Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto watumikishwa kwenye mashamba ya tumbaku Malawi: OHCHR

Mwanamke akivuna tumbaku nchini Malawi
© ILO/Marcel Crozet
Mwanamke akivuna tumbaku nchini Malawi

Watoto watumikishwa kwenye mashamba ya tumbaku Malawi: OHCHR

Haki za binadamu

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameeleza wasiwasi wao juu ya idadi kubwa ya watoto wanaotumikishwa kwenye mashamba ya tumbaku nchin Malawi, wakitaka serikali na kampuni za tumbaku zinazoendesha shughuli zao nchini humo kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa kwenye mnyororo mzima wa kilimo cha zao hilo.

Wataalamu hao wamesema hayo katika taarifa yao waliyoitoa leo huko Geneva, Uswisi wakiongeza kuwa “licha ya kutokomezwa kwa mfumo wa unyarubanja, bado kuna hofu kubwa juu ya uhusiano kati ya wenye mashamba na wafanyakazi na hatari ya watoto kusafirishwa au kutumikishwa mashambani.”

Wamesema katika nchi ambako kampuni za tumbaku zimejikita, lazima ziimarishe hatua zao za kuzuia usafirishaji haramu wa watoto kwa lengo la kuwatumikisha watoto au kulazimisha watu kufanya kazi.

Tayari mazungumzo yameanza na kampuni za tumbaku

Ili kufanikisha hatua hizo, wataalamu hao wamesema tayari wameanza mazungumzo na baadhi ya kampuni kubwa za tumbaku kwenye sekta hiyo nchini Malawi ikizitaja kuwa ni Pamoja na Britisha American Tobacco, Imperial, Philip Morris International na  Japan Tobacco Group baada ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kuripotiwa kwenye sekta hiyo ya kilimo cha tumbaku.

Wataalamu wamesema Zaidi ya watu wazima 7,000 na watoto 3,000 wamekumbwa na ukiukwaji wa haki kwenye mashamba ya tumbaku nchini Malawi.

Mara nyingi mashamba hayo yako maeneo ya ndani ambako si rahisi wahusika kupatiwa msaada kuhusu haki zao za kazi halikadhalika ulinzi, na vile vile hatua za kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu ni dhaifu,” wamesema wataalamu hao.

Wamefafanua kuwa kitendo cha mashamba hayo kuwa mbali na makazi kina madhara kwa watoto kuweza kupata elimu au kwenda shuleni.

Baada ya janga la coronavirus">COVID-19 imeripotiwa kuwa Zaidi ya watoto 400,000 hawajarejea shuleni, “idadi kubwa ya watoto wanaotumikishwa kwenye mashamba ya tumbaku bado hawajarejea shuleni.”

Kuna hatua lakini hazitoshelezi

Wataalamu hao wametambua juhudi za serikali ya Malawi na baadhi ya kampuni za tumbaku za kuanzisha mpango wa mlo shuleni na kulipia watoto gharama za shule, “lakini hatua hizo bado hazitoshelezi.”

Wametoa wito kwa kuimarishwa kwa mifumo ya ufuatiliaji, usimamizi wa sheria na wajibu wa sekta ya biashara ili kuzuia ukiukwaji wa haki na ukatili na hatimaye kuhakikisha kuwa kanuni za ajira ziko na zinazingatiwa.