Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la watu kutawanywa Sudan linaongezeka huku machafuko yakisambaa: UNHCR

Watu waliotawanywa na mchafuko Sudan wakivuka mpaka kwenda Sudan Kusini
© UNHCR/Ala Kheir
Watu waliotawanywa na mchafuko Sudan wakivuka mpaka kwenda Sudan Kusini

Janga la watu kutawanywa Sudan linaongezeka huku machafuko yakisambaa: UNHCR

Amani na Usalama

UNHCR, Shirika la Umoja wa Msataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, limesema linasikitishwa na janga la watu kuendelea kuzamikika kuyahama makazi yao nchini Sudan na kukimbilia nchi jirani huku mamia ya maelfu ya watu wakikimbia mapigano ya hivi karibuni kabisa katika jimbo la Al Jazirah katikati mwa Sundan jimbo lililo, kusini mashariki mwa mji mkuu, Khartoum

 

Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR Wiliam Spindler  akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo shirika hilo pia “Lina wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za kuongezeka kwa mzozo katika jimbo la Darfur. Mnamo tarehe 16 Desemba, mapigano mapya huko El Fasher, Darfur Kaskazini, yalisababisha vifo vya raia, majeraha, na mamia ya watu kuhama zaidi, yakifuatiwa na uporaji wa nyumba na maduka, na kukamatwa kwa vijana.”

Ameongeza kuwa huko Nyala, Darfur Kusini, shambulio la anga liliripotiwa, na kusababisha vifo, majeraha na uharibifu wa makazi ya raia.

Mapigano makali, yakiwemo mashambulizi ya angani na risasi, yameripotiwa viungani mwa Wad Madani, mji mkuu wa jimbo la Al Jazirah, siku ya Ijumaa, 15 Disemba. 

Mapigano hayo sasa yamefika mjini. Baada ya mzozo kuzuka kwa mara ya kwanza katika mji mkuu wa Sudan mwezi Aprili mwaka huu, zaidi ya watu nusu milioni, ikiwa ni pamoja na wakimbizi 7,000, walikimbilia Wad Madani kutoka Khartoum.

“Kutokana na mpambano hayo ya hivi punde, hofu imeripotiwa kutanda miongoni mwa raia wa Wad Madani na watu walionekana wakiondoka mjini humo kwa magari na kwa miguu, wengine kwa mara ya pili katika miezi michache tu”. 

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, kati ya watu 250,000 na 300,000 wamekimbia Wad Madani na maeneo jirani tangu mapigano hayo mapya yaanze.

UNHCR inasambaza misaada kwa wakimbizi wanaorejea katika kituo cha usafiri huko Renk, Sudan Kusini.
© UNHCR/Andrew McConnell
UNHCR inasambaza misaada kwa wakimbizi wanaorejea katika kituo cha usafiri huko Renk, Sudan Kusini.

UNHCR yahaha kusambaza msaada

UNHCR inafanya kazi ya kuwasilisha na kusambaza misaada muhimu inayohitajika kwa watu wapya waliohamishwa kutoka Al Jazirah hadi majimbo ya Sennar na Gedaref.

UNHCR inasema licha ya juhudi za mashirika ya kitaifa na kimataifa ya kibinadamu na watendaji wa ndani kutoa msaada, hali ya jumla ya kibinadamu bado ni mbaya

Tangu vita vilipozuka mwezi wa Aprili, zaidi ya watu milioni 7 wamekimbia makazi yao nchini Sudan, wengi wao wakihama mara kwa mara kutafuta usalama wa muda. Kuhama huku mara kwa mara kunaonyesha jinsi mzozo huu umekuwa mbaya kwa raia wengi.

Spindler amesema “Tuna wasiwasi kwamba iwapo mapigano yataongezeka na kusambaa katika jimbo la White Nile, yanaweza kuathiri pakubwa kazi ya UNHCR na mashirika mengine ya kibinadamu ambayo yanatoa msaada muhimu kwa zaidi ya wakimbizi 437,000 wa Sudan Kusini na takriban Wasudan 433,000 waliokimbia makazi yao huko.”

Takriban watu milioni 18 kote nchini Sudan wanakabiliwa na njaa kali.
Nearly 18 million people across Sudan are facing acute hunger.
Takriban watu milioni 18 kote nchini Sudan wanakabiliwa na njaa kali.

UNHCR imetoa makazi ya dharura kwa familia 42,000

Tangu kuanza kwa mzozo mwezi Aprili, UNHCR imetoa makazi ya dharura kwa takriban familia 42,000 na misaada muhimu kwa karibu familia 12,000 zilizo hatarini katika Jimbo la White Nile .

Na kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa na washirika wa mashirika yasiyo ya kiserikali, UNHCR imechukua hatua kupunguza hatari ya mlipuko wa kipindupindu katika maeneo ya wakimbizi wa ndani.

Lakini, kusambaa kwa mapigano au kufurika kwa wimbi jipya la wakimbizi kunaweza kutatiza huduma za afya na za WASH (maji, usafi wa mazingira na usafi), na kusababisha athari mbaya.

Pia kuna taarifa za watu wanaoelekea Sudan Kusini, ambako mji wa mpakani wa Renk umefurika kwa kiasi kikubwa na kukosa misaada ya kutosha kukidhi mahitaji ya watu ambao tayari wamefika. 

Mvua kubwa imefanya barabara kutopitika na hivyo kukwamisha uhamisho wa wakimbizi. UNHCR na washirika wake wanafanya wawezavyo kujiandaa, lakini rasilimali tayari zilikuwa zimezidiwa uwezo sana.

UNHCR imesisitiza kuwa “Tunaendelea kutoa wito kwa pande zote katika mzozo kukomesha uhasama huo, kuheshimu usalama wa raia kwa mujibu wa sheria za kimataifa, na kuruhusu ufikiaji wa kibinadamu ili misaada na huduma muhimu za kuokoa maisha ziweze kuwafikia wale wanaozihitaji”.

Mvuana akitembea katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Salaam Darfur Kaskazini
© WFP/Leni Kinzli
Mvuana akitembea katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Salaam Darfur Kaskazini

Dunia isiipe kisogo hali ya Sudan

UNHCR imesisitiza kwamba wakati ukubwa wa mgogoro na uwezekano wa kuyumbisha hali ya utulivu katika eneo zima ukiendelea kukua, dunia lazima isisahau hali inayoendelea nchini Sudan.

“Tunashukuru ufadhili uliopokewa tayari kutoka kwa wafadhili wengi, lakini hautoshi kukidhi mahitaji ya familia ambazo zinakabiliwa na ugumu usiofikirika”. Limeongeza shirika hilo.

Mpango wa kukabiliana na wakimbizi wa Kikanda wa Sudan wa mwaka 2023, ambao ulitaka dola bilioni 1 kukidhi mahitaji ya watu milioni 1.8 nchini Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini mwaka huu, unafadhiliwa kwa asilimia 38 pekee.