Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sam Aderubo anayeleta 'utamu' kwa jamii yake kaskazini mwa Uganda 

Mmiliki wa Honey Pride, Sam Aderubo na mfugaji wa nyuki Betty Ayikoru
UN News/ Hisae Kawamori
Mmiliki wa Honey Pride, Sam Aderubo na mfugaji wa nyuki Betty Ayikoru

Sam Aderubo anayeleta 'utamu' kwa jamii yake kaskazini mwa Uganda 

Ukuaji wa Kiuchumi

Sam Aderubo alianzisha kampuni yake, Honey Pride, huko Arua, kaskazini mwa Uganda, ili kuleta matokeo chanya kwa jamii yake. Kwa msaada kutoka kwa Umoja wa Mataifa, biashara inashamiri, ikitoa kazi kwa mamia ya wafugaji nyuki wa ndani, ambao wengi wao ni wanawake na vijana waliotengwa. 

"Nilikuwa nikifanya kazi katika ofisi, na watu walikuwa wanakuja mahali pangu pa kazi kuuza 'asali ya West Nile', iliyopewa jina la mkoa ninaotoka. Nilivutiwa kuona kuwa eneo langu lilikuwa linatumika kama chapa ya biashara na kugundua kuwa West Nile ni mojawapo ya mikoa ya juu iliyoorodheshwa nchini Uganda kwa uzalishaji wa asali. Kwa hiyo, niliamua kwamba nitarudi nyumbani, na kuanzisha kampuni ya kuhudumia jumii yangu.” Anasema Sam Aderubo anapoanza kutoa maelezo kuhusu biashara hii ya asali. 

Sam Aderobu, mwanzilishi wa Honey Pride
UN News/ Hisae Kawamori
Sam Aderobu, mwanzilishi wa Honey Pride

Bidhaa inayohitajika 

Bidhaa hiyo inahitajika, ndani na nje ya nchi, na ina sifa chanya za dawa na chakula. Tuligundua kuwa kuna uwezo mkubwa wa kuizalisha kwa kiwango kikubwa. 

Hata hivyo, watu wengi katika mkoa huu wanakusanya asali tu kwa njia ya kitamaduni, kama mapenzi yao tu kwa asali. Tuliamua kuwapa wakulima mwongozo, na kuwapa ujuzi unaohitajika kwa sababu hapo awali, walikuwa wakifanya kazi bila msaada wowote rasmi; hakuna aliyekuwa tayari kuwekeza katika kuwasaidia ili kuboresha ubora wa asali yao. 

Leo, tunafanya kazi na zaidi ya wakulima 1,700, ambao huvuna asali kutoka kwa nyuki kwenye ardhi yao. Tunatoa soko la uhakika kwao, ambalo linawahimiza kuzalisha zaidi. 

Mfugaji wa nyuki Betty Ayikoru, Arua, kaskazini mwa Uganda
UN News/ Hisae Kawamori
Mfugaji wa nyuki Betty Ayikoru, Arua, kaskazini mwa Uganda

Uchumi, mazingira na jamii 

Tunaamini kwamba ufugaji nyuki ukichukuliwa hadi kufikia kiwango ambacho wakulima wanauelewa kama biashara, utaboresha maisha yao; tulipoanza biashara mwaka 2015, kilo moja ya asali iliuzwa kwa takriban Shilingi 3,500 za Uganda. Leo ni takriban Shilingi 7,000. Hii imewapa motisha wakulima wengi kuingia katika ufugaji nyuki. 

Sasa wanaweza kumudu mahitaji ya msingi, na Shawana wasiwasi kuhusu njaa. Wanaweza kununua mbuzi na wanyama wengine na kulipa ada ya shule ya watoto wao. Wengine wameweza hata kupata nyumba. Ufugaji nyuki unabadilisha maisha yao. 

Maono yetu yalikuwa kuwa waongozaji katika soko la uuzaji wa bidhaa za mizinga endelevu katika eneo la Maziwa Makuu, na kuuza kimataifa. Bidhaa zetu sasa zinakidhi viwango vya kimataifa na zinakubalika katika masoko ya nje. 

Tunajaribu kuunda timu ya usimamizi iliyo na moyo wa kazi, na wengi wao ni vijana. Tunapata usaidizi kutoka kwa programu inayoendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), programu ambayo inashughulikia mtazamo wa vijana kuhusu kilimo, na jinsi wanavyoweza kuhamasishwa kukumbatia kilimo kama chanzo cha ajira. 

Vijana tunaoshirikiana nao, wameanza kujitambua kuwa wana mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa. Kwa hivyo, wakati tunataka kupata faida, pia tuna kipengele cha kijamii kwa kile tunachofanya. 

Mfugaji wa nyuki Betty Ayikoru na familia yake katika makazi yake huko Arua, kaskazini mwa Uganda.
UN News/ Hisae Kawamori
Mfugaji wa nyuki Betty Ayikoru na familia yake katika makazi yake huko Arua, kaskazini mwa Uganda.

Kuzishinda changamoto za kifedha 

Fedha imekuwa moja ya changamoto zetu kubwa. Kwa sababu ya ukosefu wa fedha, shughuli nyingi za kutengeneza asali zimefanywa kwa mikono. Hata hivyo, shirika la Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), umetuwezesha kupata ufadhili kutoka kwa Benki ya Maendeleo ya Uganda, na kuboresha sehemu ya mchakato wetu wa uzalishaji. 

Sasa tunatumia mashine ya umeme ya kukamua asali na tuliweza kupata mashine ya kuchuja ili kuboresha ubora wa bidhaa zetu. Tunaweza kusindika takriban tani tano za asali kwa mwezi, ambalo ni ongezeko kubwa, na nina hakika kwamba tutaweza kukuza hiyo hadi takriban tani 15. 

“Tunashukuru sana kwa usaidizi tuliopokea kutoka kwa UNCDF, kwa sababu ulitusaidia pia kuboresha usimamizi wa biashara yetu, kuongeza uzalishaji, na kuboresha ubora wa bidhaa zetu.” Anahitimisha Aderubo.