Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yazindua ombi la dola bilioni 1.5 kwa ajili ya dharura kwa 2024

Mwanamke akipokea matibabu katika kituo cha matibabu ya kipindupindu nchini Sudan.
© WHO/Ala Kheir
Mwanamke akipokea matibabu katika kituo cha matibabu ya kipindupindu nchini Sudan.

WHO yazindua ombi la dola bilioni 1.5 kwa ajili ya dharura kwa 2024

Afya

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO leo limezindua ombi la dola bilioni 1.5 kulinda afya ya watu walio hatarini zaidi katika dharura 41 kote ulimwenguni kwa mwaka 2024.

Ombi hilo linahusu dharura zinazodai kiwango cha juu zaidi cha hatua za kuzikabili nazo kutoka kwa WHO, kwa lengo la kufikia zaidi ya watu milioni 87. Ombi hilo limetolewa katika muktadha wa dharura tatakuanzia migogoro, mabadiliko ya tabianchi na kuyumba kwa uchumi, ambazo zinaendelea kuchochea watu kuhama na kukimbia makwao, njaa na ukosefu wa usawa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus

"Kwa wale wanaokabiliwa na dharura, kukatizwa kwa huduma muhimu za afya mara nyingi kunamaanisha tofauti kati ya maisha na kifo. Kuanzia akina mama wanaojifungua wakati wa migogoro, misaada kwa watoto wadogo katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame, kwa wale wanaopata matibabu ya saratani au dialysis, huduma za afya huokoa maisha. Na huduma za afya pia ni muhimu kwa kuvunja mzunguko ambao mara nyingi huacha jamii katika hali ya hatari na kutegemea msaada zaidi wa dharura," 

Msaada huo wa fedha utaokoa maisha

WHO inasema msaada huo kwa mwaka 2024 utawezesha huduma ya afya ya kuokoa maisha, usambazaji wa vifaa muhimu vya afya na vinginevyo, pamoja na ukarabati wa huduma muhimu za afya ili kuhakikisha huduma endelevu. 

Limeongeza kuwa ufadhili huo unasaidia upatikanaji wa moja kwa moja wa huduma za afya kwa jamii katika maeneo ambayo ni magumu kufikiwa, kwa ushirikiano na mashirika ya ndani na hatua madhubuti za kufuatilia, kushiriki habari na kuandika kuhusu milipuko na mashambulizi kwa wahudumu wa afya. Vitendo vingine muhimu ni kudumisha mifumo iliyopo ya utunzaji wa afya na kujenga mnepo dhidi ya vitisho vya siku zijazo.

Ombi hilo linabainisha thamani chanya ya ufadhili kusaidia watu wenye mahitaji ya kibinadamu. 

Kila dola moja ya Marekani iliyowekezwa katika WHO inatoa faida kwa uwekezaji wa angalau  dola 35.

Mgawanyo wa fecha za msaada huo kikanda

Ufadhili huo utakwenda katika kanda mbalimbali za WHO ambapo Kanda ya Afrik itapata dola milioni 334, Kanda ya Mediterania ya Mashariki itapokea dola milioni 705, kanda ya Ulaya dola milioni 183, Kanda ya Pasifiki ya Magharibi dola milioni 15.2, Kanda ya Kusini-Mashariki ya Asia dola milioni 49 na Kanda ya Amerika dola milioni 131.

Dk Tedros amesema "Kwa msaada wa wafadhili, tutaokoa maisha, kukidhi mahitaji muhimu ya afya kwa walio hatarini zaidi, na kusaidia jamii kujikwamua kutoka kwa majanga na kuwajengea uwezo mkubwa wa kukabiliana na matishio ya kiafya siku zijazo. “

Ameendelea kusema kwamba “WHO inathamini usaidizi wote uliopokelewa mmwaka 2023, ambao ulituruhusu kusaidia mamilioni ya watu. Tunapoingia 2024, mshikamano na uungwaji mkono wa jumuiya ya kimataifa unahitajika zaidi kuliko wakati mwingine wowote.”