Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu mkazi wa UN Burkina Faso atangazwa kuwa persona non grata, UN yasikitishwa

Mratibu mkazi na wa masuala ya kibinadamu wa UN nchini Burkina Faso Barbara Manzi akizungumza na wakimbizi wa ndani katika makazi ya 38 Villas ya wakimbizi wa ndani Kaya Burkina Faso
© IOM Burkina Faso/Carine Bonduelle
Mratibu mkazi na wa masuala ya kibinadamu wa UN nchini Burkina Faso Barbara Manzi akizungumza na wakimbizi wa ndani katika makazi ya 38 Villas ya wakimbizi wa ndani Kaya Burkina Faso

Mratibu mkazi wa UN Burkina Faso atangazwa kuwa persona non grata, UN yasikitishwa

Amani na Usalama

Serikali ya mpito nchini Burkina Faso jana imemtangaza mratibu mkazi na mtratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini humo na ambaye pia ni afisa wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya usalama kuwa ni “persona non grata” yaani mtu aiyekubalika au kutakiwa nchini humo.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini New York Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ana Imani kuwa na mfumo wa Umoja wa Mataifa nchini Burkina Faso pamoja na dhamira na utendaji kazi wa Bi. Barbara Manzi ambaye ametangagwa kutotakiwa nchini humo.

Katibu Mkuu ameendelea kusema kwamba “mfumo wa Umoja wa Mataifa unaoongozwa na mratibu huyo Bi. Manzi umekuwa ukijitolea kufanyakazi na serikali ya mpito ya Burkina Faso ili kusaidia juhudi za maendeleo na kutoa msaada wa kibinadamu unaohitajika.”

Taarifa hiyo ya Antonio Guterres imesema kanuni za persona non grata hazitumiki kwa maafisa wa Umoja wa Mataifa. 

Chini ya ibara ya 100 na 101 ya mkataba wa Umoja wa Mataifa, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanateuliwa na Katibu Mkuu, na wanawajibika tu kwa shirika na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinajitolea kuheshimu tabia zao za kimataifa pekee.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 105 cha mkataba huo, shirika limepewa upendeleo na kinga, ikiwa ni pamoja na haki ya wafanyakazi wake kubaki Burkina Faso ili kufanya kazi zao kwa niaba ya shirika. 

Katibu Mkuu pekee, kama afisa mkuu wa utawala wa shirika, ndiye mwenye mamlaka ya kuamua, baada ya uchunguzi wa kina, kuhusiana na kujiondoa kwa afisa yeyote wa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu anasisitiza dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kushirikiana na mamlaka ya mpito nchini Burkina Faso kusaidia nchi hiyo na watu wake.