Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manusura wa ugaidi waitaka UN ihakikishe hakuna eneo linakuwa rafiki kwa ugaidi

Moishe Holzberg akiwa na Mama mlezi wake Sandra Samuel ambaye kwa ujasiri mkubwa alimwokoa wakati wa shambulio la kigaidi Tah Mahal Palace Hotel mwaka 2008 nchini India. Wakati huo Moishi alikuwa na umri wa miaka miwili.
Picha kwa hisani ya Moishe Holzberg
Moishe Holzberg akiwa na Mama mlezi wake Sandra Samuel ambaye kwa ujasiri mkubwa alimwokoa wakati wa shambulio la kigaidi Tah Mahal Palace Hotel mwaka 2008 nchini India. Wakati huo Moishi alikuwa na umri wa miaka miwili.

Manusura wa ugaidi waitaka UN ihakikishe hakuna eneo linakuwa rafiki kwa ugaidi

Amani na Usalama

“Ombi langu kwa wawakilishi wote wa nchi wahakikishe hakuna eneo lolote linakuwa salama kwa ugaidi,” amesema Nidhi Chaphekar, manusura wa shambulio la kigaidi la mwaka huko Brussels nchini Ubelgiji. Kauli  yake hiyo ameitoa huko India hii leo Ijumaa wakati wa ufunguzi wa mkutano maalum wa Kamati ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na ugaidi.

Mkutano huo umeanza kwenye mji wa Mumbai, India kwenye hotel ya Taj Mahal Palace ambayo mwezi Novemba mwaka 2008 ilikumbwa na mfululizo wa mashambulio a kigaidi yaliyosababisha vifo vya watu 31 na wengine wengi walijeruhiwa.

Miongoni mwa manusura ni Karambir Kang, ambaye alitoa ushuhuda wake kwenye mkutano huo ambako  maoni na mahitaji ya manusura wa ugaidi yalipazwa kwa sauti na dhahiri.

Kwa sasa Bwana Kang ni miongoni mwa wafanyakazi wa hoteli hiyo, na anakumbuka fika tukio lilivyokuwa, ambapo mkewe na mtoto wake wa kiume waliuawa halikadhalika wafanyakazi wenzake.

‘Nyumba yetu ilishambuliwa’

“Tulihisi nyumba yetu imeshambuliwa. Kwa hiyo tulikata kuilinda. Taj Mahal ni mnara wetu wa upendo. Ugaidi si kitu kinatokea kwa watu wengine na sehemu nyingine. Ni jambo la kihalisia, na linaweza kumtokea mtu yeyote yule,” amesema Bwana Kang.

Akiwa manusura, anasistiza kuwa “kitendo changu cha kuonesha kutokukubali,” kilikuwa ni kujenga tena hoteli ndani ya miezi 18.

“Kwa hiyo nasihi Baraza la Usalama kupinga vitendo vya kigaidi kwa kushirikiana, kuazimia dhidi ya ugaidi.”

Mohse, alikuwa na umri wa miaka miwili wakati wa tukio la shambulio. Sasa hivi naye ni manusura na aliokolewa na dada mlezi na sasa Moshe anaishi Israel na babu na bibi yake. Mama na baba yake walipigwa risasi na kuuawa wakati wa shambulio hilo la kigaidi.

“Mkutano wenu hapa Mumbai ni muhimu sana. Ni muhimu sana mpate njia mpya za kukabili ugaidi, ili mtu mwingine yeyote asipitie tena kile nilichopitia,” alitoa wito huo Moshe kupitia ujumbe wake kwa wajumbe kwa njia ya video.

“Sisi ni manusura wa shambulio dhidi ya ubinadamu”

Ufunguzi wa mkutano huo ulifanyika  kwenye hoteli hiyo ya Taj Mahal kukumbuka waliopoteza maisha na washiriki walikuwa wajumbe wa sasa wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la UN pamoja na wapya ambao wataanza jukumu lao mwakani.

Mwenyekiti wa Kamati, Balozi Ruchira Kamboj wa India, amesisitiza kuwa shuhuda hizo ni muhimu kuonesha jamii ya kimataifa madhara ya vitendo vya kigaidi na mnepo wa manusura.

“Jambo moja linalosalia kwetu sisi manusura ni machungu,” amesema Bi. Chaphekar. “Sisi tu manusura wa shambulio la ubinadamu.”

Katibu Mkuu wa UN Anónio Guterres, wiki iliyopita alizuru hoteli hiyo ya Taj Mahal Palace ambapo katika hotuba yake alirejelea mashambulio hayo na kusema, “ugaidi ni ubaya na hauna nafasi katika dunia ya leo.”

Ameongeza kuwa, “kupinga ugaidi lazima iwe kipaumbele cha dunia n ani kipaumbele cha kati cha hatua za Umoja wa Mataifa.”

Sura tofauti za ugaidi

Baada ya ufunguzi, wajumbe wa kamati walijadili mada kuu ya mkutano huo maalum ambayo ni jinsi teknolojia inatumika vibaya kusambaza vitisho na ugaidi. Waliwasilisha hofu zao na walipata taarifa kutoka kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Mtu anapofikiria utaidi, taswira inayokuja mara nyingi ni mashambulio makubwa yanayofanywa na vikundi vyenye misimamo mikali hasa dhidi ya raia.

Hata hivyo teknolojia imefichua sura mpya ya ugaidi ambayo inasogeza karibu mashambulio yasiyoonekana kwa kubonyeza tu kitufe kimoja.

Kesho jumamosi kwenye mji mkuu wa India, New Delhi kufanyika mijadala mbalimbali kuhusu ufadhili wa ugaidi, matumizi ya ndege zisizo na rubani au droni kwenye mizozo na umuhimu wa kuzingatia kanuni za haki wakati wa vita dhidi ya ugaidi.

David Scharia, Mkuu wa kitengo katika Kamati hiyo ya kukabili ugaidi amesema mkutaono utarajia kufanikiwa katika kufikia uelewa wa jinsi ya kuweka mizania ya faida na hatari za ugunduzi mpya wa kiteknolojia.