Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa Gaza: maeneo ya kusini yanafurika huku kukiwa na wimbi jipya la mabomu na watu kuhama

Mhudumu wa afya akifunga bandeji kwenye mguu wa mtoto katika hospitali moja huko Gaza.
© WHO
Mhudumu wa afya akifunga bandeji kwenye mguu wa mtoto katika hospitali moja huko Gaza.

Mgogoro wa Gaza: maeneo ya kusini yanafurika huku kukiwa na wimbi jipya la mabomu na watu kuhama

Amani na Usalama

Harakati za kusambaza misaada kwa Gaza zimezidi kuwa ngumu huku kukiwa na ripoti za kuendelea kulipuliwa kwa mabomu katika Ukanda huo usiku kucha kunakotekelezwa na jeshi la Israel na mapigano makali "katika maeneo mengi" kati yao na wapiganaji wa Hamas, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wameonya leo Novemba 27. 

Maeneo ya kaskazini na kusini mwa eneo hilo yamepigwa huku vikosi vya ardhini vya Israel vikiripotiwa pia kuingia katika maeneo ya kati, pamoja na kurushwa makombora kulikofanywa na makundi yenye silaha ya Palestina kuelekea Israel, na hali hiyo kusababisha wasiwasi kwa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, kuhusu usalama wa raia.  

Jimbo la Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza sasa "linafurika kwa kasi", Mkurugenzi wa Masuala ya UNRWA huko Gaza Tom White mwishoni mwa jana Jumanne kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter) ameweka video ikionesha msururu mrefu wa magari yakiwa yameshehemi  magodoro yaliyofungwa juu hadi chini pamoja na vitu vingine, kuonesha watu wakiyahama makazi yao.   

Barabara zimevunjwa 

Katika taarifa yake ya hivi karibuni kuhusu mzozo huo, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada (OCHA) inasema kuwa vikosi vya Israel vimeripotiwa kutekeleza mashambulizi "mazito" kutoka angani, nchi kavu na baharini "katika sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza, hususan eneo la Kati" kuanzia tarehe 23 hadi 26 Desemba. 

Hii ni pamoja na "zaidi ya mashambulizi 50" kuanzia tarehe 24 hadi 25 Desemba kwenye kambi tatu za wakimbizi - Al Bureij, An Nuseirat na Al Maghazi – hali ambayo inaripotiwa kuua watu kadhaa na kuzuia kazi ya vikundi vya misaada vilivyokabiliwa na barabara zilizoharibiwa zinazounganisha kambi hizo. 

Zimepita zaidi ya siku 80 tangu mashambulizi ya Jeshi la Ulinzi la Israel katika Ukanda huo kuanza, kujibu mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas kusini mwa Israel, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa kinyama na takriban wengine 240 walichukuliwa mateka. 

Mamlaka ya afya imeripoti kwamba Wapalestina wasiopungua 20,915 wameuawa huko tangu 7 Oktoba - ikiwa ni pamoja na watu 858 kati ya Jumamosi iliyopita na Jumanne. "Takriban asilimia 70 ya waliouawa wanasemekana kuwa wanawake na watoto...Watu wengi hawajulikani walipo, huenda wamezikwa chini ya vifusi, huku wengi wao wakisubiri kuokolewa au kupona." 

OCHA pia imeripoti kuwa wanajeshi 164 wa Israel wamefariki dunia huku wengine 874 wakijeruhiwa wakati wa operesheni za ardhini huko Gaza. 

Hofu ya kiafya iliyoibuka tena 

Hatua hiyo ilifuatia amri mpya ya uokoaji iliyotolewa na Jeshi la Ulinzi la Israel na kuathiri watu wanaoishi katika eneo la kati la Gaza. Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa UNRWA Juliette Touma alitoa onyo jipya kuhusu hali mbaya inayoathiri watu wanaoishi katika kambi za mahema kusini. 

"Una watu 400 wanaotumia choo kimoja," Bi. Touma anasema, akisisitizia wasiwasi wa mara kwa mara kuhusu kuenea kwa ugonjwa unaohusishwa na ukosefu wa mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na maji, usafi wa mazingira na chakula. 

Watoa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa tayari wameelezea jinsi wananchi wa Gaza wenye njaa walivyosimamisha malori ya misaada yaliyokuwa yakielekea wanakoenda kushusha chakula, huku kukiwa na onyo la mara kwa mara kwamba inakuwa vigumu kukidhi mahitaji ya wale wote wa kusini, ambako msongamano wa watu unakadiriwa kuwa watu 12,000 kwa kila kilomita za mraba (karibu maili 7.5).