Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa Misaada wa UN ziarani nchini Ukriane

Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths wakiwa huko Irpin, Ukraine tarehe 7 Aprili 2022
© UNOCHA/Saviano Abreu
Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths wakiwa huko Irpin, Ukraine tarehe 7 Aprili 2022

Mkuu wa Misaada wa UN ziarani nchini Ukriane

Msaada wa Kibinadamu

Mkuu wa masuala ya kibinadamu na mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths ameanza ziara ya siku nne nchini Ukraine ambapo anatarajia kukutana na viongozi wa serikali, washirika wa misaada ya kibinadamu na wananchi walioathirika na vita nchini humo.

Akiwa ameambatana na Mratibu wa misaada nchini Ukraine Denise Brown, Bwana Griffiths atatembelea maeneo mbalimbali kujionea namna misaada ya kibinadamu ilivyosaidia nchini humo pamoja na changamoto mpya zilizojitokeza kutokana na uharibifu wa miundombinu hasa katika kipindi hiki cha msimu wa baridi.

Misaada ya UN imefanya nini?

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti leo kwenye tovuti ya ofisi ya Griffiths ambaye pia ni Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA imesema akiwa katika mji wa Mykolaiv, ulioko kusini mwa Ukraine, atatembelea eneo linalohifadhi wakimbizi wa ndani pamoja na kiwanda cha mikate kinachofadhiliwa na Umoja wa Mataifa ambacho kinazalisha mikate kwa ajili ya watu wa jiji la Kherson.

“Kuanzia hapo, ataelekea Kherson, ambako ataona jinsi Umoja wa Mataifa na mamlaka za mitaa zinavyoanzisha maeneo ambayo watu wanaweza kwenda kupata joto na usalama kwani wamepoteza joto, umeme na maji katika nyumba zao,” imeeleza taarifa hiyo

Mkuu huyo wa OCHA katika siku za mwisho za safari yake atazuru mji mkuu, Kyiv, ambako atakutana na maafisa wakuu wa Serikali, pamoja na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali na jumuiya ya kidiplomasia.

Vita Ukraine

Kwa zaidi ya miezi tisa tangu vita vya Ukraine kuanza, takriban watu milioni 18 ambao ni karibu asilimia 40 ya idadi ya watu wote wa nchi ya Ukraine wamekuwa na uhitaji wa misaada ya kibinadamu.

Matukio yaliyotokea hivi karibuni ya mashambulio dhidi ya miundombinu ya nishati yanawaacha mamilioni ya watu bila joto, maji safi au umeme majumbani mwao wakati huu ambao ni msimu wa baridi.

Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kibinadamu, mengi yakiwa yasiyo ya kiserikali nchini Ukraine, yamefanikiwa kuwafikia zaidi ya watu milioni 13.5 wenye uhitaji wa misaada muhimu tangu kuanza rasmi kwa vita nchini humo tarehe 24 Februari, 2022.