Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukraine: Watoto wawili wameripotiwa kuuawa na wengine 15 wajeruhiwa

Mashirikak ya UN na wadau wake wanatoa misaada kwa watu walioathiriwa na mapigano mapya huko Lviv
© UNOCHA/Allaham Musab
Mashirikak ya UN na wadau wake wanatoa misaada kwa watu walioathiriwa na mapigano mapya huko Lviv

Ukraine: Watoto wawili wameripotiwa kuuawa na wengine 15 wajeruhiwa

Amani na Usalama

Watoto wawili wameripotiwa kuuawa na wengine 15 kujeruhiwa katika mashambulizi yanayoendelea maeneo mbalimbali nchini Ukraine hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini humo Munir Mammadzade.

Taarifa iliyotolewa leo na UNICEF kutoka Kyiv imemnukuu Mammadzade akieleza kuwa Katika siku sita zilizopita, watoto na familia, na miundombinu wanayotegemea imeshambuliwa huko Dnipro, Lviv, Kharkiv, Kyiv, Odesa, na maeneo mengine yenye watu wengi. Pamoja na watoto kuuawa na kujeruhiwa, na shule na vituo vya afya vimeharibiwa, “raia wachanga zaidi wa Ukraine wanaendelea kubeba mzigo wa mashambulizi haya. Mawazo yetu ya kutoka moyoni yako pamoja na wale wote walioathirika.”

Uharibifu ni mkubwa

Takriban shule nane na vituo 10 vya huduma za afya, ikiwa ni pamoja na hospitali ya uzazi, vimeripotiwa kuharibiwa wiki iliyopita. Nyumba zimeharibiwa, na mamilioni ya watoto wameanza mwaka mpya kwa sauti za ving'ora na milipuko ya mabomu, na hivyo kuzua hofu.

Watoto kote Ukraine wamelazimika kukimbilia katika vyumba vya chini ya ardhi, makazi yakujificha yasiyoingia mabomu na vituo vya treni, maeneo hayo yana baridi kali asubuhi.

Kwa watoto ambao nyumba zao zimeharibiwa, na wale ambao wanakosa huduma ya umeme, joto na maji yamekatika, hali ni mbaya sana kwani wanastahimili hali ya joto kali mara nyingi hufikia -20 ° C.

“Takribani watoto 1,800 wameuawa au kujeruhiwa tangu kuongezeka kwa vita nchini Ukraine, kulingana na ripoti zilizothibitishwa na Umoja wa Mataifa.“ amesema Mammadzabe amabaye pia ameeleza kuna uwezekano mkubwa nambari ya waathirika kuwa  ni kubwa zaidi.

Takribani miaka miwili ya vita

Ikifika mwezi Februari, watoto nchini Ukraine watakuwa wamevumilia miaka miwili kamili ya vita. Mamilioni ya watoto wameibiwa utoto wao. Mamilioni ya watu wamepoteza wanafamilia, marafiki, nyumba, shule na jumuiya zao. Na wanaendelea kukabiliwa na hatari kwa usalama na ustawi wao huku mashambulizi na mapigano yakiendelea, hasa kwa watoto wanaoishi katika maeneo yaliyo karibu na mstari wa mbele wa eneo la mapigano.

“Mauaji na ulemavu wa watoto, kushambuliwa kwa shule na vituo vya huduma ya afya ni ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto na lazima ukome. Sheria za vita lazima zizingatiwe. Watoto na miundombinu ya kiraia wanayoitegemea lazima ilindwe. Hatua zote muhimu za kuwalinda lazima zichukuliwe. Mashambulizi dhidi ya watoto na maeneo ya kiraia lazima yakome. “Zaidi ya yote, watoto wanahitaji amani. Watoto wanahitaji nafasi ya kuwa watoto." Ilihitimisha taarifa hiyo ya UNICEF kutoka Ukraine.