Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kujadili mashambulizi ya Marekani huko Syria na Iraq

Baraza la Usalama la UN lilipokutana leo 5 Februari 2024 kujadili tishio la amani na usalama Mashariki ya Kati
UN /Evan Schneider
Baraza la Usalama la UN lilipokutana leo 5 Februari 2024 kujadili tishio la amani na usalama Mashariki ya Kati

Baraza la Usalama lakutana kujadili mashambulizi ya Marekani huko Syria na Iraq

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu alasiri limekuwa na kikao cha dharura kufuatia ombi la Urusi, wakati huu ambao vita huko Gaza inaendelea kuchochea mivutano huko Mashariki ya Kati, hasa uwezekano wa kuathiri vibaya amani na usalama kwenye ukanda huo. Mkuu wa Idara ya UN ya Masuala ya Kisiasa, ameliomba Baraza lizuie kushamiri zaidi kwa uhasama na mivutano  kwenye ukanda mzima

Rosemary DiCarlo akihutubia mabalozi kwanza alionya ongezeko la mashambulizi huko Mashariki ya Kati ni jambo linaloweza kuchochea hatua zisizotabirika.

Amesema kama ambavyo kila mtu kwenye medani za kidiplomasia anafahamu “mivutano iliyokumba nchi kadhaa Mashariki ya Kati inazidi kuongezeka.”

Amekumbusha kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  António Guterres amerudia mara kw amara kuhusu hatari za kusambaa zaidi kwa mashambulizi ya kijeshi na hatua zisizotabirika tangu shambulio la kigaidi la Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 “lilipowasha moto” kwenye eneo hilo.

“Tumeshuhudia matukio ya takribani kila siku kwenye eneo hili. Haya yanajumuisha mashambulizi 165 dhidi ya vituo vya Marekani huko Syria na Iraq, matukio ambayo yamesababisha Marekani kushambulia nchi mbili hizo,” ameesma Bi. DiCarlo.

Tarehe 28 mwezi uliopita wa Januari, shambulio la ndege isiyo na rubani lilisababisha vifo vya askari watatu wa Marekani na kujeruhi wengine 40 kwenye kituo cha kijeshi cha Marekani kaskazini-magharibi mwa Jordan, amesema afisa huyo mwandamizi wa UN, akiongeza kuwa tarehe 2 mwezi huu wa Februari, Marekani ilifanya mashambulizi 85 ya anga huko Iraq na Syria dhidi ya kilichoripotiwa kuwa ni wanamgambo wa Kikundi cha kiislamu cha kimapinduzi cha Iran, (IRGC) na makundi mengine shirika.

“Marekani inasema ililenga maeneo ya kutoa amri na yanayodhibiti operesheni, vituo vya kiintelijensia na vyenye silaha, na kwamba haikuwa inasaka mzozo Mashariki ya Kati au kwingineko,” amesema Bi. DiCarlo akiongeza kuwa Syria na Iraq zote zimelaani mashambulio hayo.

Nchi mbili hizo pia zimedai kuwa mashambulio hayo yamesababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia.

Rosemary DiCarlo, Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kisiasa kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama lilipokutana kujadili hali ya Mashariki ya Kati
UN /Eskinder Debebe
Rosemary DiCarlo, Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kisiasa kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama lilipokutana kujadili hali ya Mashariki ya Kati

Kuanzia eneo lisilopaswa kuwa na mapigano hadi Bahari ya Sham

Bi. DiCarlo ameelezea hali tete kwingineko kwenye ukanda huo wa Mashariki ya Kati, ikiwemo kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hezbollah kwenye eneo lisilopaswa kuwa na operesheni za kijeshi linalotenganisha jeshi la Israel na lile la Lebanon.

Mashambulizi ya mara kwa mara ya maroketi yalifanyika kwenye eneo linalokaliwa la milima ya Golan kati ya Israel na wanamgambo wanaoshukiwa kuwa na ushirika na Iran, halikadhalika mashambulizi ya anga yanayodaiwa na Syria kufanywa na Israel kwenye maeneo kadhaa ya taifa hilo.

Bi. DiCarlo amesema pia kombora lililorushwa na wanamgambo wa kihouthi, na pia kwa njia ya ndege isiyo na rubni dhidi ya meli huko Bahari ya Sham, na mashambulio ya kulipiza kisasi kutoka Uingereza na Marekani.

“Nasisitiza wito wa Katibu Mkuu wa pande zote zijiepusha na kufanya hali kuwa mbaya zaidi, na zifikirie pia gharama za kibinadamu na kiuchumi za mzozo huo Mashariki ya Kati.”

Ametoa wito pia kwa Baraza la Usalama liendelee kushiriki kikamilifu kuzuia kusambaa zaidi na kuongezeka kwa mivutano inayokwamisha hali ya usalama na amani Mashariki ya Kati.