Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yazindua mpango mpya wa kukomesha kusambaa kwa uvamizi wa mbu wa malaria barani Afrika

Mbu aina ya Anopheles akiwa kwenye chandarua. Mbu huyu ndiye aenezaye ugonjwa wa Malaria.
© WHO/S. Torfinn
Mbu aina ya Anopheles akiwa kwenye chandarua. Mbu huyu ndiye aenezaye ugonjwa wa Malaria.

WHO yazindua mpango mpya wa kukomesha kusambaa kwa uvamizi wa mbu wa malaria barani Afrika

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO leo limezindua mpango mpya unaolenga kukomesha kuenea zaidi kwa mbu vamizi wa malaria barani Afrika. 

Kwa mujibu wa ripoti ya tahadhari ya mbu wa malaria iliyotolewa  mwaka 2019, WHO ilibainisha kuenea kwa mmbu aina ya Anopheles stephensi ni tishio kubwa kwa kjuhudi za kudhibiti na kutokomeza malaria hasa katika Afrika, ambako ugonjwa huo unaathiri zaidi.  

Mbu hao kwa asili hupatikana zaidi  sehemu za Asia Kusini na rasi ya Arabia, lakini sasa Anopheles stephensi wamekuwa wakipanua wigo wake katika muongo uliopita, ambapo kubainika kwake kuliripotiwa nchini Djibouti (2012), Ethiopia na Sudan (2016), Somalia (2019) na Nigeria (2020).  

WHO inassema tofauti na mbu wengine waenezaji kuu wa malaria barani Afrika, mbu hawa hustawi katika mazingira ya mijini. 

Kuenea kwa mbu Anopheles stephensi Africa 

WHO imeonya kwamba wakati zaidi ya asilimia 40 ya watu barani Afrika wakiishi katika mazingira ya mijini, uvamizi na kuenea kwa mbu wa Anopheles stephensi kunaweza kuleta tishio kubwa kwa udhibiti na kutokomeza ugonjwa wa malaria katika ukanda huo.  

Na limeongeza kuwa ufuatiliaji mkubwa wa mbu hao bado uko katika hatua ndogo za awali na utafiti zaidi na takwimu vinahitajika haraka. 

Dkt. Jan Kolaczinski, anayeongoza kitengo cha kudhibiti na kupambana na usugu wa viuatilifu katika mpango wa kimataifa wa Malaria wa WHO amesema "Bado tunajifunza kuhusu uwepo wa Anopheles stephensi na jukumu lake katika maambukizi ya malaria barani Afrika. Ni muhimu kusisitiza kwamba bado hatujui ni umbali gani aina ya mbu  hawa tayari wameenea, na ni shida gani ambazo wameleta au wanaweza kusababisha." 

Lengo la mpango huo mpya wa WHO 

Mpango huo mpya wa WHO unalenga kuunga mkono hatua madhubuti za kikanda dhidi ya mbu wa Anopheles stephensi katika bara la Afrika kwa kutumia mbinu tano: 

• Mosi: kuongeza ushirikiano miongoni mwa sekta mbalimbali na mipakani 

•Pili: kuimarisha ufuatiliaji ili kubaini ukubwa wa kuenea kwa Anopheles stephensi na jukumu lake katika maambukizi; 

• Tatu:  kuboresha ubadilishanaji wa taarifa juu ya uwepo wa Anopheles stephensi na kuhusu juhudi za kuwadhibiti; 

• Nne: kuandaa mwongozo wa programu za kitaifa za kudhibiti malaria kuhusu njia zinazofaa za kukabiliana na Anopheles stephensi 

• Tano: kutoa kipaumbele katika utafiti ili kutathmini athari za uvamizi huo na nyezo zakudhibiti Anopheles stephensi 

Hatua jumuishi ni ufunguo wa mafanikio 

Who imesisitiza kuwa inapowezekana, hatua za kitaifa dhidi ya Anopheles stephensi inapaswa kuunganishwa na juhudi za kudhibiti malaria na magonjwa mengine yanayoenezwa na wadudu, kama vile homa ya kidingapopo, homa ya manjano na chikungunya.  

Hatiza za kudhibiti mbu zilizowekwa na WHO kwa mwaka 2017–2030 zinatoa mfumo wa kuchunguza na kutekeleza ushirikiano huo. 

"Hatua jumuishi zitakuwa muhimu kwa mafanikio dhidi ya Anopheles stephensi na magonjwa mengine yanayoenezwa na wadudu. Kubadilisha mwelekeo wetu kwa udhibiti wa mbu kuwa jumuishi na uliobadilishwa kuendana na mazingira unaweza kusaidia kuokoa pesa na maisha," amesema Dkt. Ebenezer Baba, mshauri wa malaria katika Kanda ya Afrika ya WHO. 

Kufuatilia kuenea kwa Anopheles stephensi 

Ramani ya Who ya vitisho vya Malaria ina sehemu maalum ya vidudu vamizi, ikijumuisha Anopheles stephensi.  

Ripoti zote zilizothibitishwa za uwepo wa Anopheles stephensi zinapaswa kuripotiwa kwa WHO ili kuruhusu ushiriki wa wazi wa takwimu na uelewa wa kisasa wa usambaaaji na kuenea kwake.  

Ujuzi huu hatimaye utatoa msingi wa kutathmini ufanisi wa juhudi zozote za kudhibiti au kukomesha  mbu aina ya Anopheles stephensi.