Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa yaendelea kukatili maisha ya watoto Gaza: UN

Timu ya wafanyakazi wa shirika la UNRWA wakiendelea kugawa msaada wa unga Kusini mwa Gaza ingawa msaada huo hautoshelezi kukidhi mahitaji
© UNRWA
Timu ya wafanyakazi wa shirika la UNRWA wakiendelea kugawa msaada wa unga Kusini mwa Gaza ingawa msaada huo hautoshelezi kukidhi mahitaji

Njaa yaendelea kukatili maisha ya watoto Gaza: UN

Amani na Usalama

Zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kukiwa hakuna makubaliano ya kusitisha mapigano yanayotarajiwa kwa Gaza, wahudumu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa leo wameelezea wasiwasi wao mkubwa kwamba kuna idadi kubwa inayoongezeka ya watoto wanaokufa kwa njaa.

Kupitia kati ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema “Hali inatisha. Kila dakika, kila saa, inazidi kuwa mbayá.” 

Zaidi ya malori 150 yamekuwa yakifika kaskazini mwa Gaza kila siku, ambapo mtoto mmoja kati ya sita wa  umri wa chini ya miaka miwili ana utapiamlo mkali na duru za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa angalau watoto 20 wamekufa kwa njaa katika siku za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na mtoto mchanga wa siku 14.

 Sigrid Kaag, Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi mpya wa Gaza akitoa maelezo kwa wanahabari kufuatia mashauriano na Baraza la Usalama.
UN Photo/Manuel Elías
Sigrid Kaag, Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi mpya wa Gaza akitoa maelezo kwa wanahabari kufuatia mashauriano na Baraza la Usalama.

Taarifa ya Sigrid Kaag

Baadaye leo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mashauriano ya faragha kuhusu hali hiyo ambapo Mratibu Mwandamizi wa wa masuala ya Kibinadamu na Ujenzi wa Gaza, Sigrid Kaag, anatarajiwa kutoa maelezo mafupi.

Zaidi ya watu 30,000 sasa wameuawa katika mashambulizi ya Israel yanayoendelea kila kila siku kote Gaza, kujibu mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,200 na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka.

Mazungumzo ya awali nchini Qatar na wiki hii mjini Cairo Misri kwa ajili ya kusitisha mapigano yanayohusiana na kuachiliwa kwa mateka 100 waliosalia na upatikanaji wa misaada zaidi ya kibinadamu kote Gaza hadi sasa hayajazaa matunda ya kumalizika kwa ghasia wala kupunguza janga la kibinadamu linaloendelea.

Mtoto 1 kati ya 6 mwenye umri wa chini ya miaka 2 Gaza ana utapiamlo mbaya zaidi
© UNRWA
Mtoto 1 kati ya 6 mwenye umri wa chini ya miaka 2 Gaza ana utapiamlo mbaya zaidi

Matumaini ya kutumia kivuko cha kaskazini

Kutokana na kukosekana kwa makubaliano ya usitishaji uhasama kati ya Hamas na Israel, timu za misaada ya kibinadamu  za Umoja wa Mataifa leo zimepanga kuchunguza uwezekano wa kutumia barabara ya kijeshi ya Israel kuelekea kaskazini mwa Gaza kusafirisha angalau malori 300 ya misaada kila siku.

Afisa mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa katika eneo linalokaliwa la Palestina Jamie McGoldrick, alitangaza mpango wa msafara wa misaada jana Jumatano. 

Amefafanua kuwa njia itawezesha malori yaliyosheheni vifaa vya kibinadamu kuwafikia watu walio hatarini kaskazini mwa eneo hilo bila kulazimika kujadili vikwazo na ukosefu wa usalama.

"Tunalazimika kutumia barabara hii ya kijeshi, barabara hii iliyozungushiwa uzio pembeni, upande wa mashariki mwa Gaza, ili kuruhusu msaada kutoka kwenye kivuko cha Kerem Shalom na Rafah, hadi kuelekea kaskazini na kuingia kaskazini, na kufikia mahali pa kuvuka huko,” amesisitiza Bwana. McGoldrick, katika mkutano kwa njia ya video kwa waandishi wa habari. 

Ameongeza kuwa "Tunalazimika kuingiza angalau malori 300 kwa siku. Hivi sasa, tutakuwa na bahati ikiwa tutapata takriban 150.

Kabla ya kuanza kwa Ramadhani siku ya Jumapili wiki hii, afisa huyo mkongwe wa masuala ya kibinadamu amebainisha kuwa misaada inayoingia Gaza mwezi Februari ilipungua kwa nusu ikilinganishwa na Januari, licha ya "mahitaji makubwa na yanayoongezeka kwa zaidi ya watu milioni 2.3 wanaoishi katika hali mbaya".