Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro Mashariki ya Kati: Umoja wa Mataifa unasaidia vipi?

Jengo liliporomoka huko Gaza.
© UNRWA/Mohammed Hinnawi
Jengo liliporomoka huko Gaza.

Mgogoro Mashariki ya Kati: Umoja wa Mataifa unasaidia vipi?

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya kazi katika eneo la Mashariki ya Kati muda wote ili kupunguza mzozo wa Israel na Palestina kwa kuwashirikisha wahusika wakuu na kutoa msaada wa dharura kwa raia walioko mashinani. 

Wakati mzozo huo ukiongezeka huku kukiwa na ongezeko la ghasia, kizuizi kamili cha chakula, maji, na huduma muhimu kiliwekwa na Israel huku ripoti zikiibuka kuhusu operesheni za ardhini za Israel huko Gaza, ambako kuna wakazi zaidi ya milioni mbili.

Jengo lililo na makao makuu ya UNRWA Gaza limeharibiwa kwa kiasi kikubwa na mashambulizi yaliyofanyika katika eneo jirani
© UNRWA
Jengo lililo na makao makuu ya UNRWA Gaza limeharibiwa kwa kiasi kikubwa na mashambulizi yaliyofanyika katika eneo jirani

Wakati ofisi za Umoja wa Mataifa huko Gaza zilipata "uharibifu mkubwa" kutokana na mashambulizi ya anga yaliyofanywa karibu na ofisi zake siku ya Jumatatu usiku (O9 Oktoba 2023), mashirika ya UN yalikuwa yakijitahidi kuwasaidia watu walioathirika katika eneo hilo na maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na Ukingo wa Magharibi, kunako kaliwa na wakimbizi 871,000 waliosajiliwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNWRA, kwa sasa lina wafanyakazi 13,000 wa kitaifa na kimataifa, wengi wao wakiwa wakimbizi wenyewe, huko Gaza na karibu 4,000 katika Ukingo wa Magharibi.

Aidha, mamia ya wafanyakazi wa UNRWA waliendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa.

Katika mpaka wa Israel-Lebanon, ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL, unafanya kazi na askari wa ardhini 9,400, wafanyakazi wa kiraia 900, na wafanyakazi wa majini 850 kwenye Kikosi Kazi chake cha Baharini.

Picha za jinsi UN inavyosaidia mashinani:

Familia zimekusanyika kwenye shule ya UNRWA ya New Gaza Boys  wakisaka hifadhi kutokana na mashambulizi
© UNRWA/Mohammed Hinnawi
Familia zimekusanyika kwenye shule ya UNRWA ya New Gaza Boys wakisaka hifadhi kutokana na mashambulizi

 

1. Ulinzi

Mashambulizi makali ya anga tangu Jumamosi yamesababisha takriban watu 190,000 kuyahama makazi yao huko Gaza, hivyo shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, linawahifadhi wanaume, wanawake na watoto 137,500 katika shule 83 kati ya 288, kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya hali ya shirika hilo. Kufikia Jumanne, vituo 18 vya UNRWA vilipata uharibifu wa moja kwa moja kutokana na mashambulizi ya anga, kukiwa na majeruhi na vifo.

2. Kupunguza mapigano

Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati (UNSCO), walikuwa wakizungumza na pande zinazohusika na mzozo huo na wadau wakuu, ikiwa ni pamoja na Marekani, Qatar na Umoja wa Ulaya, ili kupunguza hali hiyo ya mzozo.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Lebanon, UNIFIL, uliendelea kufuatilia hali ya usalama "ambayo iko tete" inayoendelea kwenye mpaka wa Israel-Lebanon, ikitoa mwongozo kwa raia na kuendele kutoa taarifa za mara kwa mara kupitia mitandao ya kijamii.

"Tumeshirikisha kikamilifu mifumo yetu ya mawasiliano na uratibu katika ngazi zote, ili kusaidia kuzuia kutokuelewana kati ya Lebanon na Israeli hali ambayo inaweza kusababisha kuongezeka kwa mzozo," UNIFIL ilisema. "Hili ndilo lengo letu kuu kwa sasa, na tunafanya kazi 24/7 kulikamilisha."

