Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TAS- Tanzania yaelimisha wanafunzi kuhusu utangamano na watu wenye ualbino

Nchini Tanzania, chama cha watu wenye ualbino, TAS kinaendesha programu za kuelimisha watu kuhusu haki za watu wenye ualbino. Pichani ni mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania, mafunzo yakiendelea kwa wanafunzi.
UN News
Nchini Tanzania, chama cha watu wenye ualbino, TAS kinaendesha programu za kuelimisha watu kuhusu haki za watu wenye ualbino. Pichani ni mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania, mafunzo yakiendelea kwa wanafunzi.

TAS- Tanzania yaelimisha wanafunzi kuhusu utangamano na watu wenye ualbino

Haki za binadamu

Nchini Tanzania, chama cha watu wenye ualbino Tanzania (TAS) kwenye mkoa wa Morogoro kimeendelea kutekeleza programu ya kuelimisha shuleni juu ya haki za watu wenye ualbino kama njia mojawapo ya kulinda kundi hilo, halikadhalika kuimarisha utangamano nao kwenye jamii.

Katika tukio la hivi karibuni zaidi, TAS mkoani Morogoro ilitembelea shule ya msingi ya Kilakala iliyoko Manispaa ya Morogoro ambako walizungumza na wanafunzi wa darasa la 6 na la 7 na kuzungumza nao jinsi ya kuishi nao katika jamii.

Akifafanua kile walichofanya, mmoja wa wawezeshaji wa programu hiyo kutoka TAS Julia Kayombo amesema kwanza waliwaeleza wanafunzi hao malengo la Chama cha watu wenye ualbino Tanzania na zaidi ya yote,  “tumewagusia watoto changamoto anazokutana nazo mtu mwenye ualbino, jinsi ya kuzitatua, vilevile tumeelimisha jinsi ya wao kutoa elimu kwa Jamii zao jinsi ya kuwalinda watu wenye ualbino, kutowatenga na zaidi.”

Julia Kayombo pia alielezea sababu za wao kuanza kutoa elimu kwa watoto walio katika shule za msingi na sekondari akisema, tuna imani wao watakapopata elimu hii, wataenda kuwaelimisha na wengine hii inaweza kuleta uelewa zaidi kwa Jamii hasa kwa watoto wenyewe kwa wenyewe wakikutana wanaweza kuongea.”

Nao baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi kilakala waliopatiwa elimu ya Ualbino, walisema wameipokea vyema na kuahidi kuifanyia kazi katika maisha yao ya kila siku.

Miongoni mwao ni Sophia Mtinda, mwanafunzi wa darasa la 6 ambaye amesema “nimejifunza kutowatenga watu wenye ualbino, na pia elimu hii niliyoipata nitawaelimisha pia watu waliokuwa wanawadharau watu wenye ualbino”

Mwanafunzi mwingine ni Martini Patrick wa darasa la 6 alisema ‘’mambo ambayo mtoto mwenye ualbino anapaswa kufanya ni kuvaa nguo ndefu, kuvaa kofia ili kujikinga na jua kali”