Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake wametuokoa na ukame Turkana

Ukame wa mara kwa mara na ushindani unaotokana na rasilimali umesababisha mzozo nchini Somalia katika miongo ya hivi karibuni.
undp Somalia
Ukame wa mara kwa mara na ushindani unaotokana na rasilimali umesababisha mzozo nchini Somalia katika miongo ya hivi karibuni.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake wametuokoa na ukame Turkana

Tabianchi na mazingira

Eneo la Katilu limenawiri na mimea imechipua. Wakulima wanasubiri kuvuna na kula matunda ya jasho lao.Turkana kusini inakabiliana na ukame kwa kuchimba na kutumia maji ya kisima kwa kilimo na matumizi.

Ukame umeiathiri kaunti ya Turkana kwa jumla lakini kijiji cha Kanyerega kimejizatiti. James Emase ni mkaazi wa Kanyerega na mkulima alienufaika na mradi na anasema,"maisha yangu yameimarika kwa sasa kwani sinunui tena chakula.Watoto wangu walikuwa wanahangaika lakini kwa sasa afya yao iko sawa.Kila tunachovuna tunakula na kikisalia tunauza sokoni ili kupata hela mkononi.”

Ili kupambana na njaa na utapia mlo,mashirika ya msaada ya Africare na Bayer Fund kwa ushirikiano na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na mpango wa Chakula WFP walikuja pamoja kufadhili mradi huu.Mashirika hayo ya Umoja wa mataifa yanawapa wakaazi elimu ya kilimo cha kisasa, mbinu za kukabiliana na utapia mlo hasa kwa watoto kwa kuzingatia lishe bora pamoja na nyenzo.

Mitambo ya sola

Maji ya kisima yanahifadhiwa kwenye matangi makubwa ili wakaazi waweze kufanya kilimo cha kumwagilia.Matumizi ya nishati ya jua yamefanikisha mahitaji ya umeme na kuyasukuma maji hadi mashambani.Kilimo kinachotumia mbegu za kisasa zilizorutubishwa na mbolea vimeleta tija kwa wakaazi wa Turkana kusini waliokuwa wanatatizwa na makali ya njaa.James Emase mkaazi wa Kanyerega anakiri kuwa,"Ukame na njaa vipo Turkana lakini sisi tuna maji yetu kwahiyo tunapambana navyo ana kwa ana.Tunatumia maji haya kwa kilimo na pia mifugo inayanywa. Hata kwa wanakijiji wasiokuwa wakaazi wa hapa pia wana uhuru wa kuwaleta wanyama wao kunywa maji.”

Ukame mkali unaua mifugo katika jamii ya wafugaji Higlo Kebele nchini Ethiopia.
© WFP/Michael Tewelde
Ukame mkali unaua mifugo katika jamii ya wafugaji Higlo Kebele nchini Ethiopia.

Katika eneo la Turkana ya kati na Loima wakaazi pia wamenufaika na mradi wa maji ya kisima.Mradi huo ulifanyika kwa ufadhili wa shirika la watoto la Umoja wa mataifa, UNICEF, na lile la msaada wa maendeleo la Korea,KOICA. Dhamira ya mradi huo ni kuchimba visima 76 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2022.Kufikia asilimia 90 ya visima hivyo vimechimbwa kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Turkana.Watoto walikuwa wanatembea mwendo mrefu hadi eneo la Kawalase kuteka maji lakini sasa mambo yamebadilika na maisha yameimarika.

Wanyama nao waliokuwa wanadhoofika kwasababu ya uhaba wa maji sasa afya yao imekuwa nzuri kwani wana maji.Lucas Eyipa ni mkaazi wa Lokoyo na msimamizi wa kisima cha eneo hilo na anaelezea jinsi maisha yao yalivyobadilika,"Watoto walikuwa wanaenda mbali sana kuteka maji kwenye eneo la Kawalase.Kwa sasa mambo ni mazuri kwani maji yako karibu na hawapotezi muda kusaka maji.UNICEF na serikali ya kaunti ya Turkana walikuja pamoja na kutuchimbia kisima ambacho kinatufaa sisi zote.”

Ukame na uhaba wa mvua

Mabadiliko ya tabia ya nchi yamesababisha maeneo mengi ya Turkana kukosa mvua za msimu kwa kipindi kirefu.Maji yaliyoko ya chemchemi ndiyo yanayotumika kwa mahitaji ya wanyama na wanadamu jambo linalohatarisha maisha ya wakaazi kama anavyosimulia Elijah Emusekidor, mwakilishi wa kijiji eneo la Lorus akisema, "tunatumia maji ya chemchemi kwani ndiyo yaliyoko na hayakauki.Tatizo ni kuwa binadamu na wanyama wanayatumia na kuuongeza uwezekano wa magonjwa kusambaa.”

Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.
UNDP/Ngele Ali
Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.

UNEA na mabadiliko ya tabia ya nchi

Kulingana na wataalam wa mazingira, mabadiliko ya tabia ya nchi yanasababishwa na gesi za viwanda ambazo zina madhara kwenye mfumo wa uhai.Kwenye kikao chake cha 5 cha baraza kuu la shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEA,wajumbe walipitisha azimio la kutambua uhusiano kati ya ufugaji, kilimo cha kisasa na athari zake kwenye mazingira ukijumuisha mabadiliko ya tabia ya nchi.Dr Victor Yamo wa shirika la kuetetea haki za wanyama la Animal Welfare Protection anafafanua kuwa,"mbinu za kitamaduni za ufugaji na kilimo zina manufaa kwenye mazingira na mfumo mzima wa uhai.Kilimo na ufugaji wa kisasa unachangia katika ongezeko la gesi za viwanda ambazo zinaaminika kuwa na mkono kwenye mabadiliko ya tabia ya nchi.UNEA sasa ilipitisha azimio linalotambua uhusiano kati ya mfumo wa uhai, kilimo na ufugaji wa kisasa na mazingira.”

Ili kuhimili athari za mabadiliko ya tabia ya nchi ipo haja ya kuelewa uhusiano katika mfumo mzima wa uhai.