Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatoa Dola mil 25 kusaidia Somalia

Picha ya angani inayoonyesha mto Juba uliokauka nchini Somalia. Ukame wa muda mrefu kutokana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa huathiri mamilioni ya watu katika eneo la Pembe ya Afrika.
UN Photo/Fardosa Hussein
Picha ya angani inayoonyesha mto Juba uliokauka nchini Somalia. Ukame wa muda mrefu kutokana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa huathiri mamilioni ya watu katika eneo la Pembe ya Afrika.

UN yatoa Dola mil 25 kusaidia Somalia

Tabianchi na mazingira

Nchini Somalia, Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 25 ili kusaidia nchi hiyo kukabiliana na athari za mafuriko.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amewaambia waandishi wa habari hii leo jijini New York Marekani kuwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na wadau wake wanakadiria kuwa takriban watu milioni 1.6 wanaweza kuathiriwa na mafuriko wakati wa msimu wa mvua wa sasa wa "deyr" - ambayo imeongezeka zaidi kwa sababu ya hali ya El Niño na hali nzuri ya Dipole ya Bahari ya Hindi.

Dujarric amesema maeneo kadhaa katika eneo la Juba ya Kati yamekuwa na mvua nyingi zaidi katika wiki moja iliyopita kuliko wastani wa msimu mzima.

Fedha hizo mpya zilizotolewa na UN ni pamoja na dola milioni 10 kutoka Mfuko Mkuu wa Kukabiliana na Dharura CERF na dola milioni 15 kutoka Mfuko wa Kibinadamu wa Somalia. 

Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia kazi zote za kuokoa maisha, milipuko ya magonjwa na kukabiliana na uhaba wa chakula.

Joto la bahari inayozunguka Kiribati katika Bahari ya Pasifiki limeongezeka kutokana na mabadiliko ya hali ya  tabianchi
UNDP/Andrea Egan
Joto la bahari inayozunguka Kiribati katika Bahari ya Pasifiki limeongezeka kutokana na mabadiliko ya hali ya tabianchi

FAO yatahadharisha kuhusu El Nino

Hali ya hewa wa El Nino itakuwa na madhara makubwa kwenye kilimo na usalama wa chakula, na kutishia maisha ya mamilioni ya watu wanaohitaji msaada wa haraka, limesema hii leo Shirika la Umoja wa Mataifa wa Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa hii leo huko Roma Italia na FAO imetoa ombi la ufadhili wa dharura wa dola milioni 160 kusaidia zaidi ya watu milioni 4.8 walio hatarini zaidi katika nchi 34 na kuzuia uharibifu na upotezaji wa mazao, mifugo, ardhi, maji na miundombinu.

Shirika hilo limeonya kuwa dunia inaingia katika mzunguko wa sasa wa El Niño huku rekodi ya watu milioni 258 wakikabiliwa na njaa kali na ni moja tu ya tano ya fedha zote zinazohitajika kukabiliana na viwango vya juu vya uhaba wa chakula ndio imepatikana. 

FAO imeeleza “Kila dola iliyowekezwa katika mnepo inaweza kuleta faida kwa familia za wakulima kwa zaidi ya dola 7 katika hasara zilizoepukwa na faida zilizoongezwa."

El Niño huathiri kilimo na uzalishaji wa chakula kwa kuleta mvua nyingi au kidogo sana, kutegemea eneo hilo, na kutatiza halijoto.

Wakulima, wafugaji, wavuvi na wazalishaji wengine wadogo wanabeba mzigo mkubwa wa majanga ya hali ya hewa.

Nchini Somalia, shirika la Umoja wa Mataifa liliwasaidia kwa kukarabati sehemu za kukatika kwa kingo za mto kando ya mto Shabelle ili kulinda hekta 40,000 za ardhi ya mazao kutokana na mafuriko.

Soma zaidi taarifa hiyo hapa