Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwakataza wanawake kufanya kazi kwenye NGOs kutawaathiri Waafghan wote: Turk

Msichana akiwa katika mazingira salama kwa ajili ya wakimbizi wa ndani Herat Afghanistan
© UNOCHA/Sayed Habib Bidel
Msichana akiwa katika mazingira salama kwa ajili ya wakimbizi wa ndani Herat Afghanistan

Kuwakataza wanawake kufanya kazi kwenye NGOs kutawaathiri Waafghan wote: Turk

Wanawake

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk ametoa wito kwa mamlaka nchini Afghanistan kufuta mara moja mtiririko wa sera zinazolenga haki za wanawake na wasichana, nchini humo akieleza kuwa zina "athari mbaya na za uharibifu" na zinaleta mvurugano katika jamii.

Kauli hii inafuatia matangazo yaliyotolewa wiki iliyopita ambapo tarehe 24 Mwezi huu wa Desemba uongozi wa Taliban ulitoa amri ya kupiga marufuku wanawake kufanya kufanya kazi katika mashirika yasiyo ya kiserikali, NGOs. Tayari pia uongozi huo ulishapiga mafuruku hivi karibuni wanawake na wasichana kupata elimu ya Chuo Kikuu.

Kamishna Turk amesema “Hakuna nchi inayoweza kuwa na maendeleo ya kweli ya kijamii na kiuchumi wakati ikitenga nusu ya watu wake. Vizuizi hivi visivyoeleweka vilivyowekwa kwa wanawake na wasichana sio tu vitaongeza mateso ya Waafghan wote lakini, ninaogopa, kwani vinaleta hatari mpaka nje ya mipaka ya Afghanistan.”

Mkuu huyu wa ofisi ya Haki za Binadamu ameongeza kuwa amri hii iliyotolewa hivi karibuni itakuwa na matokeo mabaya kwa wanawake wote wa Afghanistan “Kupiga marufuku wanawake kufanya kazi katika NGOs kutawanyima wao na familia zao mapato yao, na haki yao ya kuchangia vyema katika maendeleo ya nchi yao na ustawi mzima wa raia wenzao.”

Kundi la wasichana wanafunzi wakiwa darasani  kwenye shule ya sekondari jimboni Nurstan Afghanistan
© UNICEF/Sayed Bidel
Kundi la wasichana wanafunzi wakiwa darasani kwenye shule ya sekondari jimboni Nurstan Afghanistan

Wanawake wafanyakazi kwenye NGOs

NGOs na mashirika ya kibinadamu hutoa huduma muhimu za kuokoa maisha kwa watu wengi nchini Afghanistan, wanafanya kazi za kutoa chakula, maji, usaidizi wa makazi na huduma za afya.

Kuna maeneo ambayo ni wanawake pekee ndio wanajishughulisha kama vile huduma za kabla na baada ya kujifungua na watoto wachanga, hutolewa na wanawake pekee.

Wafanyakazi wengi wanaofanya kazi katika NGOs hizi ni wanawake na mashirika mengi yana wanawake katika nafasi za uongozi. Wanawake ni washirika muhimu kwa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine katika utekelezaji wa programu za kibinadamu na maendeleo kote nchini.

"Marufuku hiyo ya wanawake kutofanya kazi kwenye NGOs itadhoofisha kama sio kuharibu kwa kiasi kikubwa uwezo wa NGOs hizi kutoa huduma muhimu ambazo Waafghan wengi walio katika mazingira magumu wanategemea. Inasikitisha zaidi kutokea wakati huu ambapo ni msimu wa majira ya baridi nchini Afghanistan na mahitaji ya kibinadamu ni makubwa zaidi. Kazi ambayo mashirika haya yasiyo ya kiserikali hufanya ni muhimu zaidi,” Türk aliongeza.

Kamishna Mkuu pia alimeonesha wasiwasi mkubwa kwamba kuongezeka kwa ugumu wa maisha katika jamii ya Afghanistan kuna uwezekano wa kuongeza hatari ya wanawake na wasichana kukabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji wa majumbani.

"Wanawake na wasichana hawawezi kunyimwa haki zao za asili. Majaribio yanayofanywa na mamlaka Taliban kuwafanya wanawake kuwa kimya na wasionekane hayatafanikiwa, yataleta madhara kwa Waafghan wote, kuwazidishia mateso na kuzuia maendeleo ya nchi. Sera kama hizo haziwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote," Türk alisema wakati akihitimisha taarifa yake.