Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW68: Baada ya miongo kadhaa ya maendeleo, haki za wanawake zinadhoofishwa - Guterres

Wanawake na wanaume huko Cox's Bazar nchini Bangladesh wakishiriki katika tukio la Orange the World kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake. (Maktaba)
© UN Women/Magfuzur Rahman Shana
Wanawake na wanaume huko Cox's Bazar nchini Bangladesh wakishiriki katika tukio la Orange the World kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake. (Maktaba)

CSW68: Baada ya miongo kadhaa ya maendeleo, haki za wanawake zinadhoofishwa - Guterres

Wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema, "Wanawake wa kizazi changu hawakushinda vita ya kupigania haki zao, na wameshuhudia binti zao na wajukuu wakipigana vita hizo hizo."

Akizungumza leo (13 Machi) katika mkutano na wawakilishi wa asasi za kiraia kando ya Mkutano wa 68 cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake (CSW), Guterres amesema kwa kiwango cha sasa, wanawake na wasichana milioni 340 bado watakuwa wanaishi katika umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030.

Pia amesema, "Baadhi ya nchi zinashuhudia maendeleo ya miongo kadhaa kuhusu usawa wa kijinsia yakirejeshwa nyuma na kufutwa. Ulimwenguni kote, haki za wanawake zinaminywa, nafasi ya kiraia inabanwa, na watetezi wa haki za wanawake wanakabiliwa na vitisho vya vurugu kwa kuthubutu kutetea haki. Afghanistan ni mfano mbaya zaidi."

Guterres amesisitiza kwamba migogoro "inayoendelea duniani kote ni janga kwa wanawake na wasichana - kama tulivyoona waziwazi katika mwaka uliopita na zaidi."

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, hii inajumuisha: Ripoti za ubakaji na ulanguzi wa wanawake nchini Sudan; Matendo ya unyanyasaji wa kijinsia na dalili za mateso ya kingono wakati wa mashambulizi ya kigaidi yaliyotekelezwa na Hamas nchini Israel - kama ilivyobainishwa hivi majuzi katika ripoti ya Umoja wa Mataifa; Ushuhuda wa unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wafungwa wa Kipalestina, kama ilivyoainishwa katika ripoti hiyo hiyo; uharibifu wa huduma za uzazi huko Gaza, ambapo wanawake na watoto wanaripotiwa kuwa zaidi ya theluthi mbili ya makumi ya maelfu ya watu waliouawa.

Pia amesema, "Kuna hatari kubwa kwamba ubaguzi unajengwa katika namna ambayo Akili Mnemba (AI) inajikita, ambayo inaweza kuingiza upendeleo katika shughuli muhimu kama kuajiri, kupanga miji, na picha za matibabu kwa miongo kadhaa ijayo kwa madhara ya haki za wanawake. Serikali, mashirika ya kiraia, tasnia ya teknolojia, na wengine lazima waje pamoja ili kupunguza mgawanyiko wa jinsia ya kidijitali na kuhakikisha wanawake wanatoa mchango wao kamili kwa teknolojia ya kidijitali katika viwango vyote.”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake, Sima Sami Bahous, ambaye ameongoza mkutano huo, amesema, "Tunahitaji mashirika ya wanawake yenye rasilimali za kutosha kushughulikia chuki dhidi ya wanawake na wasichana, na tunahitaji kukisukuma nyuma kile kinachotusukuma nyuma."