Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msifurishe dunia hii leo, wala msiizamishe kesho- Ujumbe wa Katibu Mkuu wa viongozi wa dunia

Waathirika wa mafuriko kwenye eneo la Balochistan, nchini Pakistani.
WFP Pakistan
Waathirika wa mafuriko kwenye eneo la Balochistan, nchini Pakistani.

Msifurishe dunia hii leo, wala msiizamishe kesho- Ujumbe wa Katibu Mkuu wa viongozi wa dunia

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo ikiwa ni kuelekea Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la UN unaoanza wiki ijayo akisema ujumbe wake mkuu kwa viongozi watakaoshiriki ni dhahiri ya kwamba wachukue hatua kupunguza kiwango cha joto duniani.

Guterres amesema atawaeleza kuwa “msifurishe dunia leo, msiizamishe kesho,” kwa kutambua kuwa mkutano huu wa Baraza Kuu unafanyika zama za sasa zinazokabiliwa na tishio kubwa.

Ametaja tishio hilo kuwa ni pamoja na mgawanyiko mkubwa wa kijiografia na kimkakati, mgawanyiko aliosema ni mkubwa kuwahi kutokea tangu zama za vita baridi.

“Mgawanyiko huu unakwamisha hatua za pamoja za kukabiliana na changamoto zinazotukabili. Dunia imekumbwa na vita, changamoto za tabianchi, chuki zimezaga, na aibu kubwa inakabili dunia kutokana na umaskini, njaa na ukosefu wa usawa,” amesema Guterres.

Akifafanua kuhusu tabianchi amerejelea kile alichoshuhudia wakati wa ziara yake ya kuonesha mshikamano na Pakistani ambayo imekumbwa na mafuriko makubwa.

Kambi ya wakimbizi wa ndani ya Horseed ambayo ni moja ya maeneo yaliyoathirika vibaya na ukame Somalia
WFP/Geneva Costopulos
Kambi ya wakimbizi wa ndani ya Horseed ambayo ni moja ya maeneo yaliyoathirika vibaya na ukame Somalia

Theluthi moja ya G20 ingalikuwa imefurika, pengine wangepunguza uchafuzi

Katibu Mkuu amesema, “kinachotokea Pakistan, kinadhihirisha kutotosheleza kwa hatua za kimataifa dhidi ya janga la tabianchi ambavyo kitovu chake ni ukosefu wa haki na usaliti.”

Hata hivyo amesema iwe ni Pakistan, Pembe ya Afrika au Sahel, nchi za visiwa vidogo au zinazoendelea, suala ni kwamba nchi zilizo hatarini zaidi ambazo hazijasababisha janga la tabianchi ndio zinaathirika na janga lililochochewa na wachafuzi wakuu wambao ni kutoka nchi za kundi la nchi 20 au G20.

“Iwapo theluthi moja ya kundi la G20 ingalikuwa imezama au imefunikwa kw amaji leo hii, kama ambavyo inaweza kuwa kesho, pengine wangaliona rahisi kupunguza viwango vya utoaji wa hewa chafuzi,” amesema Guterres.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari New York, Marekani
UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari New York, Marekani

G20 ziongoze njia kwa kuongeza viwango vya kitaifa vya kupunguza utoaji hewa chafuzi

Hivyo amesema nchi zote, zile za G20 zikiongoza njia, lazima ziongeze viwango vya kitaifa vya kupunguza utoaji wa hewa chafuzi hadi pale kiwango kinachotakiwa cha nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kitakapofikiwa.

Amepatia msisitizo suala la uwekezaji katika miradi ya kuhimili na kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi akisema, hatua zisipochukuliwa sasa, fedha zisipotolewa sasa, majanga yataongezeka maradufu, huku madhara yake yakidumu miaka na miaka ijayo, ikiwemo kuongeza ukosefu wa utulivu na kuchochea uhamiaji duniani kote.

 

Ubinafsi na Uzawa vyateketeza mshikamano uliomo kwenye Chata ya UN

Bwana Guterres amesema changamoto lukuki zinazokumba Dunia hivi sasa ni matokeo ya ubinafsi na uzawa, mambo ambayo amesema yanateketeza mshikamano ulioainishwa kwenye Chata ya Umoja wa Mataifa.

Mshikamano wa kwenye Chata ya UN unararuliwa na ubinafsi na uzawa na wanaofanya hivyo ni wanasiasa ambao wanatumia mazingira duni ya maskini ili kujunifaisha kisiasa. António Guterres, Katibu Mkuu - UN

Nchini Ukraine vita inasambaratisha nchi huku ikidororesha uchumi wa dunia.

Licha ya Makubaliano ya kusafirisha nafaka kupitia baharí nyeusi, na makubaliano ya kupeleka soko la dunia chakula na mbolea kutoka Urusi, bado kuna hatari ya matukio ya uhaba wa chakula duniani mwaka huu.

Gharama za maisha zinapanda na kufikia viwango vya juu, waathirika zaidi wakiwa watu maskini.

Haki za wanawake na watoto wa kike ndio zinazidi kusiginwa.

Nchi nyingi zinazoendelea hazina uwezo wa kifedha unaotakiwa kujikwamua baada ya janga la coronavirus">COVID-19.

Watoto wa jamii ya warohingya wakicheza kwenye mvua katika kambi ya wakimbizi ya Nayapara huko Teknaf, Mashariki mwa Bangladesh
© UNHCR/Amos Halder
Watoto wa jamii ya warohingya wakicheza kwenye mvua katika kambi ya wakimbizi ya Nayapara huko Teknaf, Mashariki mwa Bangladesh

Wanasiasa wanajinufaisha na umaskini wa wananchi

Mshikamano wa kwenye Chata ya UN unararuliwa na ubinafsi na uzawa,” amesema Katibu Mkuu akisema wanaofanya hivyo ni wanasiasa ambao wanatumia mazingira duni ya maskini ili kujunifaisha kisiasa.

Guterres amesema hotuba yake itamulika masuala hayo sambamba na kuwasilisha mapendekezo kwani “kadri ufa unavyozidi kupanuka na imani inatoweka, lazima tuungane kuleta majawabu.”

Amesema majawabu hayo ni kama yake yatakayotolewa wakati wa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Marekebisho ya Mfumo wa Elimu.

Katibu Mkuu amesema watu wanataka kuona matokeo kwenye maisha yao ya kila siku la sivyo watapoteza imani na serikali na taasisi zao na kisha watapoteza pia imani na mustakhbali wao.

Amesema Mjadala Mkuu wa mwaka huu lazima ulete matumaini na matumaini hayo yanaweza kupatikana kupitia mazungumzo yanayogusa moyo wa Umoja wa Mataifa na lazima ifanyike hivyo wiki ijayo ili kukabili migawanyiko yote.