Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF: Watoto 170,000 nchini Haiti wafurushwa makwao

Familia ya watu waliohamishwa makazi yao huko Tabarre, Haiti wakusanyika kwenye tovuti.
© UNICEF/Ndiaga Seck
Familia ya watu waliohamishwa makazi yao huko Tabarre, Haiti wakusanyika kwenye tovuti.

UNICEF: Watoto 170,000 nchini Haiti wafurushwa makwao

Amani na Usalama

Wakati mzozo wa makundi yanayotumia silaha uliendelea kuongezeka nchini Haiti, shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF hii leo limeeleza idadi ya watoto waliokimbia makazi yao imefikia 170,000 na kutaja kuwa hiyo ni idadi kubwa ya kutisha inayoashirikia kuzidi kuzorota kwa usalama nchini humo huku watoto na familia zao wakizidi kuwa hatarini. 

Mwakilishi wa UNICEF nchini Haiti Bruno Maes katika taarifa yake baada ya kutembea maeneo matatu ya wakimbizi wa ndani huko Port- Au- Prince amesema kuwa “Tunashuhudia janga likitokea mbele ya macho yetu. Nchini Haiti, watoto na familia zao kilasiku wanastahimili mawimbi ya kutisha ya ukatili, kupoteza wapendwa wao, nyumba kuharibiwa na moto, na wameghubikwa na kivuli cha hofu.” 

Taarifa za awali zilizopokelewa na UNICEF zinaonesha taswira ya kutisha ya mgogoro wa sasa, ikifichua ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto. Watoto wamenaswa katikati ya mapigano hayo ya makundi yenye silaha, wanapata majeraha, au kupoteza maisha, huku baadhi ya matukio yakitokea wakati wakielekea shuleni. 

Zaidi ya hayo UNICEF imeeeleza kuna ongezeko la matukio ya watoto kuandikishwa kwa nguvu, huku wengine wakijiunga na vikundi vyenye silaha.

Vurugu hizo zikiambatana na baadhi ya maandamano zimesababisha mamia ya shule kufungwa na watoto kunyimwa haki yao ya kupata elimu. Pia inazuia upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, na kukwamisha juhudi za watendaji wa kibinadamu ambao ni muhimu katika kutoa misada ya dharura kwa wale wenye uhitaji.

“Hatuwezi kukaa bila kuchukua hatua wakati mustakabali wa watoto wa Haiti unaharibiwa na mateso yasiyokwisha. Kila wakati tusipochukua hatua, mzozo unaendelea kuongezeka na kuteketeza maisha yao. Jumuiya ya kimataifa ina jukumu la kuleta matumaini na mabadiliko kwa maisha haya ya vijana, kuhakikisha kuwa kuna mwanga zaidi na mustakabali salama zaidi kwao,” alisema Maes.

Kwa mujibu wa UNICEF takwimu za hivi punde zaidi mwezi Januari 2024, zinaonesha karibu watu 314,000 wameyakimbia makazi yao nchini kote, wengi wao wakiwa kutoka Port-au-Prince na Artibonite department, nusu yao inakadiriwa kuwa watoto. 

Katika muda wa chini ya wiki mbili, karibu watu 2,500, wengi wao wanawake na watoto, wamekimbia makazi yao mapya kufuatia mapigano katika maeneo ya Solino na Gabelliste, katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince. Hali ya sasa inaweka shinikizo kubwa kwa rasilimali ambazo ni finyu.

UNICEF inakadiriwa watoto milioni 3 nchini Haiti watahitaji msaada wa kibiandamu.

Tayari shirika hilo na wadau wake wanatoa misaada mbalimbali.

UNICEF inaomba dola milioni 221.7 kwa mwaka 2024 ili kuweza kusaidia zaidi wananchi wa Haiti hususan watoto.