Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNCCD kujengea mnepo jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Kenya

Makao makuu ya shirika la kuhifadhi misitu ICRAF nchin Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Makao makuu ya shirika la kuhifadhi misitu ICRAF nchin Kenya.

UNCCD kujengea mnepo jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Kenya

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa mataifa la kudhibiti ueneaji wa majangwa, UNCCD, liko mstari wa mbele kushirikiana na jamii kupata mbinu za kujenga mnepo dhidi ya madhila ya mabadiliko ya tabia nchi. 

UNCCD inajiandaa kwa kongamano maalum la mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP16 utakaofanyika Disemba mwaka ujao kwa ushirikiano na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kutunga sera za kupambana na mabadiliko ya tabianchi-UNFCCC itakayokutana mwezi ujao kwenye maandalizi ya Kikao cha kilele cha mabadiliko ya tabianchi cha COP28 huko Dubai. 

Kwenye mkutano wa siku 2 uliofanyika jijini Nairobi hivi karibuni, wataalam na wanaharakati walibadilishana mawazo kuhusu mbinu mujarab za kufufua mazingira yaliyoharibika na harakati wanazofanya vijijini.

Jamila Gamashana ni mwenyekiti wa kikundi cha kina mama cha Kangalika kinachohusika na uhifadhi wa mazingira na kilimo cha mazao yanayohimili makali ya mabadiliko ya tabianchi katika kaunti ya Tanariver. Kwa mtazamo wake, elimu ya kufufua mazingira yaliyoharibika inaleta tija kwenye kilimo cha kisasa kama pojo kwani “

“pojo zina pesa sana lakini tukianza kulima zinavamiwa na wadudu wa ukame. Ndio sasa tukasitisha kidogo kilimo hicho na kugeukia mahindi. Kwa Sasa tunapata mahindi na tumeboresha maisha yetu , fedha tunapata na kuinua maisha yetu.”

Suluhu za jadi za Kiafrika 

Afrika huathirika zaidi na majanga ikilinganishwa na bara lingine lolote. Azma ya Kikao hiki ni kupunguza gharama na hasara inayotokana na majangwa kupitia miradi ya uwekezaji mashambani na matumizi bora ya maji.

Uhifadhi wa mazingira ya ufukweni na mikoko ni moja ya mbinu za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Zipporah Chalwa ni afisa wa shirika la kuhifadhi mikoko na mazingira la Ceriops lililoko Ukunda, kaunti ya Kwale amehudhuria mkutano huo na anaamini kuwa jamii ikielimishwa na kuona matokeo ya juhudi zao ana kwa ana,mazingira yanasalimika kwavile,“ Chanzo kikubwa cha jamii kukosa chakula ni miti kukatwa, na hii mikoko ndiyo sehemu ambapo samaki wanazaliana. Kwahiyo mikoko ikiondolewa samaki wanakuwa hawana sehemu ya kuleana na kukua ili kuwe na chakula cha kutosha kwa jamii. Sasa wakati wana jamii waligundua hiki ndicho chanzo kupitia wale wachache tuliowapata wamejiunga na sisi. Vijana ndio sauti saa hii. Wanawake ndio wanazo juhudi lakini kazi zao sio za sana. Kwahiyo vijana wamekuwa mstari wa mbele maana shirika letu ni la vijana. Wakati wao wanaona vijana wengine wanajituma nao pia wanataka kujiunga na wenza wao kwa manufaa yao na jamii kwa jumla. 

Wajumbe wakiwa kikaoni ICRAF, makao makuu ya shirika la kuhifadhi misitu
UN News/Thelma Mwadzaya
Wajumbe wakiwa kikaoni ICRAF, makao makuu ya shirika la kuhifadhi misitu

Athari za tabia nchi Afrika

Kulingana na UNCCD, ukame mkali umeshuhudiwa zaidi barani Afrika na kipindi cha miaka 50 iliyopita, hasara za kiuchumi zimepita kiwango cha dola bilioni 70 kutokana na madhila yaliyowafika wakaazi.

UNCCD imebainisha kuwa ifikapo mwaka 2050, ukame unaoongezwa makali na mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira huenda ukawaathiri watu 3 Kati ya 4 kote duniani.

Shirika hilo linasema suluhu ipo kwenye kuwekeza katika mbinu mujarab za kujenga mnepo wa kuhimili  mabadiliko ya tabia nchi.

Elimu kwa watoto moja ya dawa mujarabu

Njia moja isiyokuwa na gharama kubwa ni kukielimisha kizazi kijacho kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira. 

Eva Makandi ni muasisi wa shirika la Light on A Hill la kuwafunza watoto masuala ya mazingira kwani ndio mwanga wa baadaye na’Watoto wakikua na kujua umuhimu wa kutunza mazingira yao,wakijua umuhimu wa kilimo na kupenda sana kutakuwa na matokeo makubwa kwani tutakuwa na kizazi kinachojua na kupenda mazingira yake.”

Ili kupata picha Kamili ya matunda ya kuhifadhi mazingira, wahusika waliohudhuria kongamano walishiriki kwenye maonyesho ya bidhaa za misitu.

Shughuli za kufuga nyuki kwenye misitu mbalimbali ni dhihirisho kuwa matunda yana manufaa kwa wanajamii.

Kwenye  ufunguzi wa kongamano la kimataifa la mazingira na tabianchi jijini Nairobi, mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuzuia ueneaji wa majangwa, UNCCD, Ibrahim Thiaw, alisisitiza kuwa mazingira ya nyika yana faida tele kinyume na inavyodhaniwa. 

Alibainisha kuwa Afrika ina suluhu ya matatizo ya mazingira kwanizipo mbinu za asili zilizotumika tangu jadi .

Mandhari haya ya kuvutia yalidhihirisha kuwa mazingira yanayolindwa yanamnufaisha mkaazi.

Kongamano la kilele la COP 28 limepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu mjini Dubai. 

Kwa mara ya kwanza UNCCD itakuwa na kibanda chake itakachotumia kutangaza mikakati yake. Joan Lee ni mratibu aliyesimamia masuala ya ushirikiano kwenye kongamano la Nairobi na anafafanua kuwa mengi yameandaliwa, na “Kwenye COP 28 Kwa mara ya kwanza UNCCD Itakuwa na sehemu yake iliyotengewa chini ya mpango wa UFCCC. Tutakuwa na shughuli nyingi zinazowalenga vijana, makundi ya kidini, wanawake, haki za kumiliki ardhi, jamii za kiasili na ufadhili wa sekta ya binafsi.”

 Kikao hiki cha Nairobi kilikusudia kubadili mitazamo na kujikita katika suluhu za matatizo ya mazingira ambazo zinaambatana na hali ya Afrika.