Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuendeleze mazungumzo na wataliban Afghanistan: Mwakilishi wa UN

Watoto katika kambi za wakimbizi wa ndani nchini Afghanistan
© UNICEF/Omid Fazel
Watoto katika kambi za wakimbizi wa ndani nchini Afghanistan

Tuendeleze mazungumzo na wataliban Afghanistan: Mwakilishi wa UN

Amani na Usalama

Licha ya misimamo tofauti kati ya serikali inayoongozwa na wataliban nchini Afghanistan, na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini humo, UNAMA, lazima tuendelee na mazungumzo kwa maslahi ya wananchi wa taifa hilo la Asia, amesema Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA wakati akihutubia Baraza la Usalama Jumanne ya tarehe 20 Desemba 2022.

Roza Otunbayeva ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuwa Mwakilishi wa Maalum wa UN na pia mkuu wa UNAMA amesema mazungumzo hayo ni muhimu yaendelee kwa kuzingatia changamoto zinazokumba wananchi ikiwemo kisiasa na kwenye haki za binadamu bila kusahau maendeleo chanya tangu watalibani watwae madaraka mwezi Agosti mwaka 2021.

“Hatuketi uso kwa uso na watalibani kujadili masuala kadhaa, lakini suala la msingi ni, na linalopaswa kuzingatiwa ni kuendeleza mashauriano kwa matumaini ya kwamba kutakuweko na ‘kesho bora’ ambamo kwayo kila mtu, wakiwemo wanawake, watoto wa kike, wavulana na wasichan wanaweza kuishi maisha yenye utu na usawa.

Roza Otunbayeva, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini Afghanistan, akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali ya usalama nchini humo
UN /Eskinder Debebe
Roza Otunbayeva, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini Afghanistan, akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali ya usalama nchini humo

Maisha dhalili, wananchi wanalalamika hawajui kesho yao itakuwa vipi

Bi. Otunbayeva aliteuliwa mwezi Septemba mwaka huu na tangu wakati huo ametembelea takribani Afghanistan yote ambapo amesema, “kile kilichonishtua zaidi ni maisha dhalili ya wananchi wengi wa Afghanistan ambao wanaishi katika lindi la umaskini na hawana uhakika na maisha yao.”

Anesema wakati wa ziara yake hiyo, watu wengi walimjulisha kuwa maisha hayana uhakika wa kesho.

Ingawa watalibani wanadhibiti taifa la Afghanistan hawana uwezo wa kudhibiti vikundi vya kigaidi vinavyoendesha shughuli zao nchini humo, amesema Mkuu huyo wa UNAMA.

Hivi karibuni, kundi la kigaidi linalojiita , Islamic State –Khorasan au kwa kifupi (ISKP), ambalo lina ushirika na kikundi cha kigaidi cha Daesh, kilifanya mashambulizi dhidi ya ofisi za ubalozi za Urusi na Pakistani pamoja na hoteli moja ambayo huwa inakaribisha raia wengi kutoka China.

Kwa sasa amesema watalibani wanapata upinzani kidogo kutoka ndani ya nchi hiyo na wamekataa kufanyika kwa mazungumzo baina ya waafghanistan ingawa Umoja wa Mataifa unaendelea kushawishi kuweko kwa mashauriano mapana na yewenye uwakilishi mpana.

Wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa hali ya kibinadamu nchini Afghanistan
UNAMA/Shamsuddin Hamedi
Wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa hali ya kibinadamu nchini Afghanistan

Wanawake hawana uhuru

Wataliban ambao wako madaraka baada ya kujitwalia madaraka badala ya kuweko kisheria, wameendelea kutekeleza sera katili za kijamii ikwemo maagizo yanayohatarisha mustakabali wa wanawake, ikiwemo kuwadhibiti ushiriki wao kijamii na kisiasa.

“Kuzuiwa kwao kusoma elimu ya sekondari kutamaanisha katika miaka miwili ijayo hakutakuweko na wasichana Vyuo Vikuu. Uamuzi huu hauungwi mkono kwa kiasi kikubwa miongoni mwa waafghanistan, na halikadhalika miongoni mwa baadhi ya uongozi wa watalibani,” amesema Bi. Otunbayeva.

Mwezi uliopita, kiongozi wa watalibani Afghanistan, Haibatullah Akhunzada aliagiza majaji kutekeleza adhabu za kifo kwa kunyongwa halikadhalika, adhabu ya viboko pale inapobidi kwa mujibu wa sheria ya kiislamu, Sharia.

Ingawa hukumu hizo zimeanza kutolewa tangu watalibani watwae madarakani, kitendo cha mtu kunyongwa mbele ya umma kilifanyika tarehe 7 mwezi huu wa Desemba na kuhudhuriwa na maafisa waandamizi.

Mkuu huyo wa UNAMA ameeleza "nimesisitiza kwa mamlaka hizo za watalibani kuwa hukumu ya kifo ni kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu."

“Ni dhahiri kuwa kuna tofauti kubwa juu ya misimamo ya masuala kadhaa kati ya UNAMA na mamlaka za watalibani,” amesema Mwakilishi huyo Maalum wa Katibu Mkuu nchini Afghanistan.