Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watoto milioni 3 jimbo la Al Jazirah Sudan wako hatarini huku ghasia zikiongezeka: UNICEF

Watoto ambao walikimbia na familia zao Sudan wanakula chakula kilichotolewa na shirika la WFP katika kambi ya wakimbizi Sudan Kusini
© WFP/Eulalia Berlanga
Watoto ambao walikimbia na familia zao Sudan wanakula chakula kilichotolewa na shirika la WFP katika kambi ya wakimbizi Sudan Kusini

Takriban watoto milioni 3 jimbo la Al Jazirah Sudan wako hatarini huku ghasia zikiongezeka: UNICEF

Amani na Usalama

Kuongezeka kwa mapigano katika jimbo la Al Jazirah nchini Sudan kumeripotiwa kuwalazimisha watoto wasiopungua 150,000 kutoka makwao katika muda wa chini ya wiki moja, limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Shirika hilo limesema kuzuka kwa mapigano huko Al Jazirah kunamaanisha kuwa zaidi ya nusu ya majimbo nchini Sudan ambayo ni 10 kati ya 18 yanakabiliwa na migogoro.

Karibu watu milioni 5.9 wanaishi katika Jimbo la Al Jazirah, huku takriban nusu ya watu hao wakiwa ni watoto.

Tangu kuongezeka kwa mzozo nchini Sudan 15 Aprili mwaka huu karibu watu 500,000 wamekimbia ghasia na kwenda mahali pengine nchini humo hadi Jimbo la Al Jazirah, na karibu watu 90,000 kati yao wanaotafuta hifadhi katika mji mkuu wa jimbo hilo wa Wad Madani.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema "Maelfu ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika jimbo la Al Jazirah wamelazimika kukimbia makwao kutafuta usalama huku mapigano yakizuka katika maeneo ambayo hapo awali yalionekana kuwa salama. Wimbi hili jipya la ghasia linaweza kuwaacha watoto na familia wakiwa wamenaswa kati ya mistari ya mapigano au kushikwa na mapigano, na matokeo yake ni mabaya. Huku kukiwa na ripoti za mapigano mapya kwingineko nchini humo, mamilioni ya watoto nchini Sudan kwa mara nyingine wako katika hatari kubwa.”

Wakimbizi wa Sudan nchini Chad wanabeba chakula kinachosambazwa na Umoja wa Mataifa.
WFP/Marie-Helena Laurent
Wakimbizi wa Sudan nchini Chad wanabeba chakula kinachosambazwa na Umoja wa Mataifa.

Mji wa Wad Madani kitovu cha misaada 

Kwa mujibu wa UNICEF mji wa Wad Madani unatumika kama kitovu cha huduma nyingi muhimu, za kuokoa maisha katika jimbo la Al Jazirah, pamoja na kituo cha pekee cha kusafisha figo katika jimbo hilo. 

Jiji hilo kwa sasa linahifadhi mamia ya watoto walio katika mazingira magumu waliohamishwa kutoka maeneo mengine ya nchi, na limetumika kama kitovu cha operesheni za kibinadamu tangu mapigano yalipozuka mwezi Aprili. 

Mashambulizi au kukatizwa kwa huduma hizi kunaweza kuhatarisha maisha ya maelfu ya watu, wakiwemo watoto.

Kuongezeka kwa mapigano kumesababisha kusimamishwa kwa operesheni zote za kibinadamu ndani na kutoka Jimbo la Al Jazirah kufikia tarehe 15 Desemba, na kuathiri zaidi watoto na familia zao.

Bi. Russel amesema "Wenzetu nchini Sudan wamesikia hadithi zenye kuvunja moro na kusikitisha kuhusu safari za kutisha ambazo wanawake na watoto walilazimika kufanya ili tu kufikia usalama wa jiji la Madani. Sasa, hata hali hiyo dhaifu ya usalama imesambaratishwa kwani watoto hao kwa mara nyingine wamelazimika kutoka majumbani kwao. Hakuna mtoto anayepaswa kupata vitisho vya vita. Watoto, na miundombinu ya kiraia wanayoitegemea, lazima vilindwe.”

UNICEF inaendelea kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja kote nchini Sudan, na inasisitiza wito wake kwa pande zote kwenye mzozo kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba watoto wanalindwa na kwamba upatikanaji wa haraka, salama, na usiozuiliwa wa msaada wa kibinadamu kwa watoto na familia zao katika maeneo yaliyoathirika unawezeshwa. 

Shirika hilo linasema bila ufikiaji huo, msaada muhimu wa kibinadamu wa kuokoa maisha hautaweza kufika kwa mamilioni ya watoto walio katika mazingira magumu.