis
UN Video
Rais wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la UN Balozi Dennis Francis

Ujumbe wa sikukuu ya Pasaka ulete mabadiliko chanya duniani- Balozi Francis

Amani na Usalama

Wapendwa marafiki zangu, Pasaka ni kipindi muhimu sana katika kalenda ya kiimani kwani waumini wa kikristo duniani kote wanakusanyika kwa ajili ya shamrashamra, umoja, matumaini na kutoa ahadi.

Ndivyo alivyoanza Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Balozi Dennis Francis kwenye ujumbe wake wa sikukuu ya Pasaka kwa mwaka huu wa 2024, sikukuu ambayo waumini wa kikristo duniani wanakumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

Balozi Francis anasema, Pasaka ni sherehe ya utakaso, kuzaliwa upya na kuanza tena upya. Ni ushindi wa uhai dhidi ya kifo.

Ujumbe wa Pasaka haupitwi na wakati

“Katika zama hizi za changamoto kubwa, nyakati za vita, hofu, tamaa ya umiliki wa mali na chuki ikitia kiza matumaini ya amani, ujumbe wa Pasaka ambao katu haupitwi na wakati, unaimarisha azma yetu ya kuheshimu na kutambua upekee wa hali ya kibinadamu na kuazimia tena sisi wenyewe ya kuinua hali za watu kokote waliko ili kuwapatia tena fursa ya siku angavu,” amesema Rais huyo wa Baraza Kuu.

Ni kwa mantiki hiyo anatoa wito hebu na tuweke pamoja fikra zetu na nyoto zetu katika ahadi hii ya amani, ustawi, maendeleo na uendelevu kwa kila mtu, na zaidi ya yote tuchukue hatua kila mmoja mmoja na kwa pamoja ili tuweze kufanikisha malengo haya kwa dhati kwa ajili ya wakazi wa dunia.

Kila mtu achukue hatua ili kesho ya kila mtu  iwe bora na yenye ustawi

Ametoa changamoto kwa kila mkazi wa dunia atekeleze wajibu wake ili kesho iwe bora na salama zaidi kwa ajili ya raia wa Ukraine, Urusi, Haiti, Somalia na kwa kila mtu bila kujali alivyo, duniani kote.

“Nakutakieni sikukuu njema ya Pasaka iliyojaa amani, maelewano, upendo na wingi wa kila kilicho bora,” ametamatisha ujumbe wake.

Sikukuu ya Pasaka itasherehekewa jumapili tarehe 31 Machi, 2024 ikiwa imetanguliwa na Ijumaa Kuu tarehe 29 Machi, 2024, ambayo ni kumbukizi ya kifo cha Yesu Kristo kwenye mlima wa Kalvari  huko Yerusalem, Mashariki ya Kati.