Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP, FAO na Fondation Suisse de Déminage kusafisha ardhi kwa ajili ya kilimo Ukraine

Ardhi ya kilimo nchini Ukraine imechafuliwa na mabomu ya ardhini na athari zingine.
© FAO/Viacheslav Ratynskyi
Ardhi ya kilimo nchini Ukraine imechafuliwa na mabomu ya ardhini na athari zingine.

WFP, FAO na Fondation Suisse de Déminage kusafisha ardhi kwa ajili ya kilimo Ukraine

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wamezindua mpango wa pamoja kwa ushirikiano na shirika la FSD (Fondation Suisse de Déminage) kusaidia wakulima wadogo na familia za vijijini zilizoathiriwa zaidi na vita huko nchini Ukraine.

Mpango huo umeundwa ili kuikagua ardhi ya wakulima na kuondoa vilipuzi kama mabomu ambayo yamebaki bila kulipuka na ili baadaye ardhi hiyo irejeshwe kwa wakulima ikiwa salama kwa ajili ya maisha ya kilimo, kuchangia katika kufufua uchumi wa Ukraine, na kumaliza hitaji la msaada wa kibinadamu kwa maelfu ya watu wa familia za vijijini nchini humo. 

Mpango huo tayari umeanza katika eneo la Kharkivska, na baadaye utapanua wigo  hadi katika wilaya za Mykolaivska na Khersonska, ukilenga wakulima wenye mashamba madogo zaidi ya hekta 300 pamoja na familia za vijijini zinazolima chakula kwa matumizi yao wenyewe.

Vita nchini Ukraine imeharibu kilimo na uzalishaji wa chakula, imevuruga minyororo ya usambazaji na mauzo ya nje, imesababisha kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, na kusababisha uchafuzi utokanao na kutapakaa kwa mabomu.

Uzalishaji wa chakula umepungua sana 

Kulingana na tathmini ya uharibifu wa haraka na mahitaji, iliyochapishwa Februari 2023, uzalishaji wa nafaka na mbegu za mafuta nchini Ukraine ulipungua kwa asilimia 37 mwaka wa 2022. 

Takriban asilimia 90 ya wazalishaji wadogo wa mazao waliochunguzwa na FAO nchini Ukraine waliripoti kupungua kwa mapato kutokana na vita na mmoja kati ya wakulima wanne aliripoti kuwa amesimamisha au kupunguza kwa kiasi kikubwa shughuli zake za kilimo.

"Kuifanya ardhi kuwa salama na isiyo na mabaki ya vilipuzi vya vita ni hatua ya kwanza ya kujenga upya jamii za vijijini zenye uwezo na ustawi nchini Ukraine, ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika vita hii, na kuzuia utegemezi wao wa muda mrefu wa msaada wa kibinadamu," amesema Denise Brown, Mratibu wa  masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine.

Pierre Vauthier, mkuu wa FAO nchini Ukraine amesema "Familia nyingi na wakulima wadogo katika maeneo ya mstari wa mbele hawapandi msimu huu kwa sababu wanajua mashamba yao ni hatari au wanahatarisha maisha yao kwa kupanda kwenye ardhi yenye mabomu au udongo uliochafuliwa. Tunatarajia kwamba ukarabati wa ardhi, urekebishaji na mbinu za uhifadhi unaofanywa utasaidia watu kurudi kwenye kilimo, na kurejesha maisha ya vijijini huku wakisaidia kuendeleza uzalishaji wa kilimo wa Ukraine."

Naye Matthew Hollingworth, mwakilishi wa WFP na mkurugenzi  wa shirika hilo nchini Ukraine kwa upande wake amesema "Bila ya hatua za dharura, uzalishaji wa kilimo nchini Ukraine utaendelea kuporomoka, na matokeo ya moja kwa moja katika uhakika wa chakula na mlo tofauti nchini humo, na madhara yanayoweza kujitokeza katika masoko ya kikanda na kimataifa." 

Mchakato wa mradi huo

FAO, WFP na FSD kwa uratibu wa karibu na jamii, mamlaka za mitaa na wizara ya sera ya kilimo na chakula ya Ukraine, kwanza zitatambua na kuweka ramani ardhi zinazohitaji kuondolewa mabomu kwa kutumia picha za satelaiti. 

Katika awamu ya pili, timu za uteguaji mabomu zitachunguza na kusafisha ardhi kwa kutegua mabomu na mabaki mengine ya vifaa vya milipuko ya vita, na kuweka kipaumbele kwa viwanja ambavyo vinaweza kusafishwa haraka na kazi ndogo ya kibali. 

Katika awamu ya tatu, FAO na FSD zitapima ardhi ili kutathmini uchafuzi wa mazingira unaoachwa nyuma na silaha zilizolipuka. 

FAO na WFP zitachunguza kwa wakati mmoja wakulima wadogo na familia za vijijini juu ya aina ya pembejeo na rasilimali wanazohitaji ili kuanzisha upya uzalishaji wa kilimo, na watatoa msaada wa moja kwa moja au fedha taslimu inapowezekana.

Hadi sasa, mradi huo wa dola milioni 100 unakabiliwa na pengo la ufadhili la dola milioni 90. 

FAO na WFP zinakadiria uokoaji wa kila mwaka wa hadi dola milioni 60 katika usaidizi wa moja kwa moja wa chakula kwa jamii za vijijini. 

Mradi huo umepigwa jeki na mfuko wa masuala ya kibinadamu wa Ukraine, mfuko wa pamoja wa Umoja wa Mataifa, pamoja na wafadhili wa binafsi.