Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa Dengue Afrika 2023, watu 700 walikufa, Burkina Faso ilikuwa na wagonjwa wengi- WHO

Vyandarua vya kulala hulinda dhidi ya mbu wanaobeba magonjwa kama vile homa ya dengue ya malaria.
© UNDP/Gwenn Dubourthoumieu
Vyandarua vya kulala hulinda dhidi ya mbu wanaobeba magonjwa kama vile homa ya dengue ya malaria.

Mlipuko wa Dengue Afrika 2023, watu 700 walikufa, Burkina Faso ilikuwa na wagonjwa wengi- WHO

Afya

Ugonjwa wa Dengue umeendelea kuwa ‘mwiba’ barani Afrika ambapo mwaka huu pekee umesababisha vifo vya watu 700 kati ya wagonjwa 170,000 walioripotiwa kwenye nchi 47 za ukanda wa Afrika wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO. 

Dkt. Diana Rojas Alvarez akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi leo wakati akiwapatia hali ya ugonjwa huo duniani amezitaja nchi za Afrika zilizokuwa na mlipuko wa dengue kuwa ni 15 na miongoni mwao ni Benin, Cape Verde, Chad, Cote d'Ivoire, Ethiopia, Ghana, Guinea, Mali, Nigeria na Burkina Faso.  

Burkina Faso ilikuwa na wagonjwa wengi zaidi, takribani 150,000 kati ya watu  wote hao 170,000 waliothibitika kuwa na ugonjwa huo unaoenezwa na mbu aina ya Aedes.  

“Nadhani bara la Afrika lina uzoefu mkubwa wa kukabiliana na ugonjwa wa Malaria, ambao ni mgonjwa mwingine unaoenezwa na vimelea vya mbu aina ya Anopheles anayeishi ndani ya nyumba. Hata hivyo huyu ni mbu tofauti kabisa na wana tabia tofauti,” amesema Dkt. Alvarez.  

Amefafanua kuwa baadhi ya hatua na mikakati inayochukuliwa kukabili maambukizi ya Malaria haiwezi kukabili maambukizi ya Dengue ambayo huenezwa na Aedes.  

Hivyo amesema kwenye kumkabili Aedes, kinachotakiwa sio tu matumizi ya dawa za kuua vijidudu pekee, bali pia mbinu za kuwadhibiti kuanzia wanapokuwa viluwiluwi au lava, ambapo utatumia dawa ya kuua lava.  

Amesema mbu hao pia wanaishi kwenye mimea ya maua inayowekwa ndani ya nyumba, au chombo chochote cha kuhifadhi maji masafi.  

Kwa hiyo jambo muhimu ni kusaka njia ya kuondoa mazalia ya hao mbu kama njia mojawapo ya kudhibiti viluwiluwi na mbu wakubwa,”  amesema Afisa huyo wa WHO.  

Hivyo amesema kwa sasa WHO wanashirikiana na wadau kupata mbinu ya kuhakikisha hakuna ugonjwa huo au wanapunguza kiwango cha uwepo wa ugonjwa huo ukanda wa Afrika.