Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampuni za maziwa ya watoto zatumia mitandao ya kijamii kurubuni wazazi

Sekta ya maziwa ya watoto ya viwandani hutumia mabilioni ya fedha kila mwaka kushawishi uamuzi wa wazazi juu ya kile ambacho watamlisha mtoto wao
WHO/UNICEF
Sekta ya maziwa ya watoto ya viwandani hutumia mabilioni ya fedha kila mwaka kushawishi uamuzi wa wazazi juu ya kile ambacho watamlisha mtoto wao

Kampuni za maziwa ya watoto zatumia mitandao ya kijamii kurubuni wazazi

Afya

Kampuni zinazotengeneza maziwa ya watoto ya unga zinalipa majukwaa ya mitandao ya kijamii na watu wenye ushawiwishi ili kuweza kuwafikia wajawazito na akina mama kama mbinu mojawapo ya kuuza bidhaa zao, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO hii leo, likiongeza kuwa harakati hizo zinafikisha ujumbe kwa wanawake wao katika kipindi chenye changamoto zaidi kwenye maisha yao.

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi inasema kuwa sekta hiyo ya utengenezaji wa maziwa ya watoto ina thamani ya dola bilioni 55 na sasa inatumia mbinu za masoko mtandaoni za kumlenga mama mzazi na ujumbe mahsusi kwake yeye binafsi, mbinu ambayo inatambuliwa kuwa ni matangazo ya biashara.

Tweet URL

Taarifa zinakusanywa kisiri na kuibuka na matangazo ya kumleta mtu mmoja

Taarifa hiyo imenukuu ripoti mpya ya WHO iliyopatiwa jina Kiwango na Athari za mbinu za masoko za kidijitali za kutangaza maziwa mbadala ya mama, ripoti ambayo inachambua kwa kina mbinu za masoko mtandaoni zilizobuniwa kushawishi familia changa zenye watoto juu ya jinsi ya kulisha watoto wao wachanga.

Kupitia mbinu kama vile matumizi ya apu mahsusi, vikundi vya mtandaoni vya kusaidia malezi au lishe ya watoto, malipo kwa watu wenye ushawishi mtandaoni, matangazo na mashindano, na majukuwaa ya ushauri au huduma, kampuni za kutengeneza maziwa ya watoto zinaweza kununua taarifa za mtu na kuzitumia kuandaa ujumbe mahsusi unaolenga mjamzito au mama mzazi mwenye mtoto mchanga.

Ripoti imeweka muhtasari wa matokeo ya utafiti mpya wa taarifa milioni 4 kutoka mitandao ya kijamii kuhusu ulishaji wa watoto wachanga, taarifa zilizokusanywa kati ya mwezi Januari hadi mwezi Juni mwaka jana wa 2021.

Kampeni za maziwa ya kopo zafikia watu mara 3 zaidi kuliko kampeni za  maziwa ya mama

Taarifa hizo za mtandaoni zilifikia watu bilioni 2.47 na kupendwa, kusambazwa au kupatiwa maoni mara milioni 12.

Kampuni za maziwa hayo ya watoto ya viwandani hurusha mara 90 kwa siku katika akaunti zao za mitandaoni taarifa mbalimbali zinazofikia watumiaji milioni 229, idadi ambayo ni mara tatu zaidi ya watu wanaofikiwa na taarifa kuhusu unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama, taarifa zinazotoka katika akaunti zisizo za kibiashara.

Lucy Atokoru, 28 ananyonyesha mtoto wake nyumbani kwake Omugo, Wilaya ya Arua.
© UNICEF/Zahara Abdul
Lucy Atokoru, 28 ananyonyesha mtoto wake nyumbani kwake Omugo, Wilaya ya Arua.

WHO inasema mbinu hii ya biashara inasababisha ongezeko la maziwa ya watoto ya viwandani na hivyo kuondoa ushawishi wa mama kumnyonyesha mtoot wake kama inavyopendekezwa na WHO.

Mkurugenzi wa lishe WHO, Dkt. Francesco Branca, amesema suala kwamba kampuni za kutengeneza maziwa ya watoto ya viwandani hivi sasa  zinatumia mbinu za kisiri na thabiti za masoko na matangazo kuongeza mauzo yake ni jambo lisilosameheka na lazima likome.

WHO imetaka sekta ya vyakula vya watoto iache mbinu za kinyonyaji kwenye soko la maziwa ya watoto wa viwandani na imetaka seriklai zilinde watoto wachanga na familia changa kwa kutunga, kufuatilia na kusimamia sheria ili kutokomeza matangazo ya maziwa ya watoto ya viwandani.