Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wanaowasili Armenia ikizidi kuongezeka WFP yaongeza usambazaji wa chakula

Wakimbizi wakiwasili Goris, Armenia
WHO
Wakimbizi wakiwasili Goris, Armenia

Idadi ya wanaowasili Armenia ikizidi kuongezeka WFP yaongeza usambazaji wa chakula

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP linaongeza juhudi zake za kuwasaidia watu wanaowasili kwenye mpaka wa Armenia tangu tarehe 23 Septemba, 2023 ambapo takwimu za hivi karibuni zinaonesha idadi ya wakimbizi imefikia 100,000 kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Taarifa ya WFP kutoka Yerevan Armenia imeeleza kuwa idadi ya watu wanaofika mpakani imeongezeka sana katika siku za hivi karibuni, na kusababisha kuongezeka kwa foleni za wanaowasilini mpakani. 

Nanna Skau ambaye ni Mwakilishi na Mkurugenzi wa WFP nchini Armenia amesema “Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu athari kwa maisha ya raia. Wakati hali inavyoendelea, ni muhimu watu walioathirika wapate usaidizi wa kibinadamu kwa wakati na uwe endelevu”.

Miongoni mwa mwanaowasili ni pamoja na wazee na watoto wengi. 

Chakula chamoto

Wale wanaofika mpakani mara nyingi huwa katika hali ya uchovu na wanahitaji msaada wa dharura wa haraka, ikiwa ni pamoja na chakula cha moto na msaada mwingine wa chakula.

WFP imejenga vituo katika eneo la Goris lililo karibu na mpaka katika jimbo la kusini mashariki la Syunik, ili kutoa huduma ya chakula cha moto kwa watu wanaoingia Armenia. 

Zaidi ya milo 2,000 ya moto ilisambazwa kwa watu wanaovuka mpaka siku ya Alhamisi. WFP inapanga kuongeza chakula ili kutoa milo 21,000 katika wiki mbili zijazo.

WFP pia inatoa vifurushi vya chakula vikijumuisha vyakula vyenye protini nyingi, nafaka na mafuta ya kupikia kwa watu 30,000.

Shirika hilo pia liko tayari kutoa kadi za chakula kusaidia zaidi ya watu 6,000 na, kufanya kazi na wadau wengine na wafadhili, ili kuongeza zaidi upatikanaji wa chakula kulingana na mahitaji.