Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko makubwa yanaathiri maelfu ya watu waliokimbia makazi yao Pembe ya Afrika: UNHCR

Wanawake wanatembea katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyofurika kaskazini mashariki mwa Kenya.
© UNHCR/Mohamed Maalim
Wanawake wanatembea katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyofurika kaskazini mashariki mwa Kenya.

Mafuriko makubwa yanaathiri maelfu ya watu waliokimbia makazi yao Pembe ya Afrika: UNHCR

Tabianchi na mazingira

Maelfu ya familia zilizokimbia makazi yao, ikiwa ni pamoja na wakimbizi nchini Ethiopia, Kenya na Somalia, wako katika harakati za kukimbia tena, wakiepuka janga la mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika ukanda huo, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi msemaji wa UNHCR William Spindler amesema “Tangu mwanzoni mwa Novemba, zaidi ya wakimbizi 795,000 wamerekodiwa nchini Somalia. Wengi wa walioathiriwa, haswa katika maeneo ya kusini na katikati mwa nchi, tayari walikuwa wakimbizi wa ndani kutokana na migogoro na ukame. Nyumba zimesambaratishwa au kuharibiwa sana na, katika maeneo mengine, watu wanajificha chini ya miti kwenye sehemu za mwinuko. Pia kuna taarifa za kusikitisha za watu kuzama majini.”

Ameendelea kusema kwamba katika mkoa wa Somalia nchini Ethiopia, mamlaka inakadiria kuwa zaidi ya watu 20 wamekufa, wakati zaidi ya watu nusu milioni wameathiriwa na mafuriko. 

Karibu familia 40,000, sawa na karibu watu 240,000, ikiwa ni pamoja na wale wanaosaka usalama kutokana na vita iyoendelea Somalia, wamekimbia makazi yao, zaidi ya nusu yao katika wilaya za Dollo Ado na Bokolmayo. 

Pia amesema katika makazi matano ya wakimbizi, wakimbizi 213,000 wamekumbwa na athari za mafuriko. Maji safi na salama ya kunywa ni haba, kupata huduma za afya ni vigumu na karibu familia 1,000 zimepoteza makazi yao. Licha ya matatizo hayo, wakimbizi wengi wametoa michango ya ukarimu kusaidia wanajamii wanaowapokea ambao pia wameathiriwa na mvua kubwa.”

Kambi ya wakimbizi ya Dadaab iko kaskazini mashariki mwa Kenya.
© UNHCR
Kambi ya wakimbizi ya Dadaab iko kaskazini mashariki mwa Kenya.

Kambi ya wakimbizi ya Daadab imeathirika pia

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa UNHCR takriban watu 25,000 katika kambi za wakimbizi za Dadaab nchini Kenya wameathiriwa na mafuriko, huku wengi wakitafuta hifadhi katika shule ndani ya kambi hizo na pia katika jamii zilizo karibu. 

Wakimbizi wengine pia wamefungua nyumba zao ili kuwahifadhi watu wapya waliokimbia makazi yao, na hivyo kusababisha msongamano katika kaya nyingi. UNHCR inasema barabara zilizofurika maji zimekuwa zikikwamisha harakati za watu na hivyo kuwawia vigumu sana watu wanaoishi katika mazingira magumu kupata huduma ikiwemo wajawazito kufika hospitalini. 

Katika kambi ya Kakuma, familia 100 zililazimika kuhamia maeneo salama kutokana na mmomonyoko mkubwa wa udongo uliosababishwa na mvua hizo.

Uwezo wa watu kuishi umeathirika

Zaidi ya kuhama makwao  UNHCR inasema maisha ya watu yameathiriwa sana. Katika eneo moja kusini mwa Ethiopia, zaidi ya asilimia 65 ya ardhi inaripotiwa kufunikwa na mafuriko. 

Wakati huo huo, zaidi ya mifugo 1,000 wamekufa, na ekari nyingine 1,000 za mazao zimeangamizwa katika mkoa wa Somalia, na hivyo kuhatarisha hali ya chakula ambayo tayari ni mbayá kuzidi kuwa mbayá zaidi.

Pia shirika hilo limeonya kwamba hali ya usafi inatia wasiwasi sana kwani mamia ya vyoo vya jumuiya vimeharibiwa, na hivyo kuwaweka watu katika hatari ya magonjwa ya kuambukiza, ikiwa ni pamoja na kipindupindu. Kwa kuongezea, barabara nyingi zimeharibiwa, na kuathiri ufikiaji wa watu kwenye huduma muhimu kama vile za afya.

Pia limesema mahitaji ya haraka ya watu kwa sasa ni “chakula, makazi ya dharura, vyombo vya jikoni, mablanketi na vitu vingine vya msaada, maji safi na huduma za usafi. Familia zinazoishi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko pia zinahitaji msaada wa haraka ili kuhamia maeneo yenye mwinuko.”.

UNHCR na wadau wanaendelea kutoa msaada

UNHCR na washirika wamesema wanaendelea kusambaza vifaa vya msaada kwa waliokimbia makazi mapya, pamoja na vifaa vya heshima kwa wanawake na wasichana walioathirika. 

Familia pia zinapokea msaada wa pesa taslimu kununua vifaa vya ujenzi vya ndani ili kukarabati au kuimarisha makazi yao na kukidhi mahitaji mengine ya dharura. Mifuko ya mchanga imetolewa ili kuwalinda watu dhidi ya maji ya mafuriko. Msaada wa haraka wa wafadhili unahitajika ili kutoa msaada zaidi, ulinzi na kuokoa maisha kadiri mvua zinavyoendelea kunyesha, na kadiri athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyoonekana kwa walio hatarini zaidi.

Mafuriko hayo yanakuja miezi michache baada ya ukame wa muda mrefu na mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa, ambao athari zake bado zinaendelea kushuhudiwa na mamilioni ya watu Mashariki na Pembe ya Afrika.