Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yakaribisha kufunguliwa kwa mpaka wa Bab al-Hawa;  Misaada kupitishwa kwenda Syria

Malori yakiwa yamebeba vifaa muhimu vya misaada ya kibinadamu kutoka Uturuki kuelekea kaskazini-magharibi mwa Syria kupitia mpaka wa Bab al-Hawa.
© UNICEF/PAC
Malori yakiwa yamebeba vifaa muhimu vya misaada ya kibinadamu kutoka Uturuki kuelekea kaskazini-magharibi mwa Syria kupitia mpaka wa Bab al-Hawa.

UN yakaribisha kufunguliwa kwa mpaka wa Bab al-Hawa;  Misaada kupitishwa kwenda Syria

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha maelewano yaliyofikiwa jana kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Syria ya kuendelea kutumia kwa miezi sita ijayo mpaka wa Bab al-Hawa kufikisha misaada ya kibinadamu inayohitajika zaidi kwa mamilioni ya watu kaskazini-magharibi mwa Syria.

 

Taarifa iliyotolewa Jumanne jijini New York, Marekani na Naibu Msemaji wa UN Farhan Haq, inasema hatua hii ya hivi karibuni inafuatia mashauriano kati ya Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya dharura na ya kibinadamu, OCHA Martin Griffiths, na serikali ya Syria pamoja na wadau wake ya kuendelea kufikisha misaada ya kiutu kupitia mpaka huo wa Sri ana Uturuki.

Mpango huo unafanyika kwa kuangalia  uhitaji na unazingatia kanuni inayoruhusu ushiriki wa pande zote kwa lengo la kuona kuna vibali vya kupitisha misaada ya kiutu na ambayo inalinda uhuru wa UN katika operesheni zake.

Katibu Mkuu ameesma ridhaa hiyo iliyopitishwa na Syria hivi karibuni inatoa msingi wa UN na wadau wake kuendesha operesheni zake za kiutu kwa kuvuka mipaka kisheria kupitia mpaka wa Bab al-Hawa.

Halikadhalika amekaribisha hatua ya Syria kuongeza muda wa ridhaa yake kwa UN kutumia mipaka ya Bab al-Salam na Al-Ra’ee kwa kipindi kingine cha miezi mitatu, sambamba na ridhaa ya kuvuka mipaka iliyowekwa ndani ya Syria huko Sarmada na Saraqib kwa ajili ya kufikisha misaada kwa miezi sita ijayo.