Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kambini Kakuma: Zaidi ya watoto 22,000 wanufaika na matibabu ya utapiamlo

Mtoto akipatiwa chakula chenye virutubisho vya lishe.
© UNICEF/Odelyn Joseph
Mtoto akipatiwa chakula chenye virutubisho vya lishe.

Kambini Kakuma: Zaidi ya watoto 22,000 wanufaika na matibabu ya utapiamlo

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya watoto UNICEF nchini Kenya linatekeleza mradi wa matibabu kwa watoto wenye utapiamlo, mradi ambao umeanza kuzaa matunda kwani afya za watoto zimeanza kuimarika. 

Sabina Naboi mwenye umri wa miaka 28 mama wa watoto watatu, alizaliwa ndani ya kambi ya Kakuma iliyoko katika kaunti ya Turkana nchini Kenya.

Misimu sita mfululizo ya ukame uliochochewa na mabadiliko ya tabianchi umekuwa na athari hasi hususan kwenye suala la lishe kwa watu wengi katika kaunti hii ya Turkana na mmoja wao ni Sabina ambaye mtoto wake mwenye umri chini ya miaka mitano alipata utapiamlo.

Changamoto alizopitia Sabina

Sabina anasema,“sisi tunategemea chakula hiki cha msaada wa wakimbizi ambacho tunakipata mara moja kwa mwezi na huwa hatuwezi kufika nacho mwisho wa mwezi mwingine. Wakati nimejifungua binti yangu analia alikuwa sawa lakini alipofika miezi sita akaanza kuumwaumwa mara kuharisha yani afya yake haikuwa sawa. Nilikuwa nampeleka hospitali anapewa dawa lakini mtoto alikuwa anakonda sana.”

Mtoto wa Sabina aligundulika kuwa na utapiamlo na hivyo akapewa lishe maalum kwa ajili ya watoto wenye utapiamlo.

Vicent Opinya ni meneja wa programu ya afya katika kambi ya Kakuma anasema, “tunahudumia takribani watu 246,000 ambapo wahudumu wetu wa afya wanawapatia matibabu ya chakula maalum kilicho tayari kwa ajili ya kutibu watoto walio na utapiamlo mkali bila shida nyingine yoyote katika vituo vyetu vya wagonjwa wanje.”

Mgao wa fedha taslimu, lishe na huduma ya matibabu

Chini ya ufadhili wa Muungano wa Ulaya UNICEF na wadau wake wanatoa lishe, msaada wa fedha taslimu na matibabu kwa watoto wenye upatiamlo waliochini ya umri wa miaka mitano kwa wakazi wa Kalobeyei pamoja na Kambi ya wakimbizi ya Kakuma. Kwa sasa watoto zaidi ya 22,000 wamefikiwa na misaada hiyo ya kuokoa maisha.

Susan Jobando ni Afisa afya wa UNICEF nchini Kenya na anasema mbali na kusaidia serikali ya Kaunti ya kakuma katika masuala ya afya kwa watoto pia wanawajengea uwezo wahudumu wa afya na kuimarisha mfumo wa afya na kuhakikisha kuna mnyororo thabiti wa usambazaji matibabu ya utapiamlo kuweza kumfikia kila mtoto mwenye uhitaji.

Tukiwa na wadau kama ECHO tunaweza kuwafikia watoto wengi zaidi sio tu kama mkakati wa matibabu bali pia ni mkakati wa kujikinga ili waweze kukabiliana vyema na athari za mabadiliko ya tabianchi.”

Tabasamu sasa kwa Sabina

Sasa Sabina ana furaha kwa kuwa mtoto wake ameanza kupata nafuu na anasema, “vile ninaona afya yake iko sawa hata mimi hufurahi. Na ninaamini mwezi ujao mwili wake utarudi kama zamani (atanenepa) na utaendelea kuongezeka mpaka atoke kwenye hiyo programu ( ya kula chakula cha watoto wenye utapiamlo) na aende kwenye programu nyingine . Kila mama anataka mtoto wake awe na afya nzuri, awe na mwili mzuri.”