 

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakipiga doria huko El Odeisse, kusini mwa Lebanon.
UNIFIL/Pasqual Gorriz
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakipiga doria huko El Odeisse, kusini mwa Lebanon.

3. Huduma za dharura

Hatua iliyotangazwa ya Israel ya kuzuia chakula, maji, mafuta na umeme huko Gaza siku ya Jumatatu ilikuja huku mashirika ya Umoja wa Mataifa yakionya juu ya uhaba wa chakula na mgogoro unaokuja. Vyoo vinavyohamishika na mabafu vinatumwa kwenye makazi ya UNRWA, inapohitajika. Wapalestina huko Gaza sasa wana umeme kwa saa tatu hadi nne tu kwa siku, jambo linalozuia uwezo wa vituo vya afya kufanya kazi na kuwatibu waliojeruhiwa, hii ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA.

4. Chakula

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani -WFP na UNRWA walikuwa wakiratibu ugawaji wa mikate kwa watu waliokimbia makazi yao huko Gaza. "Takriban watu nusu milioni, au familia 112,000, hazijaweza kupata mgao wao wa chakula wiki hii tangu vituo vya usambazaji wa chakula vya UNRWA vifungwe," UNRWA ilisema.

Kufikia Jumanne, WFP ilianza kusambaza mikate, vyakula vya makopo, na vyakula vilivyo tayari kuliwa kwa watu wapatao 100,000 katika makazi ya UNRWA, huku kukiwa na mipango ya kuwafikia zaidi ya watu 800,000 walioathirika huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.

5. Afya 

Huduma za afya za dharura zinatolewa kupitia simu ya bure katika eneo lote la Gaza. Mfuko wa pamoja wa Umoja wa Mataifa (CBPF) na washirika wake walitoa dawa za kuokoa maisha na dawa za dharura na vifaa vya matibabu vilisambazwa ili kuwezesha mfumo wa afya huko Gaza kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka. Jumla ya wahudumu wa afya 125 wanafanya kazi kwa zamu katika vituo vya afya vya UNRWA, huku kliniki 15 kati ya 22 zinazotoa huduma za afya ya msingi kuanzia saa 9 asubuhi hadi saa 12 jioni kwa wagonjwa waliopewa miadi ya dharura iliyopokelewa kupitia simu ya bure.

Nambari za usaidizi na huduma za kijamii zilianza kufanya kazi kufikia Jumanne, na usaidizi wa kisaikolojia na msaada wa kwanza wa kisaikolojia ulikuwa ukitolewa kwa njia ya mtandao. Shirika  la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wamekuwa na wataalamu wa msaada wa kisaikolojia tayari kutoa msaada kwa wale wanaohitaji huko Gaza na katika Ukingo wa Magharibi. "Jumuiya inaomba UNRWA kufungua vituo vya afya vilivyofungwa kutokana na mahitaji makubwa ya huduma," shirika hilo lilisema.

Shule ya UNRWA inayohifadhi zaidi ya watu 225 waliokimbia makazi yao, ikiwa ni pamoja na familia nyingi, katika Ukanda wa Gaza ilipigwa moja kwa moja, na kupata hasara kubwa, lakini hakuna vifo viliyoripotiwa.
© UNRWA/Mohammed Hinnawi
Shule ya UNRWA inayohifadhi zaidi ya watu 225 waliokimbia makazi yao, ikiwa ni pamoja na familia nyingi, katika Ukanda wa Gaza ilipigwa moja kwa moja, na kupata hasara kubwa, lakini hakuna vifo viliyoripotiwa.

6. Ukanda wa misaada ya kibinadamu

Upatikanaji wa wafanyakazi wa kibinadamu na vifaa vinavyo hitajika katika ukanda wa Gaza ulikatwa wiki hii na ukubwa wa uhasama ulikuwa unazuia uwezo wa wafanyakazi kutoa misaada, kwa mujibu wa Mratibu wa Kibinadamu wa eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu, Lynn Hastings. Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, na washirika wao waliendelea kufanya kazi ili kuanzisha ukanda wa kuwawezesha kuwafikia watu ambao wana uhitaji mkubwa na huduma muhimu huko Gaza.