Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gabon: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alaani jaribio la mapinduzi, akiri ukiukwaji wakati wa uchaguzi

Ali Bongo Ondimba, Rais wa Jamhuri ya Gabon, akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Cia Pak
Ali Bongo Ondimba, Rais wa Jamhuri ya Gabon, akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Gabon: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alaani jaribio la mapinduzi, akiri ukiukwaji wakati wa uchaguzi

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali jaribio la mapinduzi nchini Gabon, huku akikiri kwamba "ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa kimsingi" unaonekana kutekelezwa wakati wa uchaguzi uliofanyika nchini humo mwishoni mwa wiki 

Leo Jumatano Agosti 8, jeshi la Gabon limetangaza kunyakua mamlaka katika taifa hilo lenye takribani idadi ya watu milioni 2.4 lililopata uhuru wake mwaka 1960 kutoka kwa Wafaransa.  

Kwa mujibu wa duru mbalimbali, Rais Ali Bongo Ondimba amekamatwa na kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani. Rais Odimba alitwaa mamlaka mwaka 2009 baada ya kifo cha baba yake aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka 42, Omar Bongo Ondimba.  

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini New York, mwakilishi wa Katibu Mkuu amesema kwamba mkuu wa Umoja wa Mataifa "analaani vikali jaribio la mapinduzi linaloendelea kama njia ya kutatua mgogoro wa baada ya uchaguzi." 

UN inaunga mkono watu wa Gabon 

Guterres pia ameomba jeshi la taifa na vikosi vya usalama "kuhakikisha uungwana wa kimwili kwa Rais wa Jamhuri na familia yake." Na kwamba Umoja wa Mataifa unaunga mkono watu wa Gabon. 

Aidha, Guterres ameangazia "wasiwasi mkubwa katika kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huku kukiwa na ripoti za ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa kimsingi." 

Katibu Mkuu Guterres amesisitiza, "upinzani wake mkubwa dhidi ya mapinduzi ya kijeshi." Ametoa wito kwa wote wanaohusika "kutenda kwa kiasi, kushiriki katika mazungumzo jumuishi na yenye maana na kuhakikisha kwamba utawala wa sheria na haki za binadamu zinaheshimiwa kikamilifu." 

Wafanyakazi wa UN Gabon 

Takribani wafanyakazi 776 wa Umoja wa Mataifa kwa sasa wako nchini Gabon na “wote wako salama.” Imeeleza taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Pia amesema kuwa mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika ya Kati, Abdou Abarry, anafanya mawasiliano na washirika wa kikanda na kanda kuhusu mgogoro huo.