Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA DRC yatiwa hofu na ghasia Maï-Ndombe na Kwilu

Angela N'Habimana mwenye umri wa miaka 67 akiwa na mjukuu wake aitwaye Réponse kwenye kituo cha kijamii cha Kiwanja katika eneo la Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC baada ya kukimbia mashambulizi kwenye makazi yao.
© UNHCR/Sanne Biesmans
Angela N'Habimana mwenye umri wa miaka 67 akiwa na mjukuu wake aitwaye Réponse kwenye kituo cha kijamii cha Kiwanja katika eneo la Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC baada ya kukimbia mashambulizi kwenye makazi yao.

OCHA DRC yatiwa hofu na ghasia Maï-Ndombe na Kwilu

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Bruno Lemarquis ametoa wito kwa kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kusitisha ongezeko la mapigano ya kikabila kwenye majimbo ya Maï-Ndombe na Kwilu nchini humo sambamba na kuchukua hatua za kibinadamu.

Taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshasa inasema mapigano baina ya jamii yameongezeka tangu mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu kwenye jimbo la Maï-Ndombe na sasa yamesambaa hadi jimbo jirani la Kwilu.

Zaidi ya watu 35,000 wamekimbia makazi yao kwenye majimbo hayo na kukimbilia majimbo ya jirani ya Kwango na Kishansa, imesema taarifa hiyo ikinukuu mamlaka za majimbo hayo mawili.

Kama hiyo haitoshi, zaidi ya watu 1,400 wamevuka mto Congo na kusaka hifadhi kwenye nchi jirani ya Jamhuri ya Congo huku ikiripotiwa kuwa ghasia hizo zimesababisha vifo vya watu kadhaa na nyumba pia zimechowa moto.

Hofu ya watoa misaada ya kibinadamu juu ya ghasia Maï-Ndombe

Bwana Lemarquis amesema watoa huduma za misaada ya kibinamu wana hofu juu ya kuendelea kwa ghasia, ambazo sasa pia zinaathiri majimbo mengine. Idadi kubwa ya watu wamelazimika kuhama na sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu. 

Ametaka uhamasishaji wa mamlaka na watoa misaada ya kibinadamu, amani na maendeleo kuchukua hatua ambazo zinapunguza mvutano na kupunguza mateso ya wale walioathirika na vurugu hizo.

Halikadhalika amesema « uelewa mzuri wa sababu za msingi za mgogoro pia utawezesha kutafuta suluhisho la kudumu na kuanzishwa au kuunga mkono mifumo rasmi na isiyo rasmi ya utatuzi wa migogoro."

Hadi sasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ina zaidi ya watu milioni 5 waliokimbia makazi yao ambapo migogoro ya ardhi, mapigano ya kikabila ni miongoni mwa sababu kuu za watu kukimbia makazi yao.