Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yazindua ombi la dola bilioni 4.2 kwa ajili ya kuwasaidia Waukraine

Mashirikak ya UN na wadau wake wanatoa misaada kwa watu walioathiriwa na mapigano mapya huko Lviv
© UNOCHA/Allaham Musab
Mashirikak ya UN na wadau wake wanatoa misaada kwa watu walioathiriwa na mapigano mapya huko Lviv

UN yazindua ombi la dola bilioni 4.2 kwa ajili ya kuwasaidia Waukraine

Msaada wa Kibinadamu

Takriban miaka miwili sasa tangu majeshi ya Urusi yaanzishe "vita kamili na kuikalia Ukraine, amesema leo mkuu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura Martin Griffiths akitoa ombi la dharura la pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR la dola bilioni 4.2 ili kuwasaidia walio hatarini nchini Ukraine.

Leo hii, takriban watu milioni 14.6 nchini Ukraine wanahitaji msaada wa kibinadamu sawa na asilimia 40 ya watu wote huku watu wengine milioni 6.3 wamekimbia nje ya mipaka yake kama wakimbizi.

Bwana. Griffiths amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba "Lazima tubaki kwenye mkondo unaotakiwa na watu wa Ukraine. Hakuna mahali ambapo vita havijagusa na wimbi la mashambulizi yaliyoanza kabla ya mwaka mpya".

Huku kukiwa na mashambulizi ya mara kwa mara katika maeneo ya mstari wa mbele na Urusi na katika miji ya Ukraine katika wiki za hivi karibuni, Bwana Griffiths ameangazia gharama kubwa na mbaya kwa raia inayotokana na vita hii, haswa katika mikoa ya Donetsk na Kharkiv, ambapo familia hujificha katika nyumba zilizoharibiwa vibaya bila maji ya bomba, gesi au umeme.

Miji kote Ukrainia, ikiwa ni pamoja na Dnipro (pichani), ilishambuliwa kwa mabomu sana katika kipindi cha sikukuu.
© UNOCHA/Oleksii Holenkov
Miji kote Ukrainia, ikiwa ni pamoja na Dnipro (pichani), ilishambuliwa kwa mabomu sana katika kipindi cha sikukuu.

Rasilimali zilizotumika

Watu katika vijiji vilivyo hatarini zaidi sasa wamechoka "rasilimali zao ni ndogo na wanategemea misaada inayotolewa ili kuishi, kwa uratibu wa karibu na juhudi za serikali ya Ukraine yenyewe”, ameendelea kusema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya dharura.

Mashambulizi yaliyoripotiwa ya ndege zisizo na rubani na makombora pia yamewalazimu watu na haswa wazee kutumia siku zao katika mahandaki ya chini ya ardhi. 

Watoto hawawezi kucheza nje, achilia mbali kuhudhuria shule, kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA.

Ili kuhakikisha Umoja wa Mataifa na mamia ya washirika wa misaada ndani ya Ukraine wanaweza kufikia watu milioni 8.5 walio hatarini zaidi, jumla ya dola bilioni 3.1 zitahitajika mwaka huu.

Mwaka 2023, wafanyakazi wa misaada walifikia karibu watu milioni 11 nchini Ukraine, kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa ya wafadhili na licha ya "changamoto kubwa za ufikiaji wa watu hasa kwenye maeneo yanayokaliwa na Shirikisho la Urusi”, limesema shirika la OCHA.

Athari mbayá za vita

Wakimbizi wa Ukraine katika nchi 11 jirani pia wanahitaji kuongezwa msaada endelevu, amesema Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi Filippo Grandi, alipokuwa akiomba nyongeza ya dola bilioni 1.1 kutoka kwa wafadhili kwa mwaka 2024 kusaidia watu milioni 2.3 waliokimbia makazi yao kutokana na vita, pamoja na jamii zinazowapokea.

"Kuna uwezekano mkubwa zaidi kwamba kile ambacho tumekiona katika mwezi uliopita naweza kusema ni moja ya vipindi vibaya zaidi vya vita katika suala la athari kwa raia," amesema Bwana Grandi huku akisisitiza kwamba "kipaumbele" kinabaki kuwa ni kusaidia watu nchini Ukraine pamoja na milioni sita waliokimbia nchi katika miezi michache ya kwanza ya mzozo, wengine milioni 10 sasa hawako majumbani kwao, na kufanya hili kusalia kuwa janga kubwa zaidi la wakimbizi duniani”, amesisitiza mkuu wa UNHCR.

Akitoa takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, mkuu wa UNHCR amesema kwamba watu 900,000 waliofurushwa mwanzoni na vita wanakadiriwa kurejea Ukraine.

Ameongeza kuwa lakini wengine bado wameyahama makazi yao na wanahitaji usaidizi kwa vile hawawezi kurejea katika nyumba zao ambazo zimeharibiwa au ziko kwenye mstari wa mbele na hatari sana kuishi.

Wakimbizi wa Ukraine wakiwasili katika mpaka wa Medyka nchini Poland. (Maktaba)
© IOM/Muse Mohammed
Wakimbizi wa Ukraine wakiwasili katika mpaka wa Medyka nchini Poland. (Maktaba)

Kukabili matarajio

Ukweli kwamba ombi la UNHCR 2024 ni la chini kuliko ombi la mwaka jana la dola bilioni 1.7 limeonyesha kupungua kwa mahitaji na usaidizi unaopaswa kuwa mfano kutoka kwa serikali za Muungano wa Ulaya EU, ambapo idadi kubwa ya wakimbizi wa Ukraine wamepata makazi,” amesema Bwana Grandi.

Hata hivyo, mahitaji yanasalia kuwa juu nchini Moldova nchi isiyo ya Muungano wa Ulaya ambako wakimbizi wanahitaji kufanya kazi na kuhitaji upatikanaji endelevu wa elimu na huduma za afya.

"Licha ya jitihada za kujumuishwa, ni nusu tu ya watoto wakimbizi wenye umri wa kwenda shule wameandikishwa shule katika nchi zinazowapokea, wakati robo ya wakimbizi wanaohitaji msaada wanatatizika kupata huduma za afya," limesema shirika la UNHCR. 

"Ni asilimia 40 hadi 60 pekee ndio wameajiriwa, mara nyingi katika kazi za chini ya sifa zao, na wengi hubaki katika hatari bila njia ya kujikimu."

Takwimu za hivi karibuni kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR, zinaonyesha kuwa raia 27,449 wameuawa na kujeruhiwa nchini Ukraine, ambapo kati yao 9,701 wameuawa na 17,748 kujeruhiwa. 

Takwimu halisi zina uwezekano kuwa kubwa zaidi, imesema ofisi ya OHCHR ikitoa mfano wa ucheleweshaji unaohusishwa na uhasama mkali na uthibitisho katika maeneo kama Mariupol katika mkoa wa Donetsk, Lysychansk, Popasna na Sievierodonetsk katika mkoa wa Luhansk.