Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wadau wa kibinadamu wahitaji dola milioni 194.2 kuisaidia Burundi 2023: OCHA

Mtu akitembea katika maji ya mafuriko huko Gatumba, Burundi eneo ambalo linapokea mvua zisizotabirika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
© UNICEF/Karel Prinsloo
Mtu akitembea katika maji ya mafuriko huko Gatumba, Burundi eneo ambalo linapokea mvua zisizotabirika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Wadau wa kibinadamu wahitaji dola milioni 194.2 kuisaidia Burundi 2023: OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Wadau wa masuala ya kibinadamu kwa kushirikiana na serikali ya Burundi leo wamezindua ombi la pamoja wakihitaji dola milioni 194.2 kwa ajili ya kushughulikia mahitaji ya kibinadamu nchini humo kwa mwaka huu wa 2023.

Ombi hilo lililozinduliwa mjini Bujumbura Burundi katika hafla maalum iliyoandaliwa na serikali ya Burundi na wadau wa kimataifa linadhihirisha ushirikiano wa muda mrefu baina ya jumuia ya misaada ya kibinadamu na serikali ya nchi hiyo na linalenga watu milioni 1.5 watakaohitaji msaada wa kibinadamu kwa mwaka huu wa 2023 na watu milioni 1.1 miongoni mwao ni wale walio hatarini wanaohitaji msaada maalum.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA Burundi iko katika hatari kubwa ya mabadiliko ya taianchi na majanga ya asili yamesababisha wimbi kubwa la watu kutawanywa.

Kaimu mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi John Agbor amesema  Hatua zetu za kibinadamu kwa Burundi mwaka 2023 ni matokeo ya uchambuzi wa kina wa mahitaji na changamoto zinazowakabili watu walio hatarini zaidi. Kwa pamoja, tukishirikiana na Serikali, washirika wa kibinadamu na wa maendeleo, tunaweza kufanya kazi kufikia suluhisho endelevu ili kuboresha hali ya maisha ya watu hawa na kujenga mustakabali thabiti zaidi. Sote tumeunganishwa na sababu moja, kuokoa maisha na kutomwacha mtu yeyote nyuma.”

Mwaka 2021 na 2022, changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na janga la coronavirus">COVID-19, milipuko ya magonjwa, na vita nchini Ukraine, vilizidisha mahitaji yaliyopo ya kibinadamu, na kuathiri idadi ya watu walio hatarini kama vile wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao.

OCHA imeongeza kuwa rasilimali za kutosha, zinazolingana na mpango wa hatua, bado ni changamoto.

Iwapo halitashughulikiwa, ukosefu wa ufadhili unaweza kuwa na madhara makubwa, na kuwaacha watu walio hatarini kukabili hatari za mabadiliko ya tabianchji, magonjwa, na hatari za kutokuwa na ulinzi na hivyo kuhatarisha juhudi za kuwarudisha nyumbani na Maisha yao. Pia kuvunja mzunguko wa janga la magonjwa itakuwa vigumu bila hatua za dharura ya afya na msaada wa maji, usafi wa mazingira na kujisafi. Limesisitiza shirika hilo.

Kushughulikia mahitaji ya kibinadamu Burundi ni muhimu sana na kwa kushauriana na Serikali, jumuiya ya misaada ya kibinadamu inaongoza harakati za misaada tangu 2016 ili kushughulikia mahitaji muhimu ya watu walioathirika na mwaka jana pekee watu 673,714 walipokea msaada wa kibinadamu ikiwa ni asilimia 71 ya lengo la awali.

Hata hivyo OCHA inasema bado kulikuwa na pengo kubwa la ufadhili la karibu asilimi 50 hali ambayo iliathiri kiwango cha msaada wa kibinadamu uliotolewa